Matokeo chanyA+ online




Monday, June 3, 2019

WAZIRI MHAGAMA AZINDUA BARAZA LA TAIFA LA USHAURI KWA WATU WENYE ULEMAVU

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na wajumbe wa Baraza jipya la Taifa la ushauri kwa Watu wenye Ulemavu (hawapo pichani) kuhusu umuhimu wa baraza hilo kushirikiana na Serikali wakati akizindua Baraza hilo katika ukumbi wa mikutano wa PSSSF, Jijini Dodoma.

Na; Mwandishi Wetu

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amezindua rasmi Baraza la Taifa la ushauri kwa Watu wenye Ulemavu huku akilitaka baraza hilo kufanya kazi kwa weledi na ushirikiano ili kuleta tija na mafanikio makubwa kwa Watu wenye Ulemavu nchini.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo alisema kuwa baraza linajukumu kubwa katika kuhakikisha usimamizi wa sekta ya watu wenye ulemavu pamoja na kuishauri Serikali juu ya masuala mbalimbali ya kundi hilo maalumu.
“Mtambue nafasi mliyopewa ni dhamana kubwa katika kuwahudumia watu wenye ulemavu ambao ni takribani asilimia 5 ya watanzania, hivyo ni vyema mkashirikiana na Serikali kubuni mikakati itakayosaidia kutatua changamoto zinazowakabili wenye ulemavu”, alisema Mhagama
Alifafanua kuwa Baraza hilo limeundwa kwa mujibu wa Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 ya Mwaka 2010 na Sheria hiyo imeeleza majukumu ya Baraza ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri.
“Ni matumaini yangu mtakuwa washauri wazuri wa masuala ya watu wenye ulemavu kwa kuzingatia usawa kwa wote na si maslahi binafsi,” alisisitiza Mhagama.

Naibu Waziri,Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Stella Ikupa akielezea jambo kwa wajumbe wa Baraza wakati wa uzinduzi wa Baraza hilo uliofanyika tarehe 2 Juni, 2019 Jijini Dodoma.
Sambamba na hilo alimpongeza Mwenyekiti mpya wa Baraza hilo Dkt. Lukas Kija kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli pamoja na Wajumbe wengine kutokana na uaminifu na uwezo walionao katika kusimamia masuala ya Watu wenye Ulemavu.

Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha Watu wenye Ulemavu wanapata haki zao za msingi na kwa ajili ya ustawi wao katika Nyanja mbalimbali ikiwemo elimu, afya, uchumi, kuwa na miundombinu rafiki pamoja na nyenzo za kujimudu.
Aidha Waziri Mhagama alitoa rai kwa watendaji wa Baraza hilo kuwa na miongozo yote inayohusu masuala ya Watu wenye Ulemavu itakayo wawezesha kufanikisha utendaji wao wa kazi.
Kwa Upande wake Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Stella Ikupa amesema kuwa Serikali katika mwaka 2019/2020 itaanza mapitio ya Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010 ili kuwawezesha watu wenye ulemavu kwenda sambamba na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza jipya la Taifa la ushauri kwa Watu wenye Ulemavu mara baada ya kuzindua Baraza hilo Jijini Dodoma. Wa pili kutoka kulia ni Mwenyekiti mpya wa Baraza la Taifa la ushauri kwa Watu wenye Ulemavu Dkt. Lukas Kija, wa pili kutoka kushoto ni Naibu Waziri,Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Stella Ikupa. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Bw. Andrew Massawe na kulia ni Katibu Taifa wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu (SHIVYAWATA) Bw. Jonas Lubayo.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la ushauri kwa Watu wenye Ulemavu Dkt. Lukas Kija alieleza kuwa wapo tayari kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo inayosimamia haki na ustawi wa Watu wenye Ulemavu.
Aliongeza kuwa Baraza hilo lipo tayari kutoa ushauri na hoja zenye tija kwa Serikali juu ya masuala mbalimbali ya Watu wenye Ulemavu.
Pia, Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Bw. Andrew Massawe alieleza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa Baraza hilo na kufanya kazi pamoja katika kutatua changamoto zinazowakabili Watu wenye Ulemavu nchini ikiwemo migogoro na migongano kwa wadau.
Uzinduzi wa Baraza la Taifa la Ushauri kwa Watu wenye Ulemavu umefanyika Juni 2, 2019 jijini Dodoma ambapo Baraza hilo litaongoza kwa kipindi cha miaka mitatu (2019 hadi 2021) likiongozwa na Mwenyekiti Dkt. Lukas Kija. Awali Baraza hilo lilikuwa likiongozwa na Dkt. Edward Bagandanshwa ambalo limemaliza muda wake mwaka 2017.

No comments:

Post a Comment