Baraza
la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), leo limewaondolea
hofu wadau wanaoendesha huduma mbalimbali kwenye Viwanja vya ndege,
katika mkutano ulioitishwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania
(TAA), uliofanyika kwenye Ukumbi wa Watu Mashuhuri (VIP), kuhususiana na
katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki ambalo litaanza rasmi Juni
Mosi, 2019.
Mwanasheria
wa NEMC, Manchare Heche amesema kwa upande wa viwanja vya ndege ipo
mifuko, ambayo itaendelea kutumika kwa mujibu wa Kanuni namba tisa (9)
ya sheria ya kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki ya mwaka 2019, lakini
baada ya kutumika inatakiwa ihifadhiwe sehemu maalum na kupekekwa
mahali itakapoteketezwa.
“Kweli
katazo linahusu Watanzania wote na wageni na hapa Airport wapo
wanaotumia nikiwa na maana ya wafanyakazi na wateja wakiwemo abiria,
lakini katika sheria ukiangalia kanuni ya tisa 9 ipo mifuko ya
vifungashio ambayo haijazuiwa ni kama ile ya kuhifadhi vyakula, dawa,
kilimo na inayohifadhia takataka, mfano korosho au keki wanazopewa
abiria kwenye ndege mfuko wake upo katika kipengele cha chakula, hivyo
itaendelea kutumika lakini baada ya matumizi tu itahuifadhiwa sehemu
iliyoelekezwa tayari kwa kwenda kuteketezwa,” alisisitiza Heche.
Alisema
kwa upande wa plastiki zinazofungia mizigo ya abiria wanaosafiri kutoka
ndani na nje ya nchi kwa usafiri wa ndege itatakiwa kuondolewa abiria
anapofika nchini, na zitakusanywa na kuhifadhiwa maeneo maalum kabla ya
kupelekwa eneo lililotengwa kwa ajili ya kuziteketeza.
Hatahivyo,
kutokana na matumizi makubwa ya mifuko ya plastiki nchini imesababisha
uharibifu mkubwa wa mazingira ikiwemo ya kuziba kwenye mifereji ya maji,
kuua wanyama, na kuharibu ardhi, Heche amesema kufuatia katazo hilo
serikali imefuta leseni za viwanda vinavyotengeneza mifuko ya plastiki
na pia haijawapa tena leseni wale wote leseni zao zilizomaliza muda, ili
kuhakikisha sheria na kanuni ya kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki
namba 394 ya mwaka 2019.
Heche
ametoa angalizo kwa wale wote wanaohusika na ukamataji wa watumiaji wa
mifuko hiyo, kutotumia nguvu ili kuepusha mikwaruzano na kutoelewana.
Hatahivyo,
amewataka wadau hao kuhakikisha wanadai vitambulisho kwa wale wote
watakaofika kwenye maeneo yao ya kazi kudai wanakagua endapo wanaendelea
kuuza au kutumia mifuko ya plastiki.
Kwa
upande wa Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius
Nyerere (JNIA), Paul Rwegasha amesema tayari kupitia Mamlaka ya Viwanja
vya Ndege Tanzania (TAA), wameshatoa taarifa inayokwenda kwenye vituo
vyote vya Kimataifa, ambapo kuna shirika la ndege linaloleta abiria
Tanzania, ikitaarifu juu ya katazo la mifuko ya plastiki.
“Hii
taarifa inajulikana kitaalam kama ‘timatic pre-information’ ambayo
inatumwa kwenye centre zote duniani, ambapo kuna shirika la ndege ambalo
linaleta abiria Tanzania itakuwa rahisi wao kupata taarifa ya katazo
hilo na kuwafanya wasibebe mifuko hiyo,” amesema Rwegasha.
Pia
amewataka wadau wote wanaofanya shughuli mbalimbali kwenye viwanja vya
ndege kutoa ushirikiano mkubwa kuwaeleza abiria juu ya katazo hilo, na
kuwaelekeza watumie mifuko mbadala, ambayo itakuwa ikipatikana kwenye
maduka yaliyopo kwenye majengo ya Kwanza na Pili ya JNIA.
Kwa
mujibu wa NEMC imesema watumiaji wa kawaida endapo watakamatwa na
mifuko hiyo watatozwa faini ya Tshs. 30,000, kifungo cha siku saba, au
vyote kwa pamoja; wakati kwa muuzaji anapigwa faini ya Tshs 100,000
haizidi Tshs 500,000, kifungo cha miezi mitatu; na watengenezaji
watapigwa faini ya kuanzia Tshs milioni 20 na haitazidi bilioni moja na
kifungo cha miaka miwili.
Mwanasheria
wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC),
Manchare Heche (aliyenyanyua mikono) akisisitiza jambo wakati akiongea
na wadau wanaotoa huduma mbalimbali kwenye Kiwanja cha Ndege cha
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), juu ya katazo la mifuko ya plastiki
iliyopigwa marufuku kuendelea kutumika nchini ifikapo Juni Mosi mwaka
huu. Wapili kulia ni Mkurugezi wa JNIA, Paul Rwegasha na wa kwanza
kushoto ni mkuu wa kitengo cha Mazingira cha TAA, Maxmilian Mahangila.
Mkurugenzi
wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Paul
Rwegasha (aliyesimama) akielezea mikakati iliyowekwa na Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), ya namna ya kutekeleza agizo la
serikali la katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki kwa watumiaji wa
viwanja vya ndege nchini. Wapili kushoto ni Mwanasheria wa Baraza la
Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Manchare Heche.
Kaimu
Meneja wa Mamlaka ya Hali ya Hewa kwenye Kiwanja cha Ndege cha
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Joachim Philipo akitoa ushauri
kwenye mkutano wa wadau wanaotoa huduma mbalimbali JNIA ulioitishwa na
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), na kuhusisha Wataalam
kutoka Baraza ka Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC),
ambao walitoa maelezo mbalimbali juu ya katazo la matumizi ya mifuko ya
plastiki litakaloanza rasmi Juni Mosi, 2019 kwa mujibu wa sheria.
Mmoja
wa wadau wanaotoa huduma kwenye Jengo la Kwanza la Kiwanja cha Ndege
cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNI-TBI), Uyeka Rumbyambya akiongea
katika mkutano ulioitishwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania
(TAA) leo kwenye Ukumbi wa Watu Mashuhuri (VIP), na kuwashirikisha
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), katazo hilo
la matumizi ya mifuko ya plastiki litakaloanza rasmi Juni Mosi, 2019.
Mrakibu
Msaidizi wa Uhamiaji, Anna Mushi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha
Julius Nyerere (JNIA), leo akizungumza katika mkutano wa wadau wanaotoa
huduma mbalimbali JNIA katika mkutano ulioitishwa na Mamlaka ya Viwanja
vya Ndege Tanzania (TAA), na kuwahusisha Wataalam kutoka Baraza la
Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kutokana na katazo la
matumizi ya mifuko ya plastiki ifikapo Juni Mosi, 2019.
Mwanasheria
wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC),
Manchare Heche akiwaonesha wadau wanaotoa huduma mbalimbali kwenye
Kiwanja cha Ncdege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) moja ya
mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku kuendelea kutumika nchini ifikapo
Juni Mosi, 2019 katika mkutano uliofanyika leo kwenye ukumbi wa Watu
Mashuhuri (VIP).
No comments:
Post a Comment