Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Wazee
Waasisi wa Zanzibar wataendelea kuwa ngao ya Taifa ambayo Viongozi wa
sasa pamoja na Wananchi na Kizazi Kipya wana wajibu wa kuwatunza
katika maisha yao ya kila siku.
Alisema ngao hiyo inatokana na kazi kubwa waliyoifanya wakati wa
harakati za kupigania Ukombozi wa Taifa hili ambapo kwa sasa Viongozi
waliopo madarakani pamoja na Wananchi wanaendelea kula matunda ya
Uhuru uliotokana na Wazee hao.
Balozi Seif alitoa kauli hiyo iliyowasilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi
ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed kwenye
Futari ya pamoja iliyoandaliwa kwa ajili ya Wazee wanaohifadhiwa
katika Nyumba za Serikali zilizopo Welezo Wilaya ya Magharibi “A”.
Alisema Kizazi cha sasa wakati kikiendelea kufaidika na matunda hayo
lakini kwa upande mengine wana wajibu wa kulinda na kuendeleza Uhuru
huo utakaokuwa kielelezo cha Heshima ya muda wote wa Wananchi wa
Visiwa vya Unguja na Pemba.
Mapema Mchana Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alikabidhi msaada wa Tangi la kuhifadhia Maji, Mashine yake pamoja na
Luva ya kusafishia Msikiti wa Ijumaa wa Umbuji uliopo Wilaya ya Kati
Mkoa Kusini Unguja.
Msaada huo unafuatia ahadi aliyoitoa wakati wa ufunguzi Rasmi wa
Msikiti huo alipomuwakilkisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein kwenye Ufunguzi wakeMiaka michache
iliyopita nyuma.
Akizungumza na Uongozi wa Msikiti huo Balozi Seif alisema ahadi ni
deni kitu ambacho alilazimika kukitekeleza ingawa kimechukuwa muda
mrefu kutokana na sababu mbali mbali yakiwemo majukumu yaliyotangulia
ya ahadi nyengine za awali.
Akipokea msaada huo kwa Niaba ya Uongozi wa Msikiti huo Sheha wa
Shehia ya Umbuji Bwana Muhamad Mrisho Juma alisema Waumini wa Dini ya
Kiislamu wa Kijiji cha Umbuji walilazimika kuwa na subra kutokana na
ahadi hiyo kutokana na kazi kubwa inayomkabili Balozi Seif ya
kulitumikia Taifa kila siku .
Sheha Mrisho alimuahidi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba
msaada huo muhimu kwao utatumika kwa lengo lililokusudiwa la kuombwa
kwake ili uendelee kutoa huduma katika kipindi kirefu kijacho.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
alikutana kwa mazungumzo na Ujumbe wa Viongozi Watatu wa Kampuni ya
Kimataifa ya Huduma za Afya na Uwekezaji kutoka Nchini Uturuki hapo
Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Katika mazungumzo yao Kiongozi wa Ujumbe huo Mkurugenzi Mkuu wa
Kampuni ya huduma za Afya na Uwekezaji {KAYI} Bwana Batur Engin
alimueleza balozi Seif kwamba Taasisi hiyo yenye Wafanyakazi 600
inatoa huduma katika Mataifa 200 Duniani.
Bwana Batur alisema Wahandisi wa Kampuni hiyo huendeleza kazi za
Miundombinu ya Ujenzi wa Hospitali kubwa za kisasa zenye vifaa vya
Teknolojia mpya unaofanywa katika mfumo wa ubia.
Alisema zipo Hospitali kubwa zilizojengwa katika Miji ya Paris Nchini
Ufaransa, Istambul Uturuki yenyewe pamoja na Hospiatli Kubwa zilizopo
Nchini Kenya zinazotarajiwa kukamilika Ujenzi wake hivi karibuni.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa Kampuni ya Kimataifa ya Huduma za Afya na
Uwekezaji alieleza pia Kampuni yake huendesha Miradi mengine ya
Miundombinu katika Sekta ya Mawasiliano kwa ujenzi wa Viwanja vya
Ndege, Bara bara Kubwa za Kisasa pamoja na Mahoteli Makubwa.
Alifahamisha kwamba mtazamo wa Kampuni yake kwa sasa umezingatia
kuwekeza katika Visiwa vya Zanzibar Miradi zitakayoweza kutoa huduma
katika Mwambao wa Afrika Mashariki pamoja na Ukanda Mzima wa Nchi za
Sahara.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari inaendeleza
Miradi mikubwa ya Ujenzi wa Hospitali ya Kisasa katika eneo la Binguni
pamoja na mpango wa Ujenzi wa Bandari ya Mizigo katika eneo la Mpiga
Duri.
Balozi Seif aliueleza Ujumbe wa Viongozi hao kutoka Uturuki kwamba
Kampuni yao ina fursa ya kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar katika uimarishaji wa Ujenzi wa Hospitali hiyo inayotarajiwa
pia kuwa na Kitengo cha Mafunzo ya Afya.
“ Inapendeza kuona Ujenzi wa Hospitali Kubwa ya Binguni inafanana na
mtazamo wa Kampuni hiyo katika uimarishaji wa Miradi yake katika
Huduma za Afya na Uwekezaji Vitega Uchumi”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba Serikali hivi
sasa ina mtazamo wa uwepo wa Hospitali ya Kimataifa itakayolenga kutoa
huduma kwa Watalii pamoja na wageni wanaoingia Nchini kwa safari za
kimatembezi.
Balozi Seif alisema mtazamo huo umekuja kutokana na Zanzibar kwa sasa
kuimarika katika Sekta ya Utalii inayoweza kuchukuwa nafasi ya kwanza
ya Uchumi wake.
Alisema kuimarika kwa huduma za Afya katika Sekta ya Utalii kutaipa
hadhi Zanzibar kurejea katika hadhi yake ya kutoa huduma mbali mbali
za kibiashara ndani ya Bahari ya Hindi kama ilivyokuwa ikifanya karne
nyingi zilizopita kutokana na mazingira yake ya kuwa kituo cha
Biashara enzi hizo.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikabidhi msaada wa
Tangi la kuhifadhia Maji safi, Mashine ya kusukumuia Maji pamoja na Luva
ya kusafishia Msikiti wa Ijumaa wa Kijiji cha Umbuji akitekeleza ahadi
aliyoitoa wakati wa Ufunguzi rasmi wa Msikiti huo Miaka michache
iliyopia.
Sheha
wa Shehia ya Umbuji Wilaya ya Kati Bwana Muhamad Mrisho Juma akitoa
shukrani kwa niaba ya Ungozi wa Msikiti huo kutokana na msaada huo
adhimu.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud
Mohamed akitoa shukrani kwa niaba ya Balozi Seif mara baada ya futari ya
pamoja na Wazee wanaohifadhiwa Nyumba za Serikali Welezo.
Balozi
Seif akiagana na Wazee wanaohifadhiwa katika Nyumba za Serikali
zilizopo Welezo mara baada ya kufutari nao pamoja akiendeleza utaratibu
wake aliojipangia ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Picha na – OMPR –
ZNZ.
No comments:
Post a Comment