Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo (katikati), akizungumza na Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REB), ofisini kwake, Oktoba 9, 2019 |
Mkuu wa Mkoa wa
Arusha, Mrisho Gambo ameiasa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini
(REB), kuitendea haki nafasi waliyopewa na Mheshimiwa Rais John Magufuli; kwa
kuwatumikia wananchi kwa uaminifu na weledi, hususan katika sekta ya nishati
ambayo wanaisimamia.
Gambo ametoa wito huo
leo, Oktoba 9, 2019 wakati Kamati ya Ufundi ya Bodi hiyo, ilipomtembelea
ofisini kwake, ikiwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi
ya umeme vijijini, mkoani humo.
“Itumieni nafasi
mliyopewa na Rais kuhakikisha wananchi, hususan walioko vijijini, wanapata
nishati ya umeme ili waweze kuboresha maisha yao.”
Aidha, Mkuu huyo wa
Mkoa, ameishauri Bodi hiyo kushughulikia maagizo yaliyotolewa na Rais Magufuli,
kupeleka umeme katika migodi mbalimbali ya madini ili kuwawezesha wachimbaji
kuendesha kazi zao kwa tija.
“Hapa tuna Soko la
Madini Karatu, nitafurahi nikisikia mmewapelekea umeme.”
Katika hatua
nyingine, Gambo ameipongeza REA kwa kuwapelekea umeme wananchi wa Wilaya ya
Longido ambao awali hawakuwa kwenye Mpango, lakini kwa maelekezo ya Wizara,
walijumuishwa na tayari walikwishaanza kuunganishiwa umeme.
Akizungumza kwa niaba
ya Ujumbe huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Bodi ya REA, Mhandisi Styden
Rwebangila amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kwamba watafanyia kazi maelekezo yake.
Amesema, Bodi imempa
Mkandarasi NIPO Group, anayetekeleza mradi wa umeme vijijini mkoani Arusha siku
21 kuhakikisha anasimika nguzo zote zaidi ya 1,000 zilizo chini, kuvuta nyaya
pamoja na kuwanganishia umeme wananchi wote waliolipia, na kwamba asipotekeleza
hayo, hatua za kimkataba zitachukuliwa dhidi yake.
Akitoa takwimu za
utekelezaji wa mradi wa umeme vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza,
mkoani humo, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa REA, Mhandisi Jones Olotu
amesema, mkandarasi amefikia asilimia 52 kati ya 62.5 alizopaswa kuwa amefikia
hadi sasa.
Aidha, alibainisha
kuwa, amewasha umeme katika vijiji 39 kati ya 126 anavyotakiwa kuwasha na
ameunga jumla ya wateja 1,880 kati ya 5,428 anaotakiwa kuwaunga kwa Mkoa mzima
wa Arusha.
Bodi inatarajiwa
kufanya maamuzi dhidi ya Mkandarasi baada ya siku 21 ilizompa kuisha. Na
Veronica Simba – ARUSHA
No comments:
Post a Comment