Maji ni hitaji muhimu
sana katika uhai wa mwanadamu na viumbe wengine na ndiyo maana Maendeleo ya
kiuchumi ya nchi yoyote duniani yawe ya viwanda, kilimo na kadhalika
yanategemea maji.
Lengo namba sita la
Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2015-2030 linaweka msisitizo wa
upatikanaji wa huduma za maji safi na salama na usafi wa mazingira kwa wote
ikienda sambamba na ulinzi wa rasilimali za maji na miundombinu ya usambazaji
maji.
Wakati mahitaji ya
maji yanaongezeka kutokana na ongezeko la idadi ya watu na kukua kwa shughuli
za kiuchumi na kijamii, maeneo kame yameendelea kuwa kame zaidi na matukio ya
mafuriko yanaongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Inaelezwa kuwa zaidi
ya watu bilioni 2.1 duniani hawapati maji safi na salama na kati ya hao, watu
milioni 844 hawapati huduma za msingi za maji ya kunywa, ambapo kati yao zaidi
ya watu milioni 340 wanatoka katika Bara la Afrika.
Hali hiyo inaonesha
jitihada zaidi zinahitajika katika kuwekeza na kuendesha mindombinu ya huduma
za maji kwa ajili ya kuongeza idadi ya watu wanaopata huduma za majisafi na
usafi wa mazingira ili kuendana na kasi ya mahitaji ya maji na malengo ya nchi
na ya Umoja wa Mataifa.
Katika Tanzania mahitaji
ya maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali kama vile majumbani, umwagiliaji,
viwanda na mazingira ni wastani wa mita za ujazo bilioni 40 kwa mwaka kati ya
mita za ujazo bilioni 126 kwa mwaka zilizopo.
Mradi wa Maji |
Aidha makadirio
yameonesha kuwa mahitaji ya maji yataongezeka kufikia wastani wa mita za ujazo
bilioni 57 kwa mwaka ifikapo mwaka 2035 na kutokana na mwenendo wa kuongezeka
kwa mahitaji ya maji nchini, Serikali imeimarisha ulinzi wa rasilimali za maji
ili kulifanya Taifa lisikumbwe na uhaba wa maji katika siku za usoni katika
maeneo ya mijini na vijijini.
Akiwasilisha Hotuba
ya Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2019/2020, Waziri wa
Maji Prof. Makame Mbarawa anasema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali
imeendelea kutekeleza miradi ya maji mijini na vijijini kwa kujenga miradi
mipya, kukarabati na kupanua miradi iliyopo kwa kutumia vyanzo vya maji vya
visima virefu na vifupi, mabwawa, chemchemi, mito na maziwa.
Prof. Mbarawa anasema
katika kipindi cha mwezi Julai 2018 hadi mwezi Desemba 2018, jumla ya miradi
198 yenye vituo vya kuchotea maji 4,719 imekamilika na kuwanufaisha wananchi
wapatao 1,252,731 waishio vijijini na miradi 653 inaendelea kutekelezwa na ipo
katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Waziri Mbarawa
anasema Serikali inaendelea na ujenzi wa miradi ya maji vijijini pamoja na
kutekeleza programu mbalimbali za kuimarisha uendeshaji na matengenezo ya
miradi hiyo ili iwe endelevu ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maji katika
vijiji 77 iliyofikia katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
“Katika mwaka
2018/2019, Serikali kwa kushirikiana na BADEA, OFID, Saudi Fund na Kuwait Fund
inatekeleza mradi wa maji Same-Mwanga–Korogwe wenye lengo la kuwapatia huduma
ya maji wakazi wa miji ya Same na Mwanga, pamoja na vijiji 38 vilivyopo
kandokando ya bomba kuu katika Wilaya za Same, Mwanga na Korogwe” anasema
Waziri Mbarawa.
Anaongeza kuwa mradi
huo unatekelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza inahusu ujenzi wa
miundombinu ya uzalishaji maji pamoja na miundombinu ya kusambaza maji katika
miji ya Same, Mwanga na vijiji tisa vilivyopo kandokando ya bomba kuu na awamu
ya pili itahusu kusambaza maji katika vijiji 29 vilivyobaki ambapo Serikali
inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa awamu hiyo.
