Kamati ya Ufundi ya
Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REB), imetoa muda wa siku 21
kwa Mkandarasi NIPO Group anayetekeleza miradi ya umeme vijijini mkoani Mwanza,
kufanya kazi zote zilizokuwa zimesimama, ikiwemo usimikaji wa nguzo takribani
1,800.
Akizungumza na
waandishi wa habari baada ya kikao kazi baina ya Bodi hiyo na Mkandarasi,
Oktoba 7, 2019 jijini Mwanza, Mwenyekiti wake, Mhandisi Styden Rwebangira alisema,
pia wamempa Mkandarasi husika siku saba kuwasilisha mpango kazi unaoainisha
namna atakavyotekeleza kazi ya usambazaji umeme katika eneo lake lote na
kukamilisha ifikapo mwishoni mwa Desemba mwaka huu, kama ilivyoagizwa na Waziri
wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.
Mhandisi Rwebangila
alisema, Bodi imelazimika kutoa maagizo hayo baada ya kufanya ziara ya siku
mbili mkoani humo na kubaini kuwa katika maeneo mengi kazi zimesimama huku
kukiwa hakuna vibarua wa mkandarasi kwenye maeneo ya kazi.
Hata hivyo, alisema
kuwa changamoto za Mkandarasi huyo ni ndogo ambazo zinaweza kutatuliwa kwa
urahisi na kwamba endapo atafuata maelekezo aliyopatiwa na Bodi, ataweza
kukamilisha kazi kwa wakati.
“Alianza kwa kasi
nzuri lakini hapa katikati akasimama. Tumemhoji na amekiri kuwa kazi zimesimama
kwa kuwa alikuwa na changamoto ya fedha iliyosababisha acheleweshe malipo ya
vibarua wake kwa takribani miezi mitatu; lakini ametuhakikishia kuwa
amekwishatatua changamoto hiyo na kwamba vibarua watarejea kazini ndani ya wiki
hii katika maeneo yote.”
Alisema, Bodi itarudi
kumkagua Mkandarasi huyo endapo ametekeleza maagizo yake baada ya siku 21 na
kwamba endapo atashindwa kutekeleza, hatua za kimkataba zitachukuliwa dhidi
yake ikiwa ni pamoja na kusitisha mkataba wake na kumwondolea sifa za kupewa
kazi nyingine za aina hiyo na serikali.
Akizungumzia zaidi
changamoto za kiutawala na kiusimamizi katika kampuni kadhaa za wakandarasi,
Mhandisi Rwebangila alisema Bodi imebaini tatizo hilo katika kampuni nyingi
ambazo zimeungana ili kufanya kazi pamoja.
Akifafanua, alisema,
kampuni hizo zinapoomba kazi zinapewa kwani zinakuwa zimejieleza kuwa
zinaunganisha nguvu ili kutekeleza kazi kwa ufanisi zaidi lakini baada ya
kupewa kazi, zinatengana na kugawana kazi hivyo kupunguza ufanisi.
Alisema, kufuatia
hali hiyo, Bodi imekuwa ikizishauri kampuni zilizoungana kuhakikisha hazigawani
kazi bali zinatakiwa kutekeleza kwa pamoja ili kuwa na ufanisi.
Aidha, alisema kuwa,
maagizo yaliyotolewa na Bodi kwa Mkandarasi yanahusu pia Mkoa wa Arusha ambao
ni eneo lingine analotekeleza kazi.
Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REB), ikikagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini wilayani Misungwi, Mkoa wa Mwanza, Oktoba 5, 2019 |
Kwa upande wake,
Mkandarasi husika, aliahidi kuwa amejipanga kutekeleza yale yote aliyoagizwa na
Bodi, na kwamba atakamilisha kazi husika kwa wakati kama ilivyoelekezwa na
serikali.
Akizungumzia mpango
wa serikali katika utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, Kaimu Mkurugenzi wa
Huduma za Ufundi kutoka REA, Mhandisi Jones Olotu, alisema ifikapo Januari
2020, Mzunguko wa Pili wa Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Kwanza, unatarajiwa
kuanza.
Alisema katika
Mzunguko huo wa Pili, vijiji vyote Tanzania Bara vitafikiwa na nishati ya
umeme.Na
Veronica Simba – Mwanza
No comments:
Post a Comment