Ahimiza vijana wajitokeze kwa wingi, aonya asasi za kiraia za kutoa elimu ya mpigakura zisijihusishe na ushabiki wa kisiasa
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua rasmi zoezi la uboreshaji wa Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura na kuwahimiza vijana waliotimiza miaka 18
wajitokeze kwa wingi kujiandikisha.
“Nitoe
rai kwa vijana wote wa Kitanzania waliotimiza umri wa miaka 18 au wale
ambao watatimiza umri huo ifikapo Oktoba, 2020 wajitokeze kwa wingi na
kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Hawa ndio
walengwa wakuu kwa sababu wanaingia kwa mara ya kwanza katika uchaguzi.”
“Ikumbukwe
kwamba, bila kujiandikisha hawataweza kutumia haki yao ya msingi ya
kuchagua viongozi wanaowataka. Hivyo, kujiandikisha kwao
kutawahakikishia ushiriki wao katika uchaguzi wa viongozi,” amesema
Waziri Mkuu.
Waziri
Mkuu ametoa rai hiyo leo, (Alhamisi, Julai 18, 2019) wakati akizindua
zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililofanyika
kwenye uwanja wa Mandela, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Waziri
Mkuu ambaye amewasili mkoani Kilimanjaro leo asubuhi kwa ziara ya
kikazi za siku nne, ametumia fursa hiyo kuwasisitiza vijana na wale
wanaorekebisha taarifa zao kwamba hakuna mtu atakayeruhusiwa kupiga kura
katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kama hajajiandikisha katika Daftari
la Kudumu la Wapiga Kura ama hana kadi ya mpigakura.
Amesema
zoezi hilo ambalo limeanza leo, linafanyika kwa mara ya kwanza tangu
kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Amesema litafanyika nchi
nzima na linatarajiwa kukamilika Machi, 2020.
“Watakaohusika
awamu hii ni wapigakura waliotimiza miaka 18 hivi karibuni, wale
watakaotimiza miaka 18 wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 2020, waliohama
kata au Jimbo na kuhamia maeneo mengine ya kiuchaguzi, waliopoteza kadi
au kadi zao kuharibika, wanaohitaji kurekebisha taarifa zao mfano majina
ambayo hapo awali yalikuwa yamekosewa sambamba na kuwaondoa wapiga kura
waliopoteza sifa kama vile kufariki,” amesema.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu ameziasa asasi za kiraia ambazo zimepewa
vibali vya kutoa elimu ya mpigakura, zijiepushe na ushabiki wa kisiasa
na badala yake zizingatie mwongozo wa elimu ya mpigakura uliotolewa na
Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
“Nimeambiwa,
Tume imetoa vibali vya kutoa elimu ya mpigakura kwa baadhi ya Asasi za
Kiraia. Rai yangu kwa asasi zilizopata vibali hivyo ni kuendelea kutoa
elimu hiyo kwa wananchi kwa kuzingatia mwongozo wa uliotolewa na Tume ya
Taifa ya Uchaguzi. Niendelee kuwaasa pia kutohusisha ushabiki na
mijadala ya kisiasa muda wote mtakapokuwa mkitoa elimu hiyo,” amesema.
Amesema
ana imani kuwa wananchi wakipata elimu kuhusu uboreshaji kama
inavyoendelea kutolewa, basi watahamasika kutumia haki yao ya kikatiba
ya kujiandikisha katika daftari hilo na hatimaye kushiriki katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Amesema
zoezi la majaribio ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
katika Kata ya Kibuta katika Halmshauri ya Wilaya ya Kisarawe na Kata ya
Kihonda katika Halmashauri ya Manispaa ya Wilaya ya Morogoro,
lilifanyika kwa mafanikio makubwa.
Mapema,
akitoa maelezo kuhusu zoezi hilo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi, Jaji Semistocles Kaijage, alisema katika zoezi la sasa, Tume
itaendelea kutumia teknolojia ya kielektroniki ya Biometric (BVR) na
imeandaa BVR kits 3,000.
Alisema
kwa Tanzania Bara, Tume hiyo imeongeza vituo vya uandikishaji kutoka
36,549 vilivyotumika mwaka 2015 hadi kufikia 37,407; kutokana na zoezi
la uhakiki wa vituo vya kuandikisha wapiga kura lililoendeshwa mwaka
jana.
“Kutokana
na hilo, vituo 6,208 vilibadilishwa majina, vituo 817 vimehamishwa
kutoka mtaa mmoja au kijiji kimoja na kwenda kingine na vituo 19
vilihamishwa kutoka kata moja kwenda kata nyingine.”
“Kwa
upande wa Zanzibar, vituo vya uandikishaji vimeongezeka kutoka 380 na
kufikia 407. Kwa sasa kila kijiji au mtaa, utakuwa na kituo kimoja,”
alisema.
Alisema
vituo vya uandikishaji vitafunguliwa saa 2 asubuhi hadi saa 12 jioni na
zoezi la uboreshaji litafanyika kwa siku saba kwa kila kituo cha
kujiandikisha iwe ni Tanzania Bara au Zanzibar.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akibonyeza kitufe, wakati akizindua zoezi la
uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, katika viwanja vya
Mandela mkoani Kilimanjaro Julai 18.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu).
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akishuhudia kijana Nehemia Mhando, akiandikishwa
kwenye daftari la kudumu la wapiga kura, katika uzinduzi wa daftari
hilo, uliyofanyika kwenye viwanja vya Mandela mkoani Kilimanjaro Julai
18.2019.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akimkabidhi kadi ya kupigia kura, kijana Nehemia
Mhando, baada ya kuzindua daftari la kudumu la wapiga kura, katika
uzinduzi wa daftari hilo, uliyofanyika kwenye viwanja vya Mandela mkoani
Kilimanjaro Julai 18.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Walemavu, Jenista
Mhagama, katika uzinduzi wa daftari la kudumu la wapiga kura,
uliyofanyika kwenye viwanja vya Mandela mkoani Kilimanjaro Julai
18.2019.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiketa jambo na Mwenyekiti wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi, Jaji Semistocles Kaijage, kabla ya uzinduzi wa
daftari la kudumu la wapiga kura, uliyofanyika kwenye viwanja vya
Mandela mkoani Kilimanjaro Julai 18.2019.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye
Walemavu, Jenista Mhagama, akizungumza na wananchi waliyohudhuria katika
uzinduzi wa daftari la kudumu la wapiga kura, uliyofanyika kwenye
viwanja vya Mandela mkoani Kilimanjaro Julai 18.2019.
No comments:
Post a Comment