Kamishina wa Uraia na Pasipoti, Gerald Kihinga
Akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo) Pichani kuhusu kushikiliwa kwa
Mwanahabari, Erick Bendera, katika Mkutano
uliofanyika Ofisi za Idara ya Uhamiaji kanda ya Dar es Salaam.(PIcha na Mpiga
picha Wetu).
Serikali kupitia Idara
ya Uhamiaji imetoa ufafanuzi kuhusu Mwandishi wa kujitegemea Erick Kabendera
baada ya kusambaa kwa taarifa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii,
kuwa amekamatwa na anahojiwa kuhusu uraia wake na Idara ya Uhamiaji Jijini Dar
es Salaam.
Akizungumza Jijini Dar
es Salaam, Kamishna wa Uraia na Pasipoti wa Idara ya Uhamiaji Gerald Kihinga, amesema
kuwa Erick Kabendera ameshikiliwa na Jeshi
la Polisi na Uhamiaji Jijini Dar es Salaam kwa mahojiano zaidi ili kuweza
kupata taarifa juu ya uraia wake.
Kamishna huyo wa
Uhamiaji amesema Idara ya Uhamiaji inadhamana kubwa ya kusimamia na kutekeleza
Sheria ya uraia wa Tanzania sura ya 357 rejeo la 2002, inayotoa mamlaka kwa
taasisi hiyo kuchunguza na kuthibitisha uraia wa mtu yeyote.
“Idara ya Uhamiaji ni
chombo kilichopewa dhamana kubwa ya kutekeleza na kusimamia uraia wa Tanzania,
kwa hiyo siyo mara ya kwanza kufanya hivyo, sisi tunamshikilia Kabendera kwa
mahojiano kuhusu uraia wake, na siyo yeye tu aliyefanyiwa hivyo, idara ya Uhamiaji
inatimiza matakwa ya sheria ya uraia nchini na wala si vinginevyo” Alisema.
Alieleza kuwa idara ya
Uhamiaji ilipata taarifa za Erick Kabendera kutoka kwa raia wema na ikaamua
kumtafuta ili kufanya naye maojiano lakini hakuwa tayari kutoa ushirikiano
ikiwa ni pamoja na kukataa kufika ofisi za Uhamiaji, hali iliyopelekea
kukamatwa na sasa anaendelea kuhojiwa.
Mkuu huyo wa masuala ya
uraia na Pasipoti alifafanua kuwa, kushikiliwa huko kwa Erick Kabendera na
kuendelea na mahojiano ni swala ambalo limekuwepo kwa raia wote ambao uraia wao
una utata, wakiwemo watu wa kawaida, watu mashuhuri na wengine wowote ambao
kutaonekana uhitaji.
Amesema kumekuwa na
ushirikiano baina ya Uhamiaji na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ikwemo Polisi,
ili kutekeleza majukumu mbalimbali ya kiusalama kwa nchi hivyo kukamatwa kwa Kabendera
siyo jambo geni bali Idara inatimiza majukumu yake chini ya Sheria ya uraia wa
Tanzania sura ya 357 rejeo la 2002.
|
No comments:
Post a Comment