Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametembelea kambi ya timu ya Taifa ya
vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 na kuwaeleza kuwa Watanzania
wanamatumaini makubwa dhidi yao, hivyo waongeze bidii.
Alitembelea kambi hiyo Serengeti Boys iliyoko katika jiji la Kigali
nchini Rwanda. Waziri Mkuu alikwenda Rwanda Aprili 7, 2019
kumuwakilisha Rais Dkt. John Magufuli kwenye kumbukumbu za miaka 25 ya
mauaji ya Kimbari.
Akizungumza na wachezaji hao jana, Waziri
Mkuu aliwataka vijana wanaounda timu hiyo ya Serengeti Boys
wahakikishe wanafanya mazoezi ya kutosha ili waweze kushinda mechi
zinazofuata.
“Watanzania wanamatumaini makubwa dhidi yenu nasi tunazidi kuwaombea
kwa Mwenyezi Mungu muweze kuibuka na ushindi katika michezo yenu
iliyobakia itakayowawezesha kushiriki mashindano ya kombe la dunia.”
Kadhalika, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuipongeza timu hiyo ya
Serengeti Boys kwa namna wanavyoitangaza nchi kimataifa kupitia kwenye
mashindano mbalimbali wanayoshiriki na kuibuka na ushindi.
Waziri Mkuu alisema endapo timu hiyo ya Taifa ya vijana ya Serengeti
Boys itaibuka na ushindi katika michezo yake miwili itakuwa imekata
tiketi ya kushiriki mashindano ya dunia huko nchini Brazil kwa vijana
wa umri wa miaka 17.
Kwa upande wao, wachezaji na uongozi wa timu ya Serengeti Boys
walimkabidhi Waziri Mkuu kombe walilolipata baada ya kuichapa timu ya
Rwanda katika mashindano maalumu kwa ajili ya kujiandaa na AFCON-U17.
Mashindano hayo maalumu ya Kimataifa yalishirikisha timu za umri wa
chini ya miaka 17 kutoka nchi tatu ambazo ni Tanzania, Cameroon na
wenyeji Rwanda, ambapo Serengeti Boys ilishinda mabao mawili kwa moja
dhidi ya Cameroon na kutoka sare ya mabao matatu kwa matatu na Rwanda.
Pia, wachezaji hao wamemuahidi Waziri Mkuu kwamba watajitahidi kadiri
ya uwezo wao kuhakikisha wanaibuka na ushidi katika mechi zilizobakia
ili waweze kushiriki kombe la dunia. “Hatutawaangusha Watanzania.”
Awali, Waziri Mkuu alimshukuru Balozi wa Tanzania nchini Rwanda,
Mheshimiwa Balozi Ernest Mangu pamoja na maofisa wa ubalozi na
Watanzania waishio Rwanda kwa kuendelea kuipa moyo Serengeti Boys.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akikabidhiwa kombe kutoka Nahodha wa timu ya
Serengeti Boys, Morice Michael katika ofisi ya ubalozi wa Tanzania
nchini Rwanda, April 7,2019, kufuatia timu hiyo kuibika bingwa katika
mashindano maalum kimataifa yaliyofanyika nchini humo. Mashindano hayo
yalishirikisha timu za umri wa chini ya miaka 17 kutoka nchi tatu ambazo
ni Tanzania, Cameroon na wenyeji Rwanda. Wanaoshangilia kushoto ni
Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Ernest Mangu na Mkurugenzi wa Ufundi
wa timu ya Serengeti Boys, Khalid Abdallh.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Cherie Blair
ambaye ni Mke wa Waziri Mkuu wa Zamani wa Uingereza, Tony Blair
walipokutana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kigali nchini
Rwanda April 8, 2019. Majaliwa na Cherie walikuwa wakitoka kuhudhuria
hafla ya kumbukumbu ya miaka 25 ya mauaji ya kimbari nchini humo
iliyofanyika April 7, 2019. Katikati ni Balozi wa Tanzania nchini
Rwanda, Ernest Mangu.
Waziri
Mkuu akiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Serengeti Boys .katika
Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania. Kigali Rwanda April 7, 2019. PICHA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
No comments:
Post a Comment