Waziri wa
Nishati, Dkt. Medard Kalemani amemuagiza Meneja wa Shirika la umeme Tanzania
(TANESCO), Mkoa wa Tabora, kuwa vijiji vyote vinavyozunguka mradi wa ujenzi wa kituo
cha kupoza umeme cha Urambo, vipatiwe umeme ndani ya miezi Sita.
Alisema hayo Agosti
24, 2019 wakati alipofanya ukaguzi kwenye mradi wa Ujenzi wa njia ya
kusafirisha umeme kutoka Urambo, Tabora hadi Kigoma na kuzungumza na wananchi
katika kijiji cha Uhuru kata ya Vumilia wilayani humo.
Akizugumza na
wanachi wa kijiji hicho, Waziri Kalemani alisema “huwezi ukajenga kituo cha
kupoza hapa, halafu vijiji vilivyozunguka hapa visiwe na umeme, kwahiyo vijiji
vyote vinavyozunguka kituo hiki natoa miezi Sita viwe vimeunganishiwa umeme.”
Aidha, Dkt.
Kalemani aliwapongeza wananchi wa Wilaya hiyo kwa uvumilivu wao katika kipindi
chote kwa kutopata umeme wa uhakika na kueleza kuwa “mmehangaika miaka
mingi lakini, Serikali yenu ni sikivu ndiyo maana sasa inaleta umeme imara unaotabirika,
na ninampongeza sana Mheshimiwa Rais Magufuli kwa kutoa fedha za kutosha za
kujenga mradi huu.”
Vilevile Dkt.
Kalemani alisema kukamilika kwa mradi huo kutaokoa pesa nyingi zinazotumika
kununua mafuta kwa ajili ya kuendeshea mitambo ya umeme.
Alitoa mfano
kuwa, Mkoa wa Kigoma unatumia takribani shilingi bilioni 1.1 kwa mwezi
kuendesha mitambo ya mafuta ambapo kwa mwaka inatumika bilioni 13.2 hivyo umeme
wa gridi utaokoa fedha hizo.
Alieleza kuwa,
mradi huo wa njia ya kusafirisha umeme unatekelezwa
na TANESCO wenyewe na hawatatumia wakandarasi wa nje ya nchi.
Katika ziara
hiyo, Dkt Kalemani aliwasha umeme katika kijiji cha Madundulu tarafa ya Usoke,
wilayani Urambo.Na Hafsa Omar, Tabora
No comments:
Post a Comment