Matokeo chanyA+ online




Tuesday, June 4, 2019

DKT. GWAJIMA AWAKUMBUKA YATIMA, AWAPA MKONO WA EID

 Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Dorothy Gwajima akiwa katika picha ya Pamoja na watoto wa kituo cha matumaini kilichopo Miuji Jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Doroth Gwajima amewataka wazazi na walezi kuwa makini na kuimarisha ulinzi na usalama wa mtoto wakati wa msimu sikukuu ya Eid.
Dr.Gwajima ameyasema hayo alipotembelea kituo cha kulelea watoto cha Nyumba ya matumaini kilichopo Kata ya Miuji Jijini Dodoma na kutoa misaada ya vitu mbali mbali kwa ajili ya sikukuu.

Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Dorothy Gwajima akifurahia kumbeba mtoto Queen wakati alipotembelea kituo cha kwatoto cha matumaini kilichopo Miuji Jijini Dodoma
“Ni wajibu wa kila mzazi kutekeleza jukumu lake la msingi la kuhakikisha mtoto yuko salama na anasherekea sikukuku katika mazingira rafiki na yenye kumjenga kimwili na kiakili zaidi bila kupata dhahama ya aina yeyote” Alisema Gwajima.
 Aidha Dr. Gwajima amekipongeza kituo hicho kwa jukumu kubwa walilo nalo lakuhakikisha watoto waliopo hapo wanapata malezi bora huku akiwaasa watoto kuzidisha upendo na mshikamano miongozi mwao.
  

Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na mtoto wakati akikagua kituo wakati wa ziara yake katika kituo cha matumaini kilichopo Miuji Jijini Dodoma
“Tunatekeleza hili kwakuwa ni wajibu wetu kuwalea watoto kwani hata sisi leo tumekuwa watu wazima kwa sababu ya juhudi za wakubwa zetu, nanyi watoto mtakuwa wakubwa kama sisi na mtakuja  kuwa viongozi wa taifa hili katika nyanja mbali mbali, hivyo pendaneni na kuishi kwa amani na msome kwa bidii” alisema Gwajima.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia masuala ya ustawi wa Jamii, OR-TAMISEMI, Rashed  Maftah, alisema zoezi hilo ni moja ya majukumu yao ya msingi na wajibu wao katika kuzihudumia Mamlaka zote 184 nchini katika kuhakikisha watoto waliokatika mazingira magumu wanapata  vituo vya kuwalea katika misingi bora na usalama wao unaimarika.

 Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Dorothy Gwajima akifurahi  katika picha ya Pamoja na mtoto Maria wa kituo cha matumaini kilichopo Miuji Jijini Dodoma
“Dini iliyosafi ni yenye kuwajali Yatima na wenye uhitaji kwa kuunganika na kushiriki nao katika mahitaji yao ya Msingi, aidha Sheria ya mtoto  namba 21 ya mwaka 2009 kanuni ya 12 inahimiza suala la kulelea watoto” Alisema Maftah.
Akizungumza kwa niaba ya Walezi wa kituo hicho, mmoja ya walezi, Sister Urea, alisema kituo hicho kina jumla ya watoto 63 na kimekuwa kikifanya kazi zake toka mwaka 1995 kwa kuhudumia watoto wanaopatikana katika mazingira magumu na ukatili wa kijinsia kutoka mikoa ya Dodoma na Singida.

Afisa Ustawi wa Jamii toka OR-TAMISEMI anayeshughulikia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi Nkinda Ziada Shekalaghe akizungumza wakati wa ziara ya Naibu Katibu Mkuu Dr.Dorothy Gwajima
Akishukuru kwa niaba ya wenzake mtoto Mariah Zahoro, alimshukuu Naibu Katibu Mkuu na ujumbe wake huku akiomba zoezi hili lisiwe la mwisho bali liwe endelevu kwani wanapopata wageni wanao watembelea wanafarijika sana.
“Tunawashukuru sana kuja kutuona na kutupatia misaada, lakini msiishie kuja kuleta misaada tu, hata kama hamna kitu msisite kuja kutusalimia na kuongea na sisi, tunaomba Mungu awazidishie pale mlipotoa na siku nyingine tena mtukumbuke” alisema Mariah.

Baadhi ya watoto katika picha ya pamoja wakimskiliza Dr.Dorothy Gwajima wakati wa ziara yake katika kituo cha matumaini kilichopo Miuji Jijini Dodoma
Kwa Mujibu wa Afisa Ustawi wa Jamii kutoka jijini Dodoma, kituo cha Nyumba ya Matumaini kilichopo Kata ya Mihuji ni moja kati ya vituo vinane vilivyopo ndani ya Halmashauri hiyo ambavyo vimekuwa mstari wa mbele kulinda haki za watoto.

No comments:

Post a Comment