Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akioneshwa mfano wa nyamera na Waziri wa
Maliasili na Utalii, Khamis Kigwangala, kwenye ofisi ya Wizara hiyo,
wakati akikagua ofisi za Wizara katika mji wa Serikali eneo la Mtumba,
jijini Dodoma, Aprili 23, 2019.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akiongea na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
(TAMISEMI), Suleiman Jaffo, kwenye ofisi ya Wizara hiyo ya muda, wakati
akikagua ofisi za Wizara kwenye mji wa Serikali eneo la Mtumba, jijini
Dodoma, Aprili 23, 2019.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akioneshwa jambo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
(TAMISEMI), Suleiman Jaffo, wakati akikagua ofisi za Wizara kwenye mji
wa Serikali eneo la Mtumba, jijini Dodoma, Aprili 23, 2019.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akitoka kwenye jengo la Ofisi ya Waziri Mkuu,
Sera, Uratibu na Bunge, wakati akikagua ofisi za Wizara kwenye mji wa
Serikali eneo la Mtumba, jijini Dodoma, Aprili 23, 2019.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akisalimiana na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa, Hussein Mwinyi, wakati akikagua ofisi za Wizara kwenye
mji wa Serikali eneo la Mtumba, jijini Dodoma, Aprili 23, 2019. (Picha
na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekagua ofisi mpya za wizara saba katika mji wa
Serikali ulioko Mtumba, Dodoma na kusisitiza waweke vibao vya ofisi na
kukamilisha mazingira ya nje.
“Kuna
wizara hazina majina kwa nje. Hakikisheni majengo yote yanawekwa majina
haraka ili kuondoa usumbufu kwa wananchi wanaokuja huku kutafuta
huduma. Kama kuna wizara mbili ziko jirani, pale njia panda wekeni kibao
kuonesha majina ya wizara zote mbili. Nia ya Serikaili ni kutoa huduma
zote kutokea hapa Mtumba,” amesema.
Ametoa
agizo hilo leo jioni (Jumanne, Aprili 23, 2019) wakati akitoa
majumuisho ya ziara hiyo fupi kwa maafisa wa Serikali waliokuwepo kwenye
ukumbi wa mikutano wa wizara ya nishati ambako ndiko alimalizia ziara
yake.
Waziri
Mkuu ametembelea wizara saba ambazo ni Maliasili na Utalii; Ofisi ya
Rais - TAMISEMI; OWM - Sera, Uratibu na Bunge; Ofisi ya Rais – Utumishi
na Utawala Bora; Mifugo na Uvuvi, Ulinzi na JKT na ya mwisho ilikuwani
ni Wizara ya Nishati.
“Nimefurahi
kukuta Mawaziri, Naibu wao na Makatibu Wakuu pamoja na wakuu wa idara
wako huku na kazi zinaendelea, lakini ni lazima nisisitize kwamba idara
zinazohamia huku ziwe ni zile zenye kutoa huduma za kila siku kwa
wananchi,” amesema.
“Ni
lazima tuwaeleze wananchi na wadau wetu ili watambue kwamba Serikali
imehamia huku, lakini wakija kutaka huduma wasikute idara inayowahusu
iko mjini au wengine wako huku na wengune wako kule.”
Kuhusu
miundombinu ya barabara, umeme na TEHAMA, Waziri Mkuu amesema Kamati ya
Kitaifa ya kuratibu zoezi la Serikali kuhamia Dodoma inasimamia kazi
hiyo ikiwemo suala la ujenzi wa kituo kikubwa cha afya ambacho kitakuwa
na huduma zote kwa viongozi lakini pia pia kitatoa huduma kwa wananchi
waishio vijiji vya jirani.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka mawaziri walioko Mtumba wajiandae
kwani kuna siku atakwenda kufanya vikao vyake kwenye wizara zao kwa
sababu amebaini kuwa kila wizara ina ukumbi mkubwa wa mikutano.
Mapema,
akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk.
Hamisi Kigwangalla alisema jumla ya watumishi 64 wameshamia kwenye ofisi
za wizara hiyo ambapo kuna vyumba 25 vya ofisi na ukumbi mmoja wa
mikutano. Pia alisema waligawa miche ya miti 13,570 kwa wizara
mbalimbali na kwamba katika ofisi yake, wamepanda miti 980.
Kwa
upande wake, Waziri wa Nchi (OR-TAMISEMI), Bw. Suleiman Jafo alisema
wamekwishahamia tangu Jumatatu iliyopita na kwa sasa wanatumia ofisi za
muda ambazo ni za mabati huku wakisimamia ujenzi wa ghorofa yao hadi
ukamilike.
Akielezea
kuhusu ujenzi wa ofisi hizo ulipofikia, Bw. Jafo alisema ifikapo
mwishoni mwa wiki watakuwa wamekamilisha kazi ya kuweka mabati na kupiga
plaster. “Tunatarajia kukamilisha kazi ya ujenzi Mei 30, kama
ilivyopangwa. Jengo lilikamilika litakuwa na kumbi mbili za mikutano na
ofisi za kuchukua watumishi 88,” alisema.
Naye
Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani alisema kuwa hadi sasa watumishi
73 kati ya 153 ndiyo wamehamia kwenye ofisi mpya za Mtumba. Alisema kwa
sasa wanatenegeza eneo la maegesho ya magari na wameshatenga eneo la
mgahawa kwa ajili ya wafanyakazi wa wizara hiyo.
No comments:
Post a Comment