Mkurugenzi
wa Huduma za Kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Dkt.Leonard Subi akiandika anayoyasikia kwenye Mkutano wa Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe.Ummy Mwalimu(kushoto) wakati
wa mkutano wake na Waandishi wa Habari uliofanyika katika Kituo cha Mikutano
cha Kimataifa Julias Nyerere Jijini Dar es Salaam leo Oktoba 3, 2019 (Picha na Idara ya Habari-MAELEZO)
Magonjwa
yanayofuatiliwa kwa karibu na kutolewa taarifa mara moja pindi
yakitokea ni, kumi na nne (14) ambayo ni pamoja na Kipindupindu, Polio,
Kimeta, Kuhara Damu, Homa ya Uti wa Mgongo, Mafua makali ya ndege,
Surua, Pepopunda ya watoto wachanga, Kichaa cha Mbwa, Ndui, Magonjwa
yanayosababishwa na Virusi na Homa yanayosababisha damu kuvuja (Ebola,
Marburg, RVF, Homa ya Dengue, Chikungunya), Macho mekundu, Tauni, na
Homa ya Virusi ya Manjano.
Utoaji
wa taarifa za magonjwa haya zimerahisishwa, ambapo vituo vyote vya
kutoa huduma za Afya nchini kuanzia ngazi ya chini hutoa taarifa hizi
kwa kupitia mfumo maalum kwa njia ya simu (Integrated Disease
Surveillance and Response - IDSR). Hii hupelekea taarifa zote muhimu
kuhusu magonjwa kupatikana kwa haraka na hatua kuchukulia mapema na
wizara ili kudhibiti magonjwa haya.
Kwa
kipindi cha mwezi Septemba 2019, Wizara imeendelea kufuatilia magonjwa
haya na matukio hatarishi kwa afya, kutoka kwenye mikoa yote nchini.
Katika mwezi Septemba, ugonjwa wa Dengue na Surua tu ndio magonjwa ya
milipuko yaliyotokea hapa nchini.
Mwenendo wa Homa ya Dengue nchini.
Kwa
Kipindi cha mwezi Septemba 2019, jumla ya wagonjwa 10 walithibishwa
kuwa na Homa ya Dengue na hakukuwa na kifo. Wagonjwa hawa walitolewa
taarifa kutoka mikoa 2 ambayo ni Dar es salaam – wagonjwa 4 (Hospitali
ya Taifa Muhimbili - 4) na Tanga – wagonjwa 6 (Tanga jiji - 6).
Ugonjwa
huu umeendelea kudhibitiwa kwa kiasi kikubwa nchini na umeendelea
kupungua mwezi hadi mwezi. Takwimu za miezi mitatu (Julai, Agosti na
Septemba, 2019) zimeonyesha kupungua kwa ugonjwa huu kwa kiasi kikubwa
ambapo mwezi Julai 2019 kulikuwa na wagonjwa waliothibishwa 732, mwezi
Agosti wagonjwa 92 na mwezi Septemba wagonjwa - 10.
Aidha
tangu mlipuko huu uanze mwezi Januari 2019 hadi kufikia tarehe 30
Septemba, 2019 kumekuwa na jumla ya wagonjwa waliohisiwa kuwa na Dengue
14,369 na kati yao waliothibishwa ni 6,785 na vifo 13 (Dar-6259,
Tanga-365, Pwani-115, Morogoro-22, Lindi-8, Arusha-5, Singida-3,
Dodoma-3, Ruvuma-2, Kagera-2 na Kilimanjaro-1).
Ili
kukabiliana na magonjwa yaenezwayo na wadudu dhurifu wakiwemo mbu,
Wizara ilizindua mpango mkakati wa kukabiliana na wadudu dhurifu na mbu
(National Vector control strategy 2019 - 2023) tarehe 27 Julai 2019, Dar
es Salaam. Uzinduzi huu uliambatana na uzinduzi wa kitaifa wa zoezi la
upuliziaji wa dawa kupambana na mbu wapevu na unyunyiziaji wa dawa za
kuua viluwiluwi wa mbu waenezao magonjwa kama vile Malaria, Dengue na
nk,. Dawa za kuangamiza wadudu zilinunuliwa pamoja na mashine kubwa (4)
za kupulizia dawa (Fogging Machine) ambazo zilisambazwa katika mikoa
iliyoathirika na ugonjwa wa Dengue yaani Dar es Salaam, Tanga pamoja na
Dodoma. Wizara imeshaagiza mashine nyingine 4 ili kuweka mkakati
endelevu wa zoezi hili.
