Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema vyombo vya Dola kwa mujibu wa
Sheria na Kanuni zilizopo wakati wote hubeba dhima ya kufanya uchunguzi dhidi
ya hujuma zinazoibuka na hatimae kuleta hatari ya uvunjifu wa Amani ndani ya
Jamii.
Alisema uchunguzi
wa hujuma zozote zile pale unapokamilika na kupatikana ushahidi kamili vyombo
hivyo havitasita kuchukuwa hatua za kisheria katika kutoa haki kwa
muhusika.
Balozi Seif Ali
Iddi alitoa kauli hiyo wakati alipofanya ziara fupi ya kuipa pole Familia ya
Mwenyekiti Mstaafu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mjini Mzee Borafia Silima
Juma kufuatia Nyumba yake kuwaka moto na kuteketeza vitu vyote vilivyomo ndani
hapo Mtaa wa Muembe Rikunda nyuma ya Jumba Nambari Mbili Michenzani.
Balozi Seif alisema
Wananchi wanapaswa kuendelea kufuata Sheria na taratibu zilizopo Nchini kwa
kuviamini vyombo vya Dola vilivyopewa jukumu kubwa na Serikali la kulinda
Mali na Maisha yao.
Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar aliitaka Familia ya Mzee Borafya kuwa na subra katika kipindi
hichi cha mpito kufuatia mtihani uliowapata na kuithibitishia kwamba Serikali
itaangalia utaratibu wa kuihami Familia hiyo kutokana na mazingira halisi ya
Nyumba hiyo ilivyo hivi sasa.
Naye Waziri wa Nchi
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed alisema
utafiti wa awali uliofanywa na Wataalamu wa Kamisheni ya kukabiliana na Maafa
Zanzibar muda mfupi baada ya tukio hilo umebaini kwamba huo ulikuwa ni moto wa
kutiwa kwa makusudi.
Waziri Aboud
alisema Wataalamu hao hivi sasa wanaendelea na uchambuzi wa kina wa utafiti wa
tukio hilo na baadae kuona jinsi gani Kamisheni hiyo inaweza kuisaidia Familia
hiyo kwa njia za Kitaalamu.
Mapema Mmoja wa
Wanafamilia wa Nyumba hiyo Bwana Salum Borafia Silima alimueleza Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar kwamba Wanafamilia hao wanaamini kwamba tukio hilo ni
hujuma ya makusudi kwa mara ya pili ndani ya kipindi cha saa Ishirini na Nne.
Bwana Salum alisema
hujuma ya kwanza ilitokea Jumamosi majira ya saa moja ya Usiku pale Mmoja
miongoni mwa Wanafamilia hao ambae ni mgonjwa alipobaini harufu ya moshi
dirishani na kupiga kelele zilizosaidia kubaini moto huo ambao uliunguza waya
na pazia la Dirisha hilo.
Alisema tukio hilo
likatokea tena Siku ya Pili ya Jumapili muda unaolingana ambalo ni kubwa zaidi
lililopelekea moto mkubwa kuripuka na kusababisha kuunguza kila kilichomo ndani
ya Nyumba hiyo ambapo baadae akalazimika kutoa Ripoti kituo cha Polisi kwa
hatua zinazofaa.
No comments:
Post a Comment