Tanzania
inaungana na ulimwengu mzima kuadhimisha Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili
wa Kijinsia nchini. Chimbuko la maadhimisho haya limetokana na Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa wa Awamu ya 7, Mhe. Koffi Annan alipotoa Tamko mwaka 2006, la
kutaka Dunia itambue kuwa lipo tatizo kubwa la ukatili wa kijinsia dhidi ya
wanawake na watoto wa kike, hivyo ikapendekezwa kuna haja ya kuwa na kipindi
maalum cha Kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia, na kukubaliwa iwe inafanyika
kuanzia tarehe 25 Novemba hadi tarehe 10 Desemba kila mwaka.
Kwa mwaka huu maadhimisho ya Kampeni hii yatafanyika
kitaifa Jijini Dodoma katika Uwanja wa Jamhuri kuanzia tarehe 25 Novemba, 2019
na kilele chake kuwa tarehe 10 Disemba, 2019. Maadhimisho haya yamelenga kuongeza ushawishi, kubadilishana
taarifa na uzoefu, kujenga uwezo wa pamoja, matumizi mazuri ya rasilimali
zinazopatikana na kuunganisha nguvu za pamoja katika kuhamasisha, kuelimisha,
kukemea na kuchukua hatua kwa pamoja ili kupinga ukatili wa kijinsia katika
jamii, kwa kuzingatia mazingira na matukio yanayoenda sambamba na kauli mbiu
husika.
Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya mwaka huu
ni “Kizazi Chenye Usawa: Simama Dhidi ya
Ubakaji”. Kauli mbiu hii inatupa jukumu sisi sote kutafakari wajibu wetu
kama kizazi kinachoamini na kuthamini usawa wa kijinsia. Kauli mbiu hii inatupa
msukumo wa kuhakikisha kuwa kila mtu katika nafasi yake anapaza sauti na
kuchukua hatua ya kuzuia na kutokomeza vitendo vya ukatli wa kingono hasa
ubakaji na matendo yote ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika maeneo
mbalimbali ikiwemo katika nyumba tunazoishi, mahali pa kazi, shuleni na mahali
pengine katika jamii zetu.
Katika kupambana na tatizo la ukatili wa
kijinsia,Wizara inawaomba watanzania na wadau kuunganisha nguvu na
kubuni mikakati ya kijamii ambayo italeta suluhisho la kudumu. Katika baadhi
ya maeneo ya nchi yetu matokeo mazuri yameanza kupatikana kwa kuwashirikisha
wananchi wenyewe na hasa kuwahusisha
viongozi wa kijamii kama vile viongozi wa dini, viongozi wa kimila, wazee
maarufu na watu wengine ambao wana sauti katika jamii husika.
Tunatoa wito kwa wadau wote na wanachi kushiriki na kutumia kampeni
hii kupata elimu na uelewa kuhusu namna
ya kuzuia na kutokomeza ukatili wa kijinsia na kuwa na sauti ya pamoja katika
kukabiliana na vitendo hivyo.
No comments:
Post a Comment