Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed ameiomba Jamhuri ya Watu
wa China kurejesha utaratibu wa madaktari wa nchi hiyo wanaokuja
kufanyakazi Zanzibar kukaa miaka miwili badala ya mwaka mmoja wa sasa.
Alisema tokea kuanzisha uhusiano wa madaktari wa China kuja Zanzibar
mwaka 1965 walikuwa wakikaa kipindi cha miaka miwili lakini utaratibu
huo ulibadilika miaka ya hivi karibuni na hivi sasa wanakaa mwaka
mmoja.
Waziri wa Afya alitoa ombi hilo alipokutana na Ujumbe wa wataalamu wa
afya kutoka Mji wa Xuzhou ambao upo nchini kufanya tathmini ya
Madaktari wanaokuja kufanyakazi Zanzibar katika hospitali ya Abdlala
Mzee Mkoani na Mnazimmoja.
Aliueleza ujumbe huo kwamba utaratibu wa zamani wa timu za madaktari
wa China kukaa miaka miwili ulikuwa unatoa fursa nzuri kwa madaktari
wa Zanzibar kujenga uzoefu na kujifunza mambo mengi ya kitaalamu
kutoka kwao.
Alisema madaktari wa Zanzibar wanapopata uzoefu kwa vitendo kutoka kwa
madaktari wa China inawasaidia kufanya vizuri wanapopata nafasi ya
masomo ya juu nje ya nchi.
Waziri Hamad aliushauri ujumbe huo kuwaelekeza madaktari wa China
waliopo Zanzibar kuwapa mafunzo madaktari wa Hospitali ya Abdalla Mzee
ya kutumia mashine mpya zilizowekwa katika hospitali hiyo na
kuitafsiri teknolojia iliyotumika ili baada ya kuondoka waweze
kuzitumia.
Aidha Waziri wa Afya aliwahimiza madaktari wazalendo kuwa tayari
kujifunza utaalamu kutoka madaktari wa China ambao wamekuwa wakifanya
matibabu ya kitaalamu na kuwashirikisha.
Kiongozi wa ujumbe huo Zhou Guangchum alimuhakikishia Waziri wa Afya
kwamba nchi yake itaendelea kuisaidia Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar na kuongeza msaada wake hasa katika sekta ya afya.
Aliahidi kuwa atalifikisha nchini kwake ombi la kurejesha utaratibu wa
zamani wa madaktari wanaokuja Zanzibar kukaa kwa kipindi cha miaka
miwili ili waweze kutoa mchango mkubwa zaidi kwa ndugu zao.
Waziri
wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed akizungumza na ujumbe kutoka Mji
wa Xuzhou Nchini China uliokuja kufanya tathmini ya Madaktari wa nchi
hiyo wanaokuja kufanya kazi Zanzibar Ofisini kwake Mnazimmoja Mjini
Zanzibar.
Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed akiagana na Kiongozi wa
ujumbe kutoka Mji Xuzhou Nchini China Zhou Guangchum baada ya kumaliza
mazungumzo yao yaliofanyika Ofisini kwake.
Picha na Makame Mshenga.Na Ramadhani Ali - Maelezo Zanzibar
No comments:
Post a Comment