Matokeo chanyA+ online




Monday, August 12, 2019

SERIKALI YAWATAKA WANUNUZI WA PAMBA WAONGEZE KASI

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wanunuzi wa zao la pamba katika maeneo mbalimbali nchini wahakikishe wanaongeza kasi ya ununuzi wa zao hilo ili wakulima waweze kupata fedha zao kwa wakati.

Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga pamoja na Manaibu Waziri wake kubaki katika mikoa yote inayolima zao la pamba hadi wakulima wote watakapolipwa fedha zao na kuhakikisha pamba yote iliyomo mikononi mwa wakulima inauzwa.

Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Agosti 8, 2019) wakati alipotembelea Chama cha Msingi cha Itemelo kilichoko eneo la Dutwa wilayani Bariadi, Simiyu kwa ajili ya kujionea mauzo ya zao la pamba.

Waziri Mkuu amesema ataendelea kusimamia mwenendo wa zao hilo kwa ukaribu lengo likiwa kuona wakulima wananufaika kwa kupata tija. “Ilani ya CCM ya 2015/2020 inasisitiza kilimo na inataka wakulima wapate masoko ya uhakika na tunalitekeleza jambo hilo na pamba yote itanunuliwa.”

Amesema Serikali inataka kuona pamba yote iliyoko kwa wakulima inatoka ili wakulima waweze kulipwa fedha ambazo zitawawezesha kujikimu kimaisha pamoja na kununua pembejeo kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa AMCOS wahakikishe wanawatambua wakulima kwa majina, maeneo wanayoishi pamoja na ukubwa wa mashamba yao ili waweze kuagiza pembejeo kulingana na mahitaji halisi.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewasihi wakulima kufungua akaunti katika taasisi mbalimbali za kifedha lengo likiwa ni kuhifadhi vizuri fedha wanazozipata kutokana na mauzo ya pamba ili ziweze kuwasaidia baadaye.

Pia, Waziri Mkuu amewasisitiza wakulima hao waendelee kutunza vizuri pamba yao na kuipeleka ghalani ikiwa katika hali nzuri ya usafi na ubora wa hali ya juu, kwani kwa sasa pamba ya Tanzania inasifika kwa ubora katika soko la dunia.

Kwa upande wa masoko hususan ya pamba, Waziri Mkuu aliwasisitizia wananchi wa Dutwa na Watanzania kwa ujumla kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. Magufuli inaendelea kuhakikisha uwepo wa masoko ya uhakika wa mazao yote hususan yale ya kimkakati.

Pia, Waziri Mkuu ameongeza kuwa moja ya agenda muhimu ya ziara yake ya Kiserikali aliyoifanya nchini Misri mwezi Julai 2019 ilikuwa ni kutafuta masoko ya uhakika ya mazao ya Tanzania likiwemo na zao la pamba.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally alipokaribishwa kuwasalimu wananchi alimshukuru Waziri Mkuu kwa kutoa msukumo katika ununuzi zao la pamba. Aidha alimuomba Waziri Mkuu aongeze msukumo zaidi ili wakulima walipwe fedha zao kwa wakati.

Naye,Waziri wa Kilimo Hasunga amesema kuwa hali ya malipo kwa wakulima wa zao la pamba kwa sasa ni ya kuridhisha kwa kuwa wakulima katika maeneo mbalimbali wameanza kulipwa.

Pia Waziri huyo amemuahidi Waziri Mkuu kwamba wataendelea kubakia katika mikoa inayolima pamba kwa ajili ya kufuatilia mwenendo wa mauzo ya pamba ili kuhakikisha wakulima wote wanalipwa fedha zao kwa wakati.

Kuhusu suala la makato ya fedha za pembejeo ambazo wakulima wanalalamikia kukatwa kiasi kikubwa kuliko kiwango halisi wanachostahili, Waziri huyo wa Kilimo amesema atalishughulikia.

Aidha,Mbunge wa jimbo la Bariadi, Andrew Chenge amesema amefanya ziara katika kata 20 kati ya 30 kwenye jimbo hilo na changamoto kubwa ya wananchi ni mauzo ya pamba. “Ujio wa Waziri Mkuu umeleta manufaa kwani wanunuzi wameanza kuja kwa kasi”.

Mbunge huyo amemuomba Waziri Kuu awafikishie salamu zao kwa Rais Dkt. John Magufuli kwamba wanamshukuru kwa namna anavyowajali wakulima mbalimbali nchini wakiwemo na wa zao la pamba.

Kwa upande wake, Mbunge wa jimbo la Itilima, Njalu Silanga ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Nsangali ambayo inanunua pamba amemuahidi Waziri Mkuu kwamba ifikapo kesho (Ijumaa, Agosti 9, 2019) saa nane mchana atakuwa amelipa sh. milioni 135 zinazohitajika na amcos ya Itemelo ili kulipia deni la pamba iliyoko ghalani.

Awali, Katibu wa Amcos ya Itemelo, Lucas Ephraim alimuomba Waziri Mkuu awasaidie kuyahimiza makampuni mbalimbali yanayonunua yapeleke fedha kwa wakati ili kukidhi makisio tarajiwa.

Katibu huyo alisema chama chao kinahudumia vijiji vitano vikiwa na jumla ya wakulima 2,665 wa pamba wenye jumla ya ekari 9,675. Pia chama chao kinahitaji sh. milioni 135.139 ili kulipia deni la pamba ambayo iko ghalani.
PMO_2269
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akishuhudia kazi ya kupima pamba kwa njia ya kielektroniki wakati alipokagua ununuzi wa pamba  katika Chama cha Ushirika  cha Msingi cha Itemelo  kilichopo eneo la Dutwa mkoani Simiyu, Agosti 8, 2019   Kulia ni  Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga na wa tatu Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka.

No comments:

Post a Comment