Rais
wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Mhe. Felix Antoine Tshisekedi
amemaliza Ziara ya Kitaifa ya siku 2 aliyoifanya hapa nchini kwa
mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli.
Mhe.
Tshisekedi ameagwa na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli katika uwanja wa
ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kuelekea
nchini Burundi.
Mapema
leo asubuhi Mhe. Rais Tshisekedi ametembelea mradi wa ujenzi wa reli ya
kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge Railway) katika eneo la
Vingunguti Jijini Dar es Salaam na baadaye akatembelea Bandari ya Dar es
Salaam ambayo hutumika kupitisha mizigo ya DRC.
Akiwa
Ikulu Jijini Dar es Salaam Mhe. Rais Tshisekedi amefanya mazungumzo na
mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli na baadaye viongozi hao wamezungumza na
wananchi kupitia vyombo vya habari.
Mhe.
Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Tshisekedi kwa kufanya Ziara ya
Kitaifa hapa nchini na kwa dhamira yake ya kukuza na kuimarisha zaidi
uhusiano na ushirikiano kati ya DRC na Tanzania hususani katika uchumi.
Mhe.
Rais Magufuli amesema kiwango cha biashara kinachofanywa kati ya
Tanzania na DRC ni kidogo ikilinganishwa na ukubwa wa uhusiano na fursa
zilizopo kati ya nchi hizo, ambapo katika mwaka uliopita biashara kati
ya Tanzania na DRC ilikuwa na thamani ya shilingi Bilioni 305.375,
wafanyabiashara wa DRC walikuwa wamewekeza nchini Tanzania miradi 8
yenye thamani ya shilingi Bilioni 13.144 na kukiwa na Watanzania
wachache ambao wameweka nchini DRC.
Amefafanua
kuwa japo kuwa sekta ya usafirishaji inaridhisha kidogo kwa DRC
kuongeza mizigo inayopita Bandari ya Dar es Salaam kutoka tani Milioni
1.176 ya mwaka 2017 hadi kufikia tani Milioni 1.78 ya mwaka 2018, kuna
haja ya kuchukua hatua madhubuti zaidi za kukuza biashara na uwekezaji
ikiwemo kuondoa vikwazo, kutumia fursa mbalimbali zilizopo ikiwemo
madini, uvuvi, kilimo, ujenzi wa viwanda na kulitumia ipasavyo soko la
nchi hizo lenye jumla ya watu Milioni 140.
Kwa
upande wa Tanzania, Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na kujenga reli
ya kati (SGR), kupanua Bandari ya Dar es Salaam, kuanzisha huduma za
pamoja za bandari kwa saa 24 (siku zote 7 za wiki) na kuimarisha
miundombinu ya barabara katika njia 8 za kuingia na kutoka DRC, Tanzania
imeongeza muda wa kusubiri bandarini kutoka siku 24 hadi 30 kwa mizigo
ya DRC, imeondoa katazo la ufunguaji makontena na kufuta tozo ya
kusindikiza mizigo hadi mpakani mwa Tanzania na DRC.
Aidha,
Mhe. Rais Magufuli amesema Tanzania itaikarabati meli ya MV. Liemba
inayotoa huduma kati ya Tanzania (Kigoma) na DRC, itajenga meli mpya
mbili ambapo moja itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 600 na mizigo tani
400 na ya pili itakuwa meli ya mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 2,000
na ameafiki mapendekezo ya Mhe. Rais Tshisekedi ya reli ya kati ya
Tanzania kujengwa kutoka Isaka – Rusumo – Kigali hadi Mashariki ya Kongo
ili kufikisha mizigo moja kwa moja nchini DRC.
Mhe.
Rais Magufuli amewataka Mawaziri na Wataalamu wa Tanzania na wenzao wa
DRC (watakaoteuliwa) ndani ya mwaka huu, kuitisha kikao cha Kamati ya
Pamoja ya Ushirikiano (Joint Permanent Commission – JPC) ambacho
hakijawahi kufanyika tangu mwaka 2002 ili kujadili na kurejesha maeneo
muhimu ya ushirikiano ikiwemo ushirikiano katika usafiri wa anga kati ya
Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) na Shirika la Ndege la Congo (Congo
Airways).
Mhe.
Rais Magufuli amemtakia heri Mhe. Rais Tshisekedi katika uongozi wake
na amemshauri kusimama kidete kutatua matatizo ya wananchi wa DRC huku
akisisitiza kuwa kwa utajiri wa DRC, uchumi wa nchi hiyo haupaswi kukua
kwa kiwango kidogo cha asilimia 4.
Kwa
upande wake, Mhe. Rais Tshisekedi amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa
kumwalika kufanya Ziara ya Kitaifa hapa nchini na amebainisha kuwa lengo
la ziara yake ni kuimarisha na kukuza zaidi udugu, urafiki na uhusiano
wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na DRC.
Mhe.
Tshisekedi amesema katika mazungumzo yake na Mhe. Rais Magufuli
wamekubaliana kuwa bila amani jitihada za maendeleo katika eneo lote la
maziwa makuu hazitafanikiwa, hivyo wana kila sababu ya kuhakikisha
kunakuwa na amani ya kudumu pamoja na kutumia vizuri fursa mbalimbali za
kukuza uchumi ukiwemo ukanda wa ziwa Tanganyika wenye urefu wa kilometa
554.
Amesema
ana matumaini kuwa JPC itakayofanyika itatatua changamoto zote za
kukuza biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na DRC na ameahidi kufanya
kazi kwa ushirikiano wa karibu na Mhe. Rais Magufuli.
Pamoja
na kumshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa ahadi yake ya kuunga mkono ombi la
DRC kujiunga katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Rais Tshisekedi
ameahidi kuhudhuria Mkutano wa 39 Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini
mwa Afrika (SADC) utakaofanyika mwezi Agosti mwaka huu hapa Tanzania na
amebainisha kuwa anaamini kuwa SADC ni jumuiya yenye fursa na manufaa
makubwa ya kiuchumi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
14 Juni, 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli
akimsindikiza mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)
Mhe. Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo baada ya kuhitimisha ziara yake
rasmi ya siku mbili jijini Dar es salaam leo
Juni 14, 2019
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na
mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Mhe. Félix
Antoine Tshisekedi Tshilombo anayeagana na Katibu Mkuu wa Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa afrika Mashariki Mhe. Faraji Kasidi
Mnyepe baada ya kuhitimisha ziara yake rasmi ya siku mbili jijini Dar es
salaam leo Juni 14, 2019
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongea na
Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es
salaam Mhe. Paul Makonda wakati wakisumbiri ili kumuaga mgeni wake Rais
wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Mhe. Félix Antoine Tshisekedi
Tshilombo baada ya kuhitimisha ziara yake rasmi ya siku mbili jijini Dar
es salaam leo Juni 14, 2019
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na
mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Mhe. Félix
Antoine Tshisekedi Tshilombo anayeagana na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Profesa palagamaba Kabudi baada ya
kuhitimisha ziara yake rasmi ya siku mbili jijini Dar es salaam leo Juni
14, 2019
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na
mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Mhe. Félix
Antoine Tshisekedi Tshilombo anayeagana na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na
Usalama katika
Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam baada ya
kuhitimisha ziara yake rasmi ya siku mbili leo Juni 14, 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe
Magufuli akiagana kwa furaha na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya
Kidemokrasia 54 ya Congo (DRC) Mhe. Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo
katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es
salaam baada ya kuhitimisha ziara yake rasmi ya siku mbili leo Juni
14, 2019
PICHA NA IKULU
No comments:
Post a Comment