Waziri
wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ameiagiza Bodi na Menejimenti ya Shirika la
Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha kuwa wanafanya tafiti kubaini vyanzo vipya
vya uzalishaji umeme ili kuongeza kiasi cha nishati hiyo nchini na kuweza
kufikia lengo la kuwa na megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.
“Lazima
tufanye tafiti kubaini vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme ukiacha hivi
vilivyopo, hata kama tusipotekeleza leo, vizazi vijavyo vitatekeleza miradi
hiyo, mfano tafiti za mradi wa umeme wa Julius Nyerere (MW 2115) zilifanyika
miaka mingi iliyopita, lakini mradi tunautekeleza sasa, hivyo nasi hatuna budi
kuibua vyanzo vingine.” Alisema