Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akiwasha rasmi umeme katika shule ya msingi Gararagua, iliyopo wilayani Siha, Mkoa wa Kilimanjaro akiwa katika ziara ya kazi, Agosti 25, 2019 |
Naibu
Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ametoa onyo kali kwa Mkandarasi Urban &
Rural Engineering, ambaye anatekeleza mradi wa umeme vijijini awamu ya tatu
mkoani Kilimanjaro, kwa kumwambia asiijaribu serikali kwa kutikisa kibiriti
kwani njiti zimejaa na kitawaka.
Alitoa
onyo hilo kwa nyakati tofauti Agosti 25, 2019 akiwa katika ziara ya kazi kwenye
Wilaya za Hai na Siha, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi na
viongozi wao kuwa kasi ya mkandarasi huyo hairidhishi.
Akizungumza
katika mkutano na wananchi wa Hai, Naibu Waziri Mgalu alikiri mbele yao kuwa
utendaji kazi wa mkandarasi husika unasuasua na zaidi ameonesha vitendo vya
utovu wa nidhamu kwa serikali kwa kutoitikia wito alipoitwa kushiriki kwenye
ziara hiyo pasipo kutoa sababu yoyote.
Akielezea
zaidi, Naibu Waziri alisema yeye binafsi alijaribu kuwasiliana na mkandarasi
huyo kwa njia ya simu pasipo mafanikio na hata ujumbe mfupi wa maandishi aliomtumia
kumtaka apokee simu, haukujibiwa; kitendo ambacho alikiita ni dharau.
“Sasa mimi nataka nitoe salamu kwake. Mkandarasi Urban
& Rural Engineering naona unatikisa kibiriti, unataka ujue kama kina njiti
au hakina, na kama njiti zimejaa au zina baruti. Nataka nikwambie kibiriti
kimejaa, njiti zina baruti na kitawaka.”
“Ulichokifanya ni dharau na unatupelekea tufanye
maamuzi ya kuanza mapitio; na ni kweli nathibitisha ameshindwa kazi,” alisema
Naibu Waziri.
Kufuatia hali hiyo, alimwagiza Msimamizi wa Mradi
husika kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kumjulisha mkandarasi huyo
kwenda Dodoma mara moja kushiriki katika kikao kitakachofanya mapitio ya suala
hilo ili ikibidi hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.
“Kama ameshindwa kazi, tutawapatia wakandarasi wengine
au hata TANESCO wanaweza kumalizia kazi husika.”
Awali, Meneja wa TANESCO wa Mkoa wa Kilimanjaro,
Mhandisi Mahawa Mkaka, alimweleza Naibu Waziri kuwa, Mradi wa Umeme Vijijini
Awamu ya Tatu mkoani Kilimanjaro unagharimu kiasi cha shilingi za kitanzania
takribani bilioni 12.
Alisema, Mradi unahusisha ujenzi wa kilomita 150 za
msongo wa umeme wa kilovoti 33, ujenzi wa kilomita 334 za msongo wa umeme wa
kilovoti 400 na ufungaji wa mashine umba (transfoma) 132 na kwamba unatarajiwa
kuunganishia umeme jumla ya wateja 3,572 katika vijiji 75 ndani ya mkoa.
Aliongeza kuwa, kwa ujumla utekelezaji wa mradi husika
mkoani humo umefikia asilimia 43 hadi sasa.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri aliwasha umeme katika
shule za msingi za Roo na Msamadi zilizopo wilayani Hai, pamoja na eneo la
viwanda Mwangaza na shule ya msingi Gararagua wilayani Siha. Pia, alizungumza
na wananchi wa Kata ya Ngarenairobi wilayani Siha. Na Veronica Simba – Kilimanjaro
No comments:
Post a Comment