Matokeo chanyA+ online




Tuesday, November 26, 2019

WABUNGE KUTOKA KOREA WATEMBELEA HOSPITALI YA MLOGANZILA

Dkt Magandi katika picha ya pamoja na wabunge walioongozana na mwenyekiti wa Kamati ya Afya ya Bunge la Korea ya Kusini waliokuja kutembelea hospitalini hapa. 
 
Wabunge kutoka Korea wametembelea Mloganzila Wabunge wa Serikali ya Korea ya Kusini wakiongozwa na mwenyekiti wa kamati ya afya ya Bunge hilo, leo wametembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila ili kufahamu huduma zinazotolewa hospitalini hapa.
Akizungumza wakati wa kuwakaribisha wageni hao, Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi amewaeleza kuwa hospitali ya Mloganzila ina vifaa tiba vya kisasa na inatoa huduma mbalimbali za afya ambapo kwa siku inahudumia wagonjwa wa nje 400 hadi 450.
 


 Mtaalam wa Maabara katika Hospitali ya Mloganzila, Bw. Mbaruku Kisutu akiwaelezea wageni hao namna wataalam wa maabara wanavyofanya kazi.
 Dkt. Frida Shao kutoka Kitengo cha Magonjwa ya Dharura katika hospitali ya Mloganzila (EMD) akiwaelezea wageni hao kazi zinazofanywa na kitengo hicho.
 
“Hospitali yetu ina vifaa vya kisasa kama vile CT-Scan na MRI pamoja na kutoa huduma kwa wagonjwa ambapo kwa siku tunawahudumia wagonjwa 400 hadi 450,” Amesema Dkt. Magandi.
Aidha Dkt. Magandi amefafanua kuwa lengo la kuanzishwa kwa hospitali kama ya Mloganzila ni ili kupunguza gharama za kupeleka wagonjwa nje ya nchi na badala yake kuimarisha huduma za afya zinazotolewa na wataalam nchini ili kuweza kutibu magonjwa ambayo hapo mwanzo yalihitaji mgonjwa kupelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
 Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi (kushoto), kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Afya ya Bunge la Korea ya Kusini, Bw. Kim Se-Youn wakisikiliza utambulisho wa wageni waliofika hospitalini hapa.
 Baadhi ya wabunge waliofika hospitali ya Mloganzila wakisikiliza mambo mbalimbali yaliyokuwa yakizungumzwa katika kikao hicho.
Mtaalam wa mashine ya CT-Scan, Dkt. Charles Nchimbi akiwaelezea wageni jinsi mashine hiyo inavyofanya kazi.
 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Afya ya Bunge la Korea ya Kusini, Bw. Kim Se-Youn amesema kuwa wamefurahishwa na namna hospitali inavyohakikisha kuwa jamii inayowazunguka inapata huduma bora za afya.
“Tumefurahi sana kuitembelea hospitali hii na tunatumaini kuwa hospitali ya Mloganzila itaendelea kushirikiana na Serikali yetu ya Korea katika kuhakikisha huduma bora za afya zinatolewa kwa watanzania,” Amesema Bw. Kim.

Wageni hao wametembelea kitengo cha magonjwa ya dharura (EMD), radiolojia pamoja na maabara na kujionea namna wataalam wanavyofanya kazi.

No comments:

Post a Comment