Mikoa
hii pia (Dar es salaam, Dodoma, Tanga) ilishafanya uzinduzi wa Mkakati
wa Kudhibiti Mbu na Wadudu wadhurifu pamoja na kuendesha zoezi la
kuangamiza mbu. Hatua hii imesaidia kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa
Dengue nchini kama inavyoonyeshwa katika takwimu.
Aidha,
zoezi hili la uzinduzi linaendelea kufanyika katika Mikoa yote ili
kutokomeza magonjwa yaenezwayo na wadudu hao. Elimu endelevu pia
inaendelea kutolewa kwa wananchi juu ya namna kujikinga na kudhibiti
ugonjwa huu
Mwenendo wa Ugonjwa wa Kipindupindu nchini.
Ugonjwa
wa Kipindupindu umedhibitiwa, na kwa sasa HATUNA KABISA mgonjwa wa
Kipindupindu nchini. Mara ya mwisho kupata mgonjwa wa Kipindupindu
nchini ilikuwa tarehe 14 mwezi Julai 2019.
Kwa
kipindi cha kuanzia tarehe 1 Januari hadi Julai 2019, kulikuwa na jumla
ya wagonjwa 424 na vifo 8 vya ugonjwa wa Kipindupindu. Wizara
inaendelea kuchukua hatua za kudhibiti ugonjwa huu, ikiwa ni pamoja
kufuatilia hatua zinazochukuliwa za kuzuia ugonjwa huu na timu ya Mkoa
na Halmashauri ambazo ni pamoja na; Kutoa elimu ya afya kwa wananchi
ya namna kujikinga kupata ugonjwa huu, Ufuatiliaji wa usafi wa
mazingira.
Wizara
inakamilisha Mpango Mkakati wa Kipindupindu wa mwaka 2019 hadi 2023
ambao utekelezaji wake utajikita katika maeneo yanayotoa wagonjwa mara
kwa mara (Hotspot areas) ambayo ni Dar es Salaam (Halmashauri zote),
Ngorongoro (Arusha), Simanjiro (Manyara), Handeni na Mkinga (Tanga),
Kilwa (Lindi), Ulanga (Morogoro), Mbarali na Chunya (Mbeya), Songwe,
Sumbawanga DC (Rukwa), Mpanda (Katavi), Nyasa (Ruvuma) na Iringa DC
(Iringa).
Mpango
huu, unalenga kutokomeza Kipindupindu kabisa. Katika mpango huu maeneo
yalijikita ni pamoja na: Uratibu na ushirikishwaji wa wadau katika ngazi
zote katika kudhibiti ugonjwa, kuimarisha ufuatiliaji na upimaji wa
wagonjwa, Kuimarisha utoaji wa matibabu sahihi na mapema kwa wagonjwa,
ushirikishwaji wa jamii katika kudhibiti na ugonjwa, kuweka mazingira ya
kuwepo kwa maji safi na salama na masuala ya matumizi ya vyoo na
vilevile kuimarisha utoaji wa chanjo kwa maeneo sugu na vigezo
vitakavyotumika.
Wizara
imeendelea pia na utekelezaji wa Kampeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira
yenye kaulimbiu isemayo “USICHUKULIE POA NYUMBA NI CHOO”, ikiwa ni moja
ya mikakati ya kutokomeza Kipindupindu na magonjwa ya kuhara. Kampeni
hii ambayo ipo katika awamu ya pili, ilizinduliwa rasmi Disemba, 2017 na
Mhe. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Uanzishwaji
wa Kampeni hii ni sehemu ya jitihada za serikali kujielekeza katika
kutekeleza lengo namba 6.2 la Malengo ya Maendeleo Endelevu (Sustainable
Development Goals) pamoja na lengo namba 3 linahusu kuboresha Afya.
Katika kipindi cha miaka mitatu ya utekelezaji (2016-2019), jumla ya
kaya 2,464,225 zimejenga au kuboresha vyoo kufikia kiwango cha ubora
kati ya lengo la kaya 3,360,000. Hii ni sawa na asilimia 73.3. Kwa
upande wa taasisi, shule 1,670 kati ya lengo la shule 2,520 zimejenga
vyoo bora kwa kuzingatia uwiano.
Kwa
ujumla kaya zenye vyoo bora katika ngazi ya kaya zimeongezeka kutoka
asilimia 46 Julai, 2016 hadi asilimia 57.2 Juni, 2019, na kaya
zisizokuwa na vyoo zimepungua kutoka asilimia 7.5 hadi asilimia 2.5
katika kipindi hicho.
Mwenendo wa Ugonjwa wa Surua nchni.
