Matokeo chanyA+ online




Thursday, October 3, 2019

TANZANIA YAPIGA HATUA USAMBAZAJI WA MAJI VIJIJINI

Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa kazi mbalimbali za Serikali, Mkutano huo ulifanyika leo Oktoba 3, 2019 Jijini Dar es Salaam.

Na: Mwandishi Wetu – Maelezo, Dodoma

Tanzania yapiga hatua katika usambaji wa huduma za upatikanaji wa maji safi na salama mijini toka asilimia 45 mwaka 2015 hadi 95 mwaka huu na asilimia 46 mwaka 2015 hadi asilimia 65 mwaka huu kwa vijijini.
Hayo yamebainishwa na Mkrugenzi wa Idara ya Habari –MAELEZO na MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi wakati akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam kati mkutano wake wa kawaida wa kila mwezi kuelezea utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, akisisitiza jambo kwa Waandishi wa Habari (hawapo pichani), kuhusu utekelezaji wa kazi mbalimbali za Serikali, katika mkutano wake na Waandishi wa Habari ulifanyika leo Oktoba 3, 2019 Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mkutano huo, Dk. Abbasi amesema kuwa mwaka 2015, Serikali ya Awamu ya Tano iliweka lengo la kufikisha maji vijijini kwa asilimia 85 na mijini asilimia 95 ifikapo mwaka 2020.
Dkt Abbasi amesema kuwa katika kufikia lengo hilo kazi kubwa imefanyika ambapo zaidi ya miradi 289 na vituo zaidi ya 89,780 vimekamilika ambapo Serikali imetumia zaidi ya TZS bilioni 336.15.
“Kazi kubwa inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali vijijini ikiwemo kukamilisha vituo 44,590 vya maji.” Alisema Dkt. Abbasi
Hadi Septemba mwaka huu zaidi ya miradi mikubwa 17 ya maji imekamilishwa ambapo zimetumika zaidi ya TZS bilioni 823.61. Wakati miradi mingine mikubwa zaidi ya 35 ya maji ikiendelea kukamilishwa nchini, wastani wa upatikanaji wa maji safi mijini umefikia asilimia 80.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, akikaribisha swali kutoka kwa Mwandishi wa Habari (hayupo pichani), wakati wa Mkutano wake na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa kazi mbalimbali za Serikali, ulifanyika leo Oktoba 3, 2019 Jijini Dar es Salaam.

Kwa uwekezaji huu, wastani wa jumla wa upatikanaji wa maji vijijini umepanda kutoka chini ya asilimia 46 mwaka 2015 hadi asilimia 65 mwaka huu huku kwa upande wa mijini, mwaka 2015 Serikali iliweka lengo la kufikisha maji kwa asilimia 95 kwa wakazi wa mijini kutoka wastani wa asilimia 67;
Katika hatua nyingine Dkt. Abbasi alitumia mkutano huo kuwaondoa hofu wakulima wa zao la Korosho akisema kuwa kumeanza kuibuka wasiwasi katika jamii na baadhi ya watu kuanza kuwatisha wakulima kuwa msimu mpya wa korosho unakuja, watakosa maghala ya kuhifadhi korosho zao.
“Niwahakikishie wakulima kuwa hadi kufikia Septemba 30, 2019, Serikali imeshauza korosho zote kwa jumla ya wanunuzi 21 wa ndani na nje ya nchi. Kuna tani zaidi ya 4,595.90 zitabanguliwa nchini na zaidi ya tani 211, 587 ambapo tani 107,187 zitapitia Bandari ya Dar na tani 104,400 kupitia Bandari ya Mtwara zitasafirishwa kwenda nje ya Tanzania,” alisisitiza Dkt. Abbasi.
Alifafanua kuwa hadi sasa zaidi ya tani 98,860 zimekwishachukuliwa na kusafirishwa nje ya nchi kupitia Bandari za Mtwara na Dar sawa na asilimia 41 ya korosho zote na zoezi la kuondoa korosho iliyobaki kupelekwa kwa wanunuzi linatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 21 mwaka huu.
“Naomba kusisitiza tena, faida kubwa ya mchakato huu ni kwa wakulima kupata bei ya haki katika zao la korosho lakini funzo la korosho si tu limeweka mazingira mazuri zaidi katika misimu ijayo ambapo korosho itanunuliwa kwa mfumo madhubuti lakini pia mazao mengine yamepata nguvu ya kuwekewa mifumo na hivyo wakulima kupata bei inayowanufaisha kwa kuwapa faida.”Alisema Dkt. Abbasi.
Msemaji Mkuu wa Serikali amekuwa na utamaduni wa kuzungumza na wananchi kila mwanzoni mwa mwezi kupitia vyomba vya habari kwa lengo la kuhabarisha umma juu ya hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ili wananchi taarifa sahihi za namna Serikali yao inavyowajali katika kuwaletea maendeleo.

No comments:

Post a Comment