Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amepokea kwa mshtuko na
masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya watu zaidi ya 60 na majeruhi takribani
70 walioungua kwa moto baada ya lori lililokuwa na shehena ya mafuta kupata
ajali na kisha kulipuka moto Mjini Morogoro.
Ajali hiyo
imetokea leo tarehe 10 Agosti, 2019 majira ya saa 2 asubuhi ambapo lori hilo
lililokuwa linatoka Dar es Salaam limepinduka jirani na Kituo Kikuu cha Mabasi
cha Msamvu baada ya dereva wa lori kumkwepa mwendesha pikipiki na kisha mafuta
yaliyokuwa yakimwagika kushika moto na kuunguza watu waliokuwa wanayachota.
Mhe. Rais Magufuli
ametoa pole kwa familia, ndugu, marafiki na wote waliopoteza jamaa zao katika
ajali hii na pia amewaombea majeruhi wapone haraka.
“Nimeumia sana kusikia
idadi kubwa ya Watanzania wenzetu waliopoteza maisha katika ajali hii, natoa
pole kwa wote walioguswa na vifo hivi hasa familia za Marehemu wote, nawaombea
Marehemu wapumzike mahali pema peponi na majeruhi wote wapone haraka”
amesema Mhe. Rais Magufuli na kumuagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe
Steven Kebwe kufikisha salamu zake za pole kwa familia na wote walioguswa na
vifo hivyo.
Mhe. Rais Magufuli
ameagiza Wizara zote zinazohusika kushughulikia ajali hii na ametaka Hospitali
ya Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili
kuhakikisha majeruhi wote wanapatiwa matibabu ili kuokoa Maisha yao.
Aidha, Mhe. Rais
Magufuli ameelezea kusikitishwa kwake na vitendo vya watu kuvamia magari
yanayopata ajali kwa lengo la kujipatia bidhaa mbalimbali zilizobebwa na magari
hayo na ametaka vitendo hivyo vikome.
“Baadhi ya magari haya
yanabeba mafuta ambayo ni hatari kama ilivyotokea Morogoro, yapo magari
yanabeba kemikali za sumu, yapo magari yanabeba milipuko nakadhalika, nawaomba
sana tuache tabia hii” amesisitiza Mhe. Rais
Magufuli.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es
Salaam
10 Agosti,
2019
No comments:
Post a Comment