Naibu
waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
akizindua Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro
mwishoni mwa wiki, kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Ngollo Malenya na
kulia kwa Naibu Waziri ni Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba nchini
Stela Tulo.
Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Ngollo Malenya wakati wa
uzinduzi wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Ulanga Mwishoni mwa
wiki. Kushoto ni Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba nchini Stela
Tulo.
Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
akizungumza wakati wa uzinduzi wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya
Ulanga mkoani Morogoro mwishoni mwa wiki. Wa pili kushoto ni Mkuu wa
Wilaya ya Ulanga Ngollo Malenya na wa kwanza kulia ni Msajili wa
Mabaraza ya Ardhi na Nyumba nchini Stela Tulo. (PICHA ZOTE NA HASSAN MABUYE- WIZARA YA ARDHI)
Na Munir Shemweta, WANMM ULANGA
Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
amepiga marufuku wananchi wanaoshitakiana katika Mabaraza ya Ardhi kutoa
pesa kwa ajili ya kugharimia usafiri wa kwenda eneo lenye mgogoro.
Akizungumza
wakati wa kuzindua Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Ulanga mkoani
Morogoro mwishoni mwa wiki Dkt Mabula alisema, kutoa pesa ya kugharamia
usafiri kwa mmoja wa wanaoshitakiana katika Mabaraza ya Ardhi kwenda
eneo la tukio kunaweza kuleta ushawishi kwa wajumbe wake hasa kwa yule
aliyetoa kiasi kikubwa cha pesa.
Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, ni lazima wakati
wa zoezi la kwenda eneo lenye mgogoro kwa wanaoshitakiana katika
Mabaraza ya Ardhi Mkurugenzi wa Halmashauri husika aratibu zoezi hilo
huku ratiba nzima ikiwasilishwa kwa Mkuu wa Wilaya katika kipindi cha
mwezi mmoja.
‘’
Jamaa anatoa laki mbili anayelalamika hana kitu unategemea hapo haki
itatendekaje, ni marufuku kabisa na taratibu zote za kwenda uwandani
zipitie kwa DC na ratiba ijulikane mapema’’ alisema Dkt Mabula.
Akigeukia
uzinduzi wa Baraza la Ardhi na Nyumba katika wilaya ya Ulanga, Dkt
Mabula alisema Serikali imezindua Baraza hilo ili kupeleka huduma
karibu na kurahisisha usikilizaji kesi za ardhi kwa wananchi ambao
baadhi ya maeneo wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kupata huduma hiyo na
kubainisha kuwa sasa wananchi wa Ulanga watapata haki kwa wakati na kwa
umbali mdogo.
Aliwaasa
wananchi wa wilaya ya Ulanga kulitumia vyema Baraza Ardhi na Nyumba
lililozinduliwa na kuwataka kuhakikisha wanafuata taratibu zote za
utatuzi wa migogoro ya ardhi pamoja na kuachana na ile migogoro ya
kifamilia kwa kutumia Mabaraza ya Vijiji na Kata kushughulikia migogoro
hiyo.
Dkt
Mabula aliusifu mkoa wa Morogoro kwa kutoa mafunzo kwa wajumbe wa
Mabaraza ya Ardhi na kubainisha kuwa mafunzo hayo yawe chachu kwa
wajumbe wake kutenda haki wakati wa kufanya maamuzi kwa kuwa tayari wana
weledi katika eneo hilo.
Kwa
upande wake Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba nchini Stela Tulo
alisema, uzinduzi wa Barazala la Ardhi katika wilaya ya Ulanga limejibu
kiu ya muda mrefu ya wananchi wa wilaya hiyo kupata huduma kwa ukaribu
ambapo awali iliwalazimu kusafiri umbali mrefu hadi Kilombero kupata
huduma.
Kwa
mujibu wa Stela, kuzinduliwa kwa Baraza la Ulanga sasa kunaufanya mkoa
mzima wa Morogoro kuwa na Mabaraza ya Ardhi na Nyumba Manne (4) na
kubainisha kuwa Baraza hilo sasa linaongeza idadi ya Mabaraza
yanayofanya kazi nchini kufikia 54 kati ya 97 yaliyoidhinishwa.
Msajili
huyo wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba nchini alisema, mkoa wa Morogoro
pekee kwa sasa una Mashauri 2,500 ya ardhi kati ya 29,000 nchi nzima na
kubainisha kuwa, kuzinduliwa kwa Baraza la Ulanga ni moja ya jitihada
kuhakikisha Mashauri katika mkoa huo yanapungua kama siyo kuisha kabisa.
No comments:
Post a Comment