Waziri
wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza na Mkurugenzi Mkaazi wa
Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) Tanzania Ndg Andy
Karas katika Ofisi za Wizara ya Kilimo Jijini Dar es salaam, leo Tarehe 1
Julai 2019. (Picha Zote Na Mathias Cnal, Wizara ya Kilimo)
Waziri
wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiwa na picha ya pamoja na mratibu
wa mradi wa maboresho ya sera (ASPIRES) Prof David Nyange katika Ofisi
za Wizara ya Kilimo Jijini Dar es salaam, leo Tarehe 1 Julai 2019.
Waziri
wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na
Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa
(USAID) Tanzania Ndg Andy Karas katika Ofisi za Wizara ya Kilimo Jijini
Dar es salaam, leo Tarehe 1 Julai 2019. Wengine pichani ni Naibu
Mkurugenzi wa ofisi ya ukuaji wa uchumi (USAID) Tanzania Bi Michelle
Corzine, na Mtaalamu wa sera katika usimamizi wa miradi Ndg Semaly
kisamo
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo - Dar es salaam
Waziri
wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) leo Tarehe 1 Julai 2019 amekutana na
kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Marekani la
Maendeleo ya Kimataifa (USAID) Ndg Andy Karas katika Ofisi za Wizara ya
Kilimo Jijini Dar es salaam.
Katika
mazungumzo hayo Mhe Hasunga amemueleza Mkurugenzi huyo kuwa Wizara ya
Kilimo imejipanga kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo ili
kuondokana na dhana ya kilimo cha kujikimu na kuhamia katika kilimo cha
kibiashara. Waziri Hasunga alisema kuwa ili kuongeza tija katika Kilimo,
Wizara yake imejipanga kuimarisha utafiti.
Alisema
kuwa maendeleo ya kilimo yanategemea zaidi utafiti hususani wa udongo
vilevile kubaini teknolojia bora itakayo pelekea kukisogeza kilimo
katika hatua kubwa ya mafanikio na kimageuzi.
Amesema
kuwa pamoja na mambo mengine wizara ya kilimo pia imejipanga katika
kuongeza thamani ya mazao ya kilimo kuliko kusafirisha pasina kuongeza
thamani.“Tukiongeza
thamani ni wazi kuwa uchumi utapanda, lakini zaidi ajira ziataongezeka
kwa wananchi, tutakuwa na Pato zuri la kigeni sambamba na utambulisho wa
nchi” Alikaririwa Mhe Hasunga
Kuhusu
sekta ya umwagiliaji Mhe Hasunga alisema kuwa Tanzania ina jumla ya
Hekta zaidi ya Milioni 29 zinazofaa katika umwagiliaji lakini ni hekta
475,000 ndizo ambazo zimefanyiwa kazi.
“Kwa
maana hiyo kuna fursa kubwa katika umwagiliaji hivyo ninyi kama wadau
kadhalika natoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kuwekeza katika
umwagiliaji” Alisema
Kuhusu
Lishe Waziri Hasunga alisema kuwa wizara imeendelea kuweka hamasa kwa
wakulima ili kuwa na lishe bora. Aliongeza kuwa watanzania wanapaswa
kuwa na utamaduni wa kula vizuri ili kuondokana na magonjwa mbalimbali
kama vile utapiamlo.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya
Kimataifa (USAID) Ndg Andy Karas ameipongeza serikali ya awamu ya tano
inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John
Pombe Magufuli kwa mikakati madhubuti ya kuimarisha sekta ya kilimo
nchini.
Aidha,
Karas amemuomba Waziri wa Kilimo kuteua watu wawili kutoka wizarani
watakaokuwa kiungo muhimu baina ya serikali na miradi ya USAID sambamba
na mtu atakayeratibu mikutano ya wadau wa maendeleo.
No comments:
Post a Comment