Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, imevipatia vikundi
71 vya wanawake, vijana na walemavu, sh230.8 milioni ya mikopo kupitia
asilimia 10 ya mapato ya ndani ili kuwanyanyua kiuchumi.
Ofisa maendeleo ya jamii wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Asia
Ngalisoni akizungumza jana alisema vikundi hivyo ni vya kata 14
vilivyonufaika na mkopo huo.
Ngalisoni alisema mkopo huo umenufaisha vikundi 71, ambapo 59 ni vya
wanawake 1,531, vikundi tisa vya vijana 238 na vikundi vitatu vya
walemavu 57.
Alisema hadi mwezi Mei mwaka huu halmashauri hiyo imekusanya sh1.7
bilioni ikiwemo mapato ya ndani na marejesho ya fedha za vikundi
vilivyokopeshwa awali.
"Mfuko huu unawanufaisha wananchi waliojiunga katika vikundi vyenye
shughuli za ujasiriamali au vinavyokusudia kuanzisha shughuli za
ujasiriamali mdogo au wa kati," alisema Ngalisoni.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula alisema fedha hizo
zinazotolewa hazina riba hivyo vikundi hivyo vinapaswa kuchukua mikopo
hiyo na kurejesha kiasi kile kile walichokopa.
"Nitoe wito kwa vikundi vyote vilivyokopeshwa na halmashauri virejeshe
fedha hizo kwa wakati ili wengine nao waweze kukopa na kujikwamua
kiuchumi," alisema Chaula.
"Mfuko huu unawanufaisha wananchi waliojiunga katika vikundi vyenye
shughuli za ujasiriamali au kinakusudia kuanzisha shughuli za
ujasiriamali mdogo au wa kati," alisema Chaula.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Jackson Sipitieck alimpongeza
mkurugenzi mtendaji wa halmashauri yake Yefred Myenzi kwa kusimamia
ipasavyo mapato hadi kufanikisha utolewaji wa mikopo hiyo.
"Wakati halmashauri nyingine zikisuasua kufanikisha mikopo sisi
Simanjiro tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani tunatoa mikopo hadi
fedha nyingine zimebaki," alisema Sipitieck.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Yefred
Myenzi alitoa wito kwa vijana wa eneo hilo kuchangamkia fursa hiyo
kwani mwitikio wao bado ni mdogo.
"Zile fedha zenu vijana za asilimia nne mnazopaswa kupewa
hamjazichukua hivyo vijana wa Simanjiro mnapaswa kubadilika ili
mnufaike kupitia mikopo hii tunayoitoa," alisema Myenzi.
Katibu wa walemavu mji mdogo wa Mirerani, William Orata alisema
kupitia mkopo waliopata wamefanikisha uanzishwaji wa mashine ya kusaga
nafaka.
Mmoja kati ya wanawake walionufaika na mkopo huo, Susan Alanyamuna
alisema wameweza kutengeneza sabuni aina ya Sidai.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, mhandisi Zephania Chaula (kushoto) akipokea mfano wa hundi kutoka benki ya NMB.
Mkuu
wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, mhandisi Zephania Chaula
(kushoto) akipeana mkono na viongozi wa vikundi vya wanawake, vijana na
walemavu baada ya kupokea mkopo uliotolewa na Halmashauri ya Wilaya hiyo
Baadhi ya vikundi vya wajasiriamali, wanawake, vijana na walemavu
waliopatiwa mkopo wa sh 230.8 milioni na Halmashauri ya Wilaya ya
Simanjiro Mkoani Manyara.
No comments:
Post a Comment