Serikali
imetoa rai kwa kampuni zinazotandaza mfumo wa nyaya za umeme kwenye majengo
maarufu kama ‘wiring’ kuangalia uwezekano wa kupunguza gharama zao hususan kwa
wananchi walioko vijijini ili waweze kuzimudu.
Rai
hiyo ilitolewa Agosti 28 mwaka huu na Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu,
wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuhitimisha ziara yake ya
siku mbili mkoani Morogoro.
Alisema
kampuni hizo zinatakiwa kutambua kuwa serikali imezitengenezea fursa kutokana
na kupeleka miundombinu ya umeme maeneo ya vijijini, la sivyo wasingepata
wateja hivyo nazo zinawajibika kuangalia hali za wananchi hao kwa kuiga mfano
wa serikali ambayo imewapunguzia gharama za kuunganisha umeme kutoka shilingi
177,000 hadi kufikia 27,000 tu.
“Hizi
bei za laki mbili hadi tatu, kwakweli siyo rafiki kwa wananchi wengi wa
vijijini ambao serikali imewapunguzia gharama za kuunganishiwa umeme kutokana
na uwezo wao. Sasa hawa wenzetu watafakari, itafika mahala umeme utafika,
wananchi wanaounganishwa ni wachache na wao watakosa biashara.
Naibu
Waziri aliiomba Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), kuangalia namna
ya kusaidia jambo hilo. “Hatuna nia ya kuwadhibiti moja kwa moja, lakini
waangalie ili bei ziendane na hali za watanzania vijijini pamoja na malengo ya
kiserikali,” alifafanua.
Katika
hatua nyingine, Naibu Waziri aliwataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya
umeme vijijini nchini kote kuongeza kasi na kusema kuwa serikali haitawaongezea
muda bali itaendelea kusimamia makubaliano baina yao, kwamba ifikapo Desemba
mwaka huu, wawe wamekamilisha ujenzi wa miundombinu husika na kubaki kazi za
kuwaunganisha wateja.
Aidha,
alitoa rai kwa wananchi vijijini ambao wameshafikiwa na miundombinu ya umeme
wachangamkie fursa kwa kulipia shilingi 27,000 tu ili waunganishwe na kuutumia
umeme kujiletea maendeleo.
“Wakati
mwingine inatunyong’onyesha tunapokuta baadhi ya maeneo watu wana uhitaji
mkubwa wa umeme lakini miundombinu haijawafikia na sehemu nyingine mradi
umefika, watumiaji wachache.”
Vilevile,
Naibu Waziri aliwasisitiza mameneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),
ngazi ya wilaya na mikoa, kuendelea kutekeleza agizo la serikali la
kuwaunganishia umeme wananchi wa vijijini kwa bei ya shilingi 27,000 tu pasipo
kuwalipisha nguzo na vifaa vingine.
Pia,
alitoa onyo kwa mameneja kuacha kuwajibu wananchi wanaopeleka maombi ya
kuunganishiwa umeme kwa gharama iliyoainishwa na serikali, kuwa bado hawajapata
waraka husika. Alisema, Waraka wameshaupata na umeainisha gharama hiyo itumike
kwa maeneo ya vijijini.
“Ni
marufuku hiyo lugha ya kwamba waraka haujafika, au kwamba hiyo ni siasa, au
kwamba hii ni ndani ya mita 30 au 40,” alisisitiza.
Alisema,
suala la msingi wanalopaswa kufanya mameneja hao ni kuwaelewesha wananchi
kwamba maombi yao yamepokelewa na wanapanga mikakati ya kuwafikishia huduma ya
umeme maana ni wajibu wao kutumia ubunifu na kujipanga namna ya kuwafikia
wateja, hususan wenye mahitaji ya nguzo nyingi.
Aliwahakikishia
watanzania kuwa agizo la kulipia shilingi 27,000 tu kuunganishiwa umeme
vijijini linatekelezeka na kwamba wale wanaohitaji nguzo nyingi wanapangiwa
mpango wa kufikiwa, bali wote watahudumiwa kwa bei hiyo.
Kwa
upande wake, Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Lawrence Maro,
alisema ofisi yake imepokea maelekezo yote ya Naibu Waziri na kuahidi kuwa
watayatekeleza kikamilifu.
“Tangu
agizo la kuwaunganisha wateja wa vijijini kwa shilingi 27,000 litolewe,
tumeshaunganisha wananchi 3,195 katika kipindi cha mwezi Mei, Juni na Julai
mwaka huu. Tunaendelea na zoezi hilo, hivyo wananchi wenye uhitaji njooni
mtuone na tutawahudumia,” alisema.
Katika
ziara hiyo ya siku mbili, Naibu Waziri aliwasha umeme katika vijiji kadhaa
pamoja na kuzungumza na wananchi wa maeneo ambayo hayajafikiwa na miundombinu
ya umeme ambapo aliwaeleza mikakati iliyopangwa na serikali kuwafikishia huduma
hiyo. Na Veronica Simba – Morogoro
No comments:
Post a Comment