Akifafanua zaidi
Prof. Mbarawa anaongeza kuwa awamu ya kwanza ya mradi umegawanywa katika
vipande vinne, kipande cha kwanza
kilichogharimu Dola za Marekani Milioni 41.36 kinahusu ujenzi wa miundombinu ya
kuzalisha maji, ulazaji wa bomba kuu la kusafirisha maji hadi kwenye tanki la
kuhifadhia maji, mtambo wa kusafisha maji pamoja na ujenzi wa matanki ya
kuhifadhi maji.
Prof. Mbarawa anasema
kuwa Serikali pia inatekeleza utekelezaji wa mradi wa maji wa Masoko uliopo
Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya ambao unahusisha ulazaji wa mtandao wa mabomba,
ujenzi 50 wa vidakio vya maji, matanki ya maji na vituo vya kuchotea maji.
Hatua za utekelezaji wa mradi zimegawanyika katika vipande vitano.
“Mradi wa maji Masoko
utakapokamilika utawanufaisha wananchi wapatao 19,624 wanaoishi katika vijiji
vya Bulongwe, Ngaseke, Igembe, Ntandabala, Lupando, Bujesi, Lufumbi, Nsyasa,
Ikama, Itagata, Busisya, Mbaka, Isabula, Lwifa na Nsanga”.
Aidha Ppof. Mbarawa
anasema mradi wa maji wa vijiji 100 vilivyopo kandokando ya bomba kuu la maji
kutoka Ziwa Victoria hadi miji ya Kahama na Shinyanga unaendelea kutekelezwa
chini ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya Kahama - Shinyanga
(KASHWASA), ambapo wamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo itahusisha vijiji
40 ambapo vijiji 33 vimefanyiwa usanifu.
Anaongeza kuwa kati
ya vijiji vilivyofanyiwa usanifu, ujenzi wa miradi kwenye vijiji 14 umekamilika
na kunufaisha wananchi wapatao 38,348. Vijiji hivyo ni Runele, Gatuli,
Nyashimbi, Magobeko, Kakulu, Butegwa, Nyang’homango, Ng'homango, Jimondoli,
Kadoto, Lyabusalu, Mwajiji, Ichongo na Bukamba.
Kuhusu mradi wa maji
wa Chiwambo uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi uliogharimu Shilingi
bilioni 4.49, ulikamilika mwezi Mei,
2018 ambapo unahudumia vijiji vijiji 30 vilivyopo Kata za Lulindi, Lupumbulu,
Namalenga, Chiungutwa, Sindano, Mchauru na Mbuyuni na utekelezaji wa mradi huo
ulihusisha ukarabati wa matanki na miundombinu ya maji iliyochakaa, ujenzi wa
matanki ya kuhifadhi maji.
Kwa mujibu wa Prof.
Mbarawa anasema Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais - TAMISEMI iliunda
Timu ya Wataalam kwa ajili ya kufanya mapitio ya usanifu wa kina wa mradi wa
maji Ntomoko uliopo katika vijiji vya Ntomoko-Fai na Makirinya Halmashauri ya
Wilaya ya Kondoa Mkoani Dodoma pamoja na vijiji vya Kinkima na Lusangi
vilivyopo Halmashauri ya Wilaya ya Chemba.
Anasema ili kuteleza
mradi huo mwezi Februari mwaka huu, Serikali ilisaini mkataba wenye thamani ya
Tsh Bilioni 2.27 na Mkandarasi tayari ameanza maandalizi ya utekelezaji wa
mradi huo ikiwa na pamoja na ujenzi wa matanki matatu, ununuzi wa pampu, ulazaji
wa mabomba ya kusafirisha maji pamoja na ujenzi wa chemba.
Serikali inaendelea
kutekeleza miradi mikubwa ya maji katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo itihada
zaidi zinahitajika katika kuwekeza na kuendesha mindombinu ya huduma za maji
kwa ajili ya kuongeza idadi ya watu wanaopata huduma za majisafi nchini.
Na Ismail Ngayonga
No comments:
Post a Comment