Naibu
Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ametoa namba yake ya simu ya mkononi kwa
wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro na kuwaelekeza ‘wambipu’ ili awapigie na
kutatua kero husika, endapo wataambiwa kulipia nguzo, nyaya au mita wakati
wakipeleka maombi ya kuunganishiwa umeme maeneo ya vijijini.
Ametoa
onyo kali kwa mameneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ngazi ya Wilaya
na Mkoa ambao watakaidi agizo la serikali linaloelekeza kuwa wananchi wote wa
vijijini waunganishiwe umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 tu pasipo kulipia
kifaa chochote ikiwemo nguzo, nyaya au mita.
Alikuwa
akizungumzia yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika sekta ya nishati,
kwenye Kongamano la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mkoa wa Kilimanjaro, leo,
Agosti 24, 2019, ambalo lililenga kumpongeza Rais John Pombe Magufuli kwa kazi
nzuri anazofanya.
“Rais
Magufuli alisema tupunguze gharama za kuunganishia wananchi umeme vijijini
kutoka shilingi 177,000 hadi 27,000 tu. Atakayekwenda TANESCO akashindwa
kuunganishwa kwa bei hiyo au akaambiwa lipia nguzo, lipia waya, lipia mita;
Namba yangu ni 0652558010. Nibipu, nitakupigia,” alisema huku akishangiliwa na umati wa wananchi.
Akitoa takwimu za waliounganishiwa umeme vijijini,
mkoani Kilimanjaro kwa gharama hiyo ya shilingi 27,000 tangu agizo hilo
lilipoanza kutekelezwa mwezi Mei mwaka huu, amesema mpaka sasa idadi imefikia
5,000 huku waliounganishwa kwa mwezi Julai pekee ni zaidi ya watu 2,000.
Amesema Mkoa wa Kilimanjaro unaongoza Tanzania kwa
kuwa na umeme katika maeneo mengi ambayo ni asilimia 87.
“Mkoa una Kata 148 ambazo zote zina umeme. Una vijiji
519 ambavyo kati yake, 453 vina umeme. Bado vijiji 66 tu ambavyo vipo wilaya ya
Hai (5), Siha (7), Rombo (8), Mwanga (4), Moshi (22) na Same (20).
Amesema, kati ya vijiji 66 vya Mkoa wa Kilimanjaro
ambavyo bado havijaunganishiwa umeme, vitabaki 35 kufikia Desemba mwaka huu na
kati ya hivyo, serikali imeiagiza TANESCO kuchukua vijiji 18 ili iviunganishe hivyo
Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili (REA III – 2), utaunganisha
vijiji 17 tu vitakavyokuwa vimesalia.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mgeni Rasmi, Naibu
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, pamoja na
mambo mengine, amempongeza Rais Magufuli kwa kuwapa nafasi za uongozi wanawake
ambao wameonesha kuwa wanaweza, akitolea mfano wa Makamu wa Rais, Mama Samia
Hassan na Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu.Na Veronica Simba – Kilimanjaro
No comments:
Post a Comment