Naibu
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso akiongea kwa simu na Mkurugenzi
Mtendaji wa Kampuni ya Nangai Engineering Ltd alipokuwa akikagua Mradi
wa Maji wa Itigi, uliopo katika Halmashauri ya Itigi, wilayani Manyoni,
mkoani Singida.
Naibu
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso akimsikiliza Mhandisi wa Maji
Halmashauri ya Itigi, Evaristo Mgaya kwenye moja ya vituo vya maji
vinavyojengwa wakati akikagua Mradi wa Maji wa Itigi, uliopo katika
Halmashauri ya Itigi, wilayani Manyoni, mkoani Singida. Kulia ni Mkuu wa
Wilaya ya Itigi, Rahabu Mwangisa.
Naibu
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso akiwa kwenye kisima cha maji kilichopo
eneo la Kanisani, moja ya visima 5 vya Mradi wa Maji wa Itigi, uliopo
katika Halmashauri ya Itigi, wilayani Manyoni, mkoani Singida.
………………
Serikali
imesema itaweka bayana majina ya makandarasi wote wanaoharibu miradi ya
maji kwa kuitekeleza chini ya kiwango na kuwachukulia hatua kali za
kisheria katika hatua ya kumaliza tatizo la utendaji mbovu kwenye kazi
za miradi ya maji linalochangia wananchi kukosa huduma ya maji.
Naibu
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ametoa kauli hiyo mara baada ya
kutoridhishwa na Mkandarasi wa Kampuni ya Nangai Engineering Ltd kufanya
kazi kwa asilimia 30 ukilinganisha na kiasi cha Shilingi milioni 250
alizolipwa, wakati mkandarasi wa Kampuni ya Nipo Africa Ltd akiwa
amefanya kazi kwa asilimia 68 huku akidai fedha za malipo za ujenzi wa
Mradi wa Maji wa Itigi uliopo katika Halmashauri ya Itigi, Wilaya ya
Manyoni, mkoani Singida alipokuwa akikagua mradi huo.
‘‘Wakandarasi
wababaishaji wa namna hii wote tutawaanika hadharani na watachukuliwa
hatua kali za kisheria na Bodi ya Wakandarasi (CRB), Wakala wa Maji
Vijijini (RUWASA) utakapoanza Julai Mosi, 2019 utakuwa ni mwisho wa
wakandarasi wababaishaji kupata kazi za miradi ya maji ’’, amesema
Aweso.
‘‘Serikali
imelenga kufikisha huduma ya maji kwa wananchi, hatutakubali mkandarasi
au mtu yeyote kukwamisha juhudi zetu za dhati za kumaliza tatizo la
maji. Kuanzia sasa tutaorodhesa wakandarasi wote wasio na sifa na
kuwafungia wasipewe kazi miradi yoyote ya maji nchini, ameelekeza Naibu
Waziri.
Aidha,
Aweso ameipongeza Kampuni ya Nipo Africa Ltd kwa kufanya kazi nzuri,
akiahidi kuyafanyia kazi madeni yao na kuwalipa haraka. Pia, amewataka
Wakurugenzi Watendaji wa Kampuni za Nangai Engineering Ltd na Nipo
Africa Ltd kukutana nae siku ya Alhamisi Julai 20, 2019 kwenye kikao
kitakaochuhusisha viongozi na wataalam wa Sekta ya Maji mkoani Singida
kitakacholenga kukwamua mradi huo uweze kukamilika kwa wakati.
Wakati
huo, Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Rahabu Mwangisa amemshukuru Naibu
Waziri kwa ahadi yake ya kumlipa mkandarasi huyo na kumuahidi kuwa
viongozi wa Wilaya ya Manyoni watasimamia mradi huo kwa ukaribu uweze
kukamilika haraka.
Ujenzi
wa Mradi wa Maji Itigi umeanza kutekelezwa mnamo 3/12/2018 na
unategemewa kukamilika 2/9/2019 kwa zaidi ya Shilingi bilioni 2.6
ukihusisha uchimbaji wa visima 5 virefu vyenye uwezo wa kutoa jumla lita
za ujazo 112,000 kwa saa, pamoja na ujenzi wa miundombinu ya maji.
Mradi
huu utakapokamilika unatarajiwa kuhudumia vijiji 6 vya Songambele,
Mlowa, Majengo, Tambukareli, Zinginali na Itigi unahusisha Mradi wa Maji
wa Itigi utakaogharimu zaidi ya Shilingi bilioni 2.6.
No comments:
Post a Comment