Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania wote wamuenzi marehemu
Askofu Mstaafu Gaberiel Mmole (80) wa Jimbo Katoliki Mtwara kwa wema,
upole na utumishi mwema aliouonesha wakati wote wa maisha yake.
Ametoa
wito huo leo (Jumanne, Mei 21, 2019) wakati wa mazishi ya Askofu Mmole
yaliyofanyika katika Kanisa Katoliki Mtwara na kuhudhuriwa na viongozi,
waumini wa Kanisa Katoliki pamoja na wakazi wa mkoa wa Mtwara
Askofu
Mmole alizaliwa Januari Mosi, 1939 katika Parokia ya Nangoo, ambapo
alibatizwa na kupata kipaimara Oktoba 5, 1952. Mwaka 1971 alipata daraja
ya upadre na kuwa Askofu kuanzia mwaka 1988, alifariki Mei 15, 2019
Mkoani Mtwara baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Maeneo
aliyoyatumikia tangu apate daraja la padri ni Paroko msaidizi wa Mnero
(1972), Pastoral Institute GABA-Uganda (1973), Gombera Namupa seminari
(1974 hadi Mei 1988), alitangazwa kuwa askofu wa Jimbo la Mtwara Machi
12, 1988 na alisimikwa kuwa askofu wa Jimbo la Mtwara Mei 25, 1988.
Mwaka
1951 hadi 1954 alipata elimu ya singi katika shule ya msingi Ndanda,
1955 alisoma Nyangao Middle School, 1956 akahamia Lukuledi ambako
alihitimu 1958. Alienda chuo cha ualimu Peramiho 1959 hadi 1960, ambapo
1962 alijiunga na seminari ndogo ya Namupa na alihitimu 1964.
1965
hadi 1966 alichukua masomo ya falsafa kwenye seminari kuu ya Peramiho
na mwaka 1967 hadi 1971 alichukua masomo ya theolojia katika seminari
hiyo hiyo ya Peramiho. 1971 alifanya mitihani ya Baccalaureate inayotoka
chuo kikuu cha Kipapa Urbaniana Roma na kupata shahada ya theolojia.
Ibada
ya mazishi imeongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo la Songea, Mhashamu
Askofu Damian Dallu ambaye alitumia muda huo kuwaasa Watanzania kuishi
katika maadili mema na kuheshimiana.
Waziri
Mkuu amesema enzi za uhai wake Askofu Mmole alitoa kipaumbele katika
masuala muhimu ya maendeleo ya jamii ikiwemo elimu ambapo alisaidia sana
watawa waliomaliza darasa la saba na kuwasaidia wajiunge na shule za
sekondari.
“Hata
uanzishwaji wa chuo kikuu cha STEMMUCO ambacho ni tawi la SAUT hapa
Mtwara ni moja ya jitihada zake alizozifanya katika kuhakikisha anawapa
elimu bora vijana na jamii.
Kifo
chake ni pigo kubwa kwa Taifa kwa sababu tumepoteza kiongozi wa kiroho
aliyesimamia kwa uadilifu ustawi wa jamii ya Kitanzania.”
Kwa
upande wake, Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Mhashamu Askofu
Gervas Nyaisonga wa Jimbo Kuu la Mbeya amesema wamepata simanzi kubwa
kufuatia kifo cha Askofu Mmole kwani walitegemea hekima zake katika
Baraza la Maaskofu.
Ameongeza
kuwa Askofu Mmole alikuwa kielelezo cha dhamira njema na alilitumikia
kanisa katika hali yoyote, hivyo yatupasa kumuombea apumzike kwa amani.
Awali,
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwaaliwashukuru viongozi wa
madhehebu mbalimbali ya dini mkoani Mtwara kutokana kwa ushirikiano
mzuri anaopata unaomwezesha kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Mazishi
hayo yamehudhuriwa na maelfu ya wananchi, maaskofu wa majimbo
mbalimbali nchini, Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Mheshimiwa Benjamin
Mkapa na mkewe Mama Anna Mkapa, Waziri wa Nchi OR-Utumishi na Utawala
Bora Mheshimiwa Huruma George Mkuchika.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akitia saini kitabu cha maombolezo ya kifo cha
Askofu Mstaafu wa Jimbo Katoliki la Mtwara, Mhashamu Gabriel Mmole
katika mazishi yaliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Watakatifu Wote Mjini
Mtwara, Mei 21, 2019. Kulia ni Askofu wa Jimbo la Geita na Makamu wa
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Flavian Kasalla.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Mazishi ya Askofu Mstaafu wa
Jimbo Katoliki la Mtwara,Mhashamu Gebriel Mmole kwenye Kanisa Kuu la
Watakatifu Wote mjini Mtwara, Mei 21, 2019.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akimpa pole Askofu wa Jimbo Katoliki la Mtwara,
Titus Joseph Mdoe katika mazishi ya Askofu Mstaafu wa Jimbo Katolki la
Mtwara, Mhashamu Gabriel Mmole yaliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la
Watakatifu Wote mjini Mtwara, Mei 21, 2019.
Waombolezaji
wakiuweka kaburini mwili wa Askofu Mstaafu wa Jimbo Katoliki la Mtwara,
Mhashamu Gabriel Mmole katika mazishi yaliyofanyika kwenye Kanisa Kuu
la Watakatifu Wote mjini Mtwara, Mei 21, 2019.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka udongo kwenye kaburi la Askofu Mstaafu
wa Jimbo la Mtwara, Mhashamu Gebriel Mmole katika mazishi yaliyofanyika
kwenye Kanisa Kuu la Watakatifu Wote mjini Mtwara, Mei 21, 2019.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa
Benjamin Mkapa wakishiriki katika Ibada ya mazishi ya Askofu Mstaafu wa
Jimbo Katoloki la Mtwara, Mhashamu, Gabriel Mmole iliyoongozwa na
Askofu wa Jimbo la Mtwara,Titus Mdoe (kushoto) kwenye Kanisa Kuu la
Watakatifu Wote mjini Mtwara, Mei 21, 2019.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka shada la maua kwenye kaburi la Askofu
Mstaafu wa Jimbo Katoliki la Mtwara, Mhashamu, Gabriel Mmole katika
mazishi yaliyofanyika kwenye Kanisa la Watakatifu Wote mjini Mtwara, Mei
21, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
No comments:
Post a Comment