Makamu
wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Iddi ameitaka
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuendelea kuimaisha
mitandao na mifumo ya biashara nchini ili kuwawezesha wafanyabiashara wa
Tanzania kuweza kuwa na uhakika wa masoko bora ya bidhaa za ndani na nje ya
nchi.
Akifunga Maonesho ya 43
ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) leo Alhamisi (Julai 11, 2019)
Balozi Idd alisema Maonesho hayo ya mwaka huu yameonesha dhamira na mwelekeo wa
Serikali katika kutumia fursa biashara na viwanda katika kujenga uchumi imara
pamoja na kutengeneza ajira kwa wananchi.
Balozi Idd alisema ni
wajibu wa TANTRADE kutumia fursa za uwepo wa makampuni ya wazalishaji, wauzaji
na wafanyabiashara kutoka nje wanaoshiriki katika maonesho hayo kuweza kujenga
mitandao imara ya mahusiano na ushirikiano kwa wafanyabiashara wa ndani ili
kuweza kuwatafutia masoko ya bidhaa zao ambazo kwa sasa zimeanza kuzalishwa
katika viwango bora nchini.
“Nawapongeza TANTRADE kwa
juhudi zenu za kuanzia klinilki za biashara, na hili limewezesha
wafanyabiashara wetu kuweza kukutana na wanunuzi mbalimbali ambao huweza kuwapa
uzoefu wa namna bora zaidi ya kuzalisha bidhaa zenye kukithi viwango na ubora
unaotakiwa” alisema Balozi Idd.
Aidha Balozi Idd
alisema Serikali kwa sasa inatekeleza Mpango Kazi wa Kuboresha Mfumo Udhibiti
wa Biashara Nchini (Blue Print), ambao umekusudia kuondoa changamoto mbalimbali
za wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi, hivyo aliitaka TANTRADE
kushirikiana na wadau na wazalishaji wa sekta binafsi ili kuiwezesha sekta ya
biashara kuvutia wawekezaji wengi zaidi.
Kwa mujibu wa Balozi Iddi
pia aliitaka TANTRADE kuweka utaratibu wa kufuatilia oda za maombi mbalimbali
zinazotolewa na wafanyabiashara kutoka nje ya nchi ili kuendelea kupanua wigo
wa soko la bidhaa za Tanzania nje ya nchi ambalo kwa sasa limeendelea kupanuka
kutokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali.
Balozi alisema ni
wajibu wa Watanzania kujenga utamaduni wa kuthamini bidhaa za ndani ili
kuziwesha kupata masoko ya uhakika kwa kuwa kwa kufanya hivyo kutatoa fursa ya
kuweza kutambulika kwa haraka pamoja na kumudu changamoto ya ushindani wa
masoko ya bidhaa zinazozalishwa nje ya nchi.
Alisema kuwa maonesho
hayo ya 43 yamethibitisha uwezo wa wafanyabiashara wa Tanzania katika kutengeneza
na kuzalisha bidhaa mbalimbali kwani
idadi ya washirki wa maonesho kutoka nje ya nchi imeweza kuongezeka kutoka
makampuni kutoka nje 2956 mwaka 2018 hadi kufikia 3250 mwaka 2019, hivyo
kudhibitisha uwezo wa serikali katika kusimamia sekta ya biashara nchini.
Balozi Idd anasema kuwa
Makampuni ya wafanyabiashara ya Tanzania yaliyoshiriki maonesho hayo yanapaswa
kupata uzoefu na uelewa mkubwa katika namna bora zaidi ya kusimamia na kuratibu
sekta ya biashara nchini katika viwango bora ili kuweza kutengeneza masoko ya
uhakika katika nchi za nje.
Kwa upande wake Waziri
wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa alisema Serikali imeendelea
kuboresha mazingira ya biashara nchini ikiwemo kuanza kufanya mapitio ya sera
na sheria mbalimbali ambazo awali zilikuwa zikileta changamoto mbalimbali kwa
wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.
Aliongeza kuwa katika
kuhakikisha kuwa sekta ya viwanda na biashara inaleta tija katika ukuaji uchumi
nchini, Serikali imekusudia kuweka msisitizo katika kujenga uchumi jumuishi kwa
kuziweka sekta ya uvuvi, kilimo na mifugo kuwa kipaumbele muhimu katika kuzitumia
rasilimali mbalimbali zilizopo katika sekta hizo katika kutengeneza ajira kwa
wananchi walio wengi.
No comments:
Post a Comment