Katika
kipindi cha mwezi Septemba 2019, mlipuko wa ugonjwa Surua ulitokea
katika kitongoji cha Kashasha, Kakoma na kijiji cha Kibare wilayani
Kyerwa mkoa wa Kagera. Jumla ya wagonjwa 17 walipatikana na ugonjwa wa
surua ambapo kati yao; wagonjwa saba walithibitishwa kwa kipimo cha
maabara. Mgonjwa wa mwisho kupatwa na dalili za surua katika eneo la
Kibare ilikuwa tarehe 14/09/2019.
Kwa
takribani wiki mbili sasa hakuna mgonjwa mwingine aliyepatikana.
Wagonjwa wote wamepona na elimu ya jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa
surua imetolewa na pia kuhamasisha kuwaleta watoto katika kampeni ya
kitaifa shirikishi ya chanjo ya surua na rubella, watoto wote chini ya
miaka mitano.
Katika
ufuatiliaji wa ugonjwa surua nchini wagonjwa wenye dalili za homa na
vipele hufuatiliwa na kuchukuliwa sampuli kupima kubaini kama wana
ugonjwa wa surua. Kwa kipindi cha mwezi Septemba 2019, jumla ya sampuli
222 za wagonjwa waliokuwa na dalili ya homa na vipele zilipokelewa na
kufangashwa na kuwasishwa maabara ya Taifa kutoka kwenye mikoa 23 ya
Tanzania bara.
Mwenendo wa Ugonjwa wa Polio nchini.
Hadi
sasa hakuna mgonjwa wa Polio aliyethibika hapa nchini tangu mwaka 1996.
Hii inatokana na jitihada kubwa za Serikali katika kutoa chanjo na
kufuatilia dalili za wagonjwa wenye ugonjwa huu na pia kwa kununua
chanjo za Polio ambazo zimeweza kuwafikia watoto wote chini ya miaka
mitano (5) kwa zaidi ya asilimia 90%.
Katika
ufuatiliaji wa ugonjwa huu, wagonjwa wote wa dalili za kupooza ghafla
(Acute Flaccid Paralysis - AFP) hufuatiliwa na sampuli kuchukuliwa na
kupimwa kujua kama wana ugonjwa wa Polio. Kwa mwezi Septemba 2019, jumla
ya sampuli 63 za AFP 63 zilifungashwa na kupelekwa maabara kwa ajili ya
vipimo. Aidha katika ufuatiliaji wa virusi vya polio katika
mazingira, ambapo kirusi hiki pia hukaa kwa muda nao unaendelea na hadi
sasa kirusi hiki kimeonekana kuwa hakipo katika mazingira yetu.
Ufuatiliaji wa mara kwa mara unaendelea. .
Katika
mpango wa kutokomeza vifo na ulemavu kutokana na magonjwa yanayozuilika
kwa chanjo. Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo na kwa
kushirikiana na Ofisi ya Rais - TAMISEMI, itaendesha kampeni ya chanjo
dhidi ya Magonjwa ya Surua, Rubella na Polio mnamo tarehe 17 hadi 21
mwezi Octoba 2019. Kampeni hii itafanyika nchi nzima kwa watoto wote
lengwa walio na umri wa chini ya miaka mitano. Nawasihi wananchi wote
washiriki ili Serikali ifikie lengo la kampeni hii.
Mwenendo wa Ugonjwa wa Ebola unaoendelea kuripotiwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)
Wizara
imekuwa ikifuatilia kwa karibu mwenendo wa ugonjwa wa Ebola unaoendelea
kuripotiwa nchini DRC na kuchukua hatua za tahadhari za kuzuia na
kukabiliana na ugonjwa huu hususani kwa kuwa kwa sasa ugonjwa huu
unaendelea kusambaa na kuingia kusini mwa DRC. Takwimu zinaonyesha kuwa
hadi kufikia tarehe 30 Septemba 2019, jumla ya wagonjwa 3,194
walithibitishwa kuwa na ugonjwa huu, na vifo 2133 (CFR 66.8%). Kutokana
na ukaribu wa nchi hii na Tanzania, Wizara imeendelea kuchukua hatua za
utayari kuzuia na kujiandaa kukabiliana na ugonjwa huu
Hatua
za utayari na kujiandaa kukabiliana na ugonjwa huu nchini ni pamoja na
kuimarisha uchunguzi wa Wasafiri kwenye mipaka yetu yote. Kuimarisha
utambuzi katika ngazi ya vituo vya kutolea huduma za Afya; Kuhakikisha
uwepo vya Vifaa Kinga hususani kwa watumishi wa Afya; Kuimarisha
utambuzi wa Ugonjwa na kuendelea kutoa Elimu kwa wananchi kuhusu namna
ya kujikinga ugonjwa huu.
Wizara
inayo namba ambayo hutumika bila malipo na wananchi kutoa taarifa za
kuwepo kwa tetesi za ugonjwa huu ambazo ni 0800110124 au 0800110125.
