WAZIRI NDALICHAKO AZINDUA MABARAZA YA UJUZI YA KISEKTA
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema
serikali kupitia Wizara ya Elimu inaendelea kuimarisha stadi na ujuzi
katika sekta sita za kipaumbele ili kufikia azma ya kuwa na uchumi wa
kati unaotegemea viwanda ifikapo 2025.
Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo
wakati wa halfa ya uzinduzi wa Mabaraza ya Ujuzi ya Kisekta jijini Dar
es Salaam ambapo mabaraza hayo yaliyoundwa kupitia Mradi wa Kukuza Ujuzi
na Stadi za Kazi (ESPJ) na sekta zilizopewa kipaumbele katika Mpango
Mkakati wa Taifa wa Kukuza na Kuendeleza ujuzi ni pamoja na Kilimo,
TEHAMA, Nishati, Ujenzi, Uchukuzi na Utalii.
“Katika azma ya Serikali ya kufikia
uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo 2025, tunapaswa kuhakikisha
nchi yetu inakuwa na nguvukazi yenye ujuzi na stadi stahiki
zinazohitajika kwenye soko la ajira,” amesisitiza Waziri Ndalichako.
Akizungumzia Mabaraza ya Ujuzi ya Kisekta
Prof. Ndalichako amesema Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
iliingia makubaliano rasmi ya ushirikiano (MoU) na Tanzania Private
Sector Foundation (TPSF) ili kusimamia uanzishaji na kuratibu mabaraza
hayo ambayo yatakuwa kiunganishi muhimu kwa kuwaleta pamoja wadau
mbalimbali wa masuala ya kuendeleza na kutumia ujuzi nchini.
“Tutaendelea kutoa ushirikiano kwa sekta
binafsi na wadau wengine kwa kuweka mifumo wezeshi na rafiki, programu
mbalimbali za kuendeleza ujuzi, na kuimarisha miundombinu ili
kuhakikisha nchi inajenga ujuzi na stadi stahiki kwa ustawi wa maendeleo
ya nchi,” amesema Prof. Ndalichako.
Waziri Ndalichako amesema kupitia
ushirikiano kati ya Sekta Binafsi na Umma serikali inatarajia kupata
ushirikiano katika programu za mafunzo ya wahitimu tarajali mahali pa
kazi (internships) na kutambua ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa
elimu (recognition to prior learning – RPL) ili kupunguza na kuondoa
changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii.
Aidha, Prof. Ndalichako ametoa ombi kwa
sekta binafsi kuendelea kupokea vijana wanaokwenda kufanya mafunzo kwa
vitendo ili kuwajengea utayari wa kuingia kwenye soko la ajira.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi
(TPSF), Salum Shamte alisema mabaraza yatakuwa ni fursa pekee ya
kuunganisha Taasisi Binafsi, Serikali na Wadau mbalimbali wa maendeleo
kutoka nje ya nchi katika kuleta ufanisi katika maendeleo.
Shamte amesema TPSF imekuwa ikitoa
ushauri na mapendekezo mbalimbali kwa serikali kupitia Baraza la Taifa
la Biashara (TNBC) katika ngazi ya wilaya, Mkoa , Wizara na hata Taifa
ili yaweze kufanyiwa kazi.
No comments:
Post a Comment