Matokeo chanyA+ online




Tuesday, August 13, 2019

BI.MWANAMWEMA SHEIN ASISITIZA SUALA MATUNZO KWA WAZEE NA WATOTO

Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Mwanamwema Shein amesema suala la matunzo ya wazee na ulezi wa watoto linaendeana na utekelezaji wa Sera na Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Amesema hayo katika hafla ya utoaji wa zawadi ya sikukuu ya Eid el Hajj kwa wazee na watoto wanaoishi katika nyumba za Wazee Weleze na Sebleni pamoja na vituo vya kutunzia watoto vya SOS na Mazizini, alizozianda kwa kushirikiana na na Mke wa Makamo wa Pili wa Rais Zanzibar Asha Suleiman Idd.

Akizungumza kwa niaba ya Mama Mwanamwema, Waziri wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake wa watoto Moudline Castico alisema katika kufanikisha malengo hayo Serikali inatumia zaidi ya shilingi Milioni 200 kwa mwezi, ikiwa ni malipo ya Pensheni jamii kwa
wazee wenye umri wa miaka 70 na kuendelea.

Sambamba na hilo, alisema Serikali inaendelea kuyafanyia matengenezo majengo ya makaazi ya wazee wasiojiweza ili kuleta ustawi bora wa maisha yao, pamoja na kuwapatia huduma bure za afya ikiwa ni kuthamini mchango mkubwa walioutowa wakati wa ujana wao.

Aidha alisema Serikali inakusudia kuifanya sheria dhana ya Pensheni jamii, ili kuepuka athari za mabadiliko ya uongozi hapo baadae. Alisema viongozi hao wameamuwa kutowa zawadi hizo ili kuhakikisha wazee na watoto ha wanafurahi na kujumuika pamoja na wananchi wengine.

Waziri Castico, aliwataka wazee hao kupitia sikukuu hiyo kuendelea kuliombea dua Taifa, ili liweze kuepukana na athari zitokazo na majanga mbali mbali.

Aidha, aliwataka wazazi na walezi kuzingatia malezi bora na maadili ya ya watoto wao kwa kujiepusha na vitendo vya kikatili na udhalilishaji.

Alisema tukio la hivi karibuni la utupaji wa mtoto Kisiwani Pemba na hatimae kuokotwa na mbwa, linathibitisha kwa kiasi gani jamii isivyojali na kuthamini malezi na mtunzo ya watoto.

Alieleza kuwa Serikali imefanya juhudi kufanikisha upatikanaji wa Mashine ya uchunguzi wa Vinasaba (DNA) ili kukabiliana na wimbi la matukio mbali mbali ya udhalilishaji.

Mapema, Mkurugenzi wa kituo cha Kulelea watoto cha SOS, Asha Salim aliwashukuru viongozi hao kwa muendelezo wao wa kila mwaka na kuwatakia kheria na afya njema katika amisha yao.

Alisitiza umuhimu wa wazazi na walezi katika utunzaji wa watoto wao na kuviomba vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na taasisi nyengine zinazohusika na haki za watoto kuwachukulia hatua wote watakaobainika kuhusika na vitendo vya udhalilishaji na utupaji watoto.

Nae, mtoto Salama Abdalla Ali wa kituo cha kulelea watoto Mazizini, kwa niaba ya watoto wenzake aliwashukuru viongozi kwa imani na mapenzi makubwa kwao na kuwakumbuka mara kwa mara, hatua aliyosema inawapa faraja.

No comments:

Post a Comment