Kuanzia 2018 hadi sasa, tetesi 28 za wagonjwa wanaohisiwa kuwa na Ebola
(washukiwa 2 kwa mwezi Septemba), zimekwisha kutolewa taarifa na
uchunguzi kufanyika kwa ukamilifu na kuthibitisha wagonjwa hawa hawakuwa
na Ebola, na taarifa zake kupelekwa pia katika Shirika la Afya Duniani.
Aidha Wizara imeendelea kufanya pia mazoezi ya kujinoa na kijipima
utayari wa kukabiliana na ugonjwa huu (Simulation Exercises) katika
mikoa ya Dar es Salaam, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro na Arusha.
NAPENDA
KUSISITIZA KUWA HADI SASA HAKUNA MGONJWA ALIYETHIBITISHWA KUWA NA
UGONJWA WA EBOLA HAPA NCHINI. WIZARA INAWASIHI WANANCHI KUTOKUWA NA HOFU
NA KUPUUZA TAARIFA ZINAZOTOLEWA KILA KUKICHA NA BAADHI YA VYOMBO VYA
HABARI NA MITANDAO YA KIJAMII.
Katika
kudhibiti ugonjwa wa Ebola na magonjwa mengine ya milipuko yenye
madhara makubwa duniani, nchi yetu kila wakati imekuwa mstari wa mbele
ikiwa ni pamoja na kusimamia kwa ukamilifu na kutekeleza Kanuni za
Kimataifa za Afya (International Health Regulation - IHR 2005). Mnamo
mwaka 2016, Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza duniani kuweza kukubali bila
kipingamizi kuleta wataalam duniani kuja kupima utayari wa nchi yetu
katika kukabiliana na magonjwa haya hatarishi (Joint external
evaluation). Hatua hii kubwa na ya uwazi ilifanywa kwa mara ya kwanza
Duniani, kama moja ya njia ya kuhakikisha nchi wanachama wa Shirika la
Afya Duniani, wanatekeleza Kanuni hizi za Kimataifa (IHR 2005). Aidha
nchi nyingine zenye uwezo mkubwa duniani zilisita kufanyiwa tathmini
hadi miaka miwili baadae, na nyingine hadi sasa hazijafanya zoezi hili.
Hivyo basi, taarifa zinazoenea kuelezea kuhusu Tanzania kutokuweka wazi
taarifa za magonjwa hususan uwepo wa ugonjwa wa Ebola nchini, si za
kweli na hivyo ziendelee kupuuzwa. Taratibu za utoaji wa taarifa za
magonjwa ya milipuko zinajulikana na ninatoa rai kwa sote tuzingatie
sheria na taratibu za nchi husika na za kimataifa.
Ikumbukwe
kuwa, ugonjwa wa Ebola ambao unaweza kusambaa kwa haraka, na ambao
madhara yake ni makubwa na yanajulikana duniani kote, kamwe hauwezi
kufichwa na nchi yetu. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
inatambua madhara makubwa ya kuficha ugonjwa kama huu kwa wananchi.
Narudia tena na kuwataka wananchi kutulia na kupuuza taarifa zisizo
rasmi kutoka kwenye baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii,
maana HAKUNA UGONJWA WA EBOLA NCHINI TANZANIA. Inaonekana kuna njama ovu
za kueneza taarifa hasi dhidi ya nchi yetu. Ninaendelea kuwasihi
Wananchi kuwa watulivu na kushikamana kwa pamoja katika kuzuia ugonjwa
huu usiiingie nchini.
Aidha,
Serikali inapenda kuwahakikishia Mataifa yote kuwa nchi yetu ni SALAMA
na HATUNA UGONJWA WA EBOLA. Nirudie tena kusisitiza kuwa Serikali
itaendelea kushirikiana na nchi na mashirika mbalimbali ya kimataifa
ikiwemo Shirika la Afya Duniani katika kujenga utayari wa kukabiliana na
tishio la ugonjwa wa Ebola. Na endapo kutatokea mtu atakaethibishwa
kuwa na ugonjwa wa Ebola nchini tutaendelea kuzingatia miongozo na
taratibu za kimataifa ikiwemo kutoa Taarifa WHO kwa mujibu wa Kanuni za
Kimataifa za udhibiti wa magonjwa hatari ya kuambukiza (IHR 2005).
Kipaumbele
cha Wizara kwa sasa ni kuendelea kuimarisha utayari wa kukabiliana na
ugonjwa huu usiingie nchini na endapo kutatokea kisa cha ugonjwa huu
nchini tuweze kukabiliana nao na kuudhibiti mara moja.
|
No comments:
Post a Comment