Ni baada ya Serikali kusikia kilio kutoka kwa wafanyabiashara
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imeanza jitihada za
kufuta tozo zote ambazo zinakwamisha mazingira ya ufanyaji wa biashara
nchini zikiwemo za kwenye pembejeo ili kuwawezesha wafanyabiashara
kuzifikisha hadi ngazi ya kijiji kwa wakulima.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Mei 23, 2019) Bungeni jijini Dodoma
wakati akijibu swali la mbunge wa Madaba, Kizito Mhagama katika
kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu. Mbunge huyo alitaka kujua
Serikali ina mpango gani wa kupunguza tozo kwa maduka yanayouza
pembejeo ili kumwezesha mkulima kupata pembejeo.
Waziri Mkuu amesema Serikali imepokea malalamiko kutoka kwa
wafanyabiashara mbalimbali wakiwemo na wauzaji wa pembejeo juu ya tozo
mbalimbali katika uendeshaji wa shughuli nzima wa biasharazao.
“Serikali imesikia vilio vyenu na sasa inafanya mapitio ya tozo hizo
na itakapofikia hatua nzuri itawajulisha na kuwashirikisha kujua ni
aina gani ya tozo ambayo itaondolewa au kuibadilisha ili muendelee
kufanya biashara zenu katika mazingira rahisi.”
Waziri Mkuu amesema kazi kubwa inayofanywa na Serikali kwa sasa ni
kufanya mapitio ya tozo zote kuanzia kwa wakulima hadi kwa
wafanyabiashara na kutengeneza mazingira mazuri ya kufanya biashara
nchini, ikiwemo ya pembejeo ili kuzifikisha kiurahisi kwa wakulima.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema kwamba tayari Mawaziri wa kisekta
wenye dhamana ambao wana tozo mbalimbali kwenye wizara zao
zinazokwamisha ufanyaji biashara katika mazingira rafiki wameshakutana
kwa ajili ya kujadili namna ya kulipatia ufumbuzi suala hilo.
“Hata juzi nilikuwa na mawaziri hao kupata taarifa zao kwa pamoja
kuona maeneo yote waliyoyapitia na tozo zote zinazokusudiwa kupitiwa
upya na kazi hiyo ikikamilika watakutana na Kamati ya Bajeti ya Bunge,
Wizara ya Fedha ili kuona namna nzuri ya kuondoa tozo hizo. Lakini
baadaye suala hilo litaenda kwenye mamlaka inayotoa ridhaa ya kuondoa
au kupunguza tozo.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema miradi mingi ya maji ambayo
inatekelezwa kwenye maeneo mbalimbali nchini baadhi yake haitekelezwi
kwa viwango vilivyokusudiwa, hivyo haiwiani na thamani halisi ya kiasi
cha fedha kinachotolewa.
Hata hivyo Waziri wa Maji wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Wizara yake kwa mwaka 2019/2020 alieleza hatua mbalimbali
zilizochukuliwa dhidi ya miradi yote ambayo haiwiani na kiasi cha
fedha kilichotolewa pamoja na hatua zilizochukuliwa dhidi ya miradi
yote.
“Moja kati ya hatua ambazo amezifanya ni pamoja na kuunda timu
inayopita kukagua miradi yote nchini na kujiridhisha kama matengenezo
yake yanakidhi thamani ya fedha iliyotolewa katika mradi huo na kama
haukidhi hatua kali zinachukuliwa kwa wahusika.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la mbunge wa Korogwe
Mjini Mary Chatanda aliyetaka kujua Serikali kama ipo tayari
kuchunguza na kuchukua hatua kwa watendaji walioshindwa kusimamia
miradi ya maji na kuisababishia hasara pamoja na wananchi kukosa
huduma waliyokusudiwa.
No comments:
Post a Comment