Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akifungua barabara ya Kanazi-Kizi-Kibaoni km 76.6 iliyokamilika kujengwa
kwa kiwango cha lami pamoja na Daraja la Kavuu M 85.3 katika sherehe
zilizofanyika katika eneo la Kibaoni mkoani Katavi.
Rais Dkt. John Magufuli
leo tarehe 09 Oktoba, 2019 ameendelea na ziara yake katika Mkoa wa Katavi ambapo
amefungua barabara ya lami ya Kanazi – Kizi – Kibaoni yenye urefu wa kilometa
76.6 na daraja la Kavuu (lenye
urefu wa meta 85.3 na
upana wa meta 4.6) lililopo katika barabara ya
Majimoto – Inyonga.
Ujenzi wa barabara
ya Kanazi – Kizi – Kibaoni ambao ni sehemu ya barabara kuu ya Sumbawanga –
Namanyere – Mpanda yenye urefu wa kilometa 245 umegharimu shilingi Bilioni
102.364, fedha zote zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akiwasalimia wananchi wa Kibaoni mkoani Katavi mara baada ya kuwasili
wakati akitokea wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa.
Ujenzi wa daraja la
Kavuu ambalo linaunganisha Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe na
Wilaya ya Mlele Mkoani Rukwa, umegharimu shilingi Bilioni 3.6, fedha zote
zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Akizungumza na
wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kibaoni Wilayani Mlele, Mhe.
Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Mkoa wa Katavi kwa juhudi kubwa katika
uzalishaji wa mazao ya chakula na amewaahidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha
miundombinu ya barabara na madaraja na kuimarisha zaidi huduma za kijamii
ikiwemo kusambaza zaidi umeme na maji.
Sehemu
ya barabara ya Kanazi-Kizi-Kibaoni km 76.6 iliyokamila kujengwa kwa
lami na kufunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kama inavyoonekana pichani.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akiwahutubia wananchi wa Kibaoni mkoani Katavi mara baada ya kufungua
barabara ya Kanazi-Kizi-Kibaoni km 76.6 iliyokamila kujengwa kwa lami
pamoja na Daraja la Kavuu M 85.3
Rais Magufuli ameiagiza
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuanza maandalizi ya ujenzi wa
barabara ya Kibaoni – Sitalike yenye urefu wa kilometa 71 ambayo ni kipande
kilichobaki kuunganisha Mkoa wa Rukwa na Katavi kupitia Hifadhi ya Taifa ya
Katavi.
Amefafanua kuwa Serikali
imedhamiria kuhakikisha barabara kuu kwa kiwango cha lami kutoka Mpanda –
Uvinza – Nyakanazi unakamilika ili ukanda wa nyanda za juu kusini
unaoiunganisha Tanzania na nchi za Zambia, Malawi hadi Afrika Kusini
uunganishwe na ukanda wa magharibi unaounganisha Tanzania na nchi za Burundi,
Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Uganda.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akizungumza na wananchi wa Kizi mkoani Rukwa wakati akielekea Kibaoni
mkoani Katavi.
Kuhusu migogoro ya
ardhi, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali imeamua vijiji 920 kati ya 975 hapa
nchini vilivyopo katika maeneo ya hifadhi kutoondolewa katika maeneo hayo,
kufuta mapori ya akiba 12 (yenye
jumla ya ekari 707,659.95) na Misitu 7 (yenye jumla ya ekari 46,715)
na kumega maeneo katika hifadhi 14 ili kuwawezesha wananchi kupata maeneo ya
kuishi, kilimo na ufugaji na kwamba katika uamuzi huo vijiji 60 vilivyonufaika
ni vya Mkoa wa Katavi.
Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi amefafanua kuwa pamoja na
hatua hiyo, wataalamu wa ardhi watapita katika vijiji hivyo ili kutoa elimu ya
matumizi bora ya ardhi ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza baina ya
wananchi.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akizungumza na wananchi wa Mulele wakati akielekea kufungua barabara ya
Kanazi-Kizi-Kibaoni km 76.6
Hata hivyo, Mhe.
Rais Magufuli ameonya kuwa baada ya Serikali kuchukua uamuzi huo, haitarajii
kuona wananchi wanaendelea kuvamia maeneo ya hifadhi na amewataka wananchi wa
Katavi kutumia maeneo hayo kuzalisha zaidi mazao mbalimbali ili kujiongezea
kipato.
Akiwa njiani kutoka
Namanyere katika Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa kuelekea Mpanda Mkoani Katavi,
Mhe. Rais Magufuli amesalimiana na wananchi wa Kizi (Nkasi) na Mirumba
(Mlele)
na baadaye amesalimiana na wananchi wa Sitalike Wilayani Mpanda ambapo
amewahakikishia kuwa vitongoji vya Igalukilo, Kabenga, Kaloleni na Situbwike
havitaondolewa katika maeneo ya hifadhi kufuatia uamuzi wa Serikali wa
kuvirasimisha vitongoji hivyo.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akiangalia wanyama aina ya viboko katika hifadhi ya Taifa ya Katavi
mara baada ya kusimama wakati akielekea Mpanda.
Wakati huo huo,
Mhe. Rais Magufuli ametembelea Hifadhi ya Taifa ya Katavi na kisha kuzungumza
na Maafisa na Askari Wanyamapori wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) ambapo
amewapongeza kwa kazi nzuri ya kuhifadhi wanyamapori ikiwemo kukabiliana na
ujangili hali iliyowezesha kuongezeka kwa idadi ya wanyama wakiwemo wale
waliokuwa hatarini kutoweka.
Mhe. Rais Magufuli
amemtaka Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA Dkt. Allan Kijazi kuchimba mabwawa ya
kuvuna maji mengi zaidi ya mvua yatakayowasaidia wanyama hasa viboko wakati wa
kiangazi kikali pamoja na kujipanga kuzuia wanyama wakali wanaoweza kuvamia
makazi ya watu na kuhatarisha maisha ya wananchi.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akizungumza na Wananchi wa Nsimbo mkoani Katavi mara baada ya kuwasili
akitokea Kibaoni.
Kesho tarehe
10 Oktoba, 2019 Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth
Magufuli ataendelea na ziara yake hapa Mkoani Katavi ambapo atazindua Kituo cha
Mabasi cha Mkoa wa Katavi, ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya
Mpanda – Tabora, atafungua barabara ya Mpanda – Sitalike na kuhutubia mkutano
wa hadhara katika uwanja wa Azimio Mjini Mpanda.
PICHA NA IKULU
No comments:
Post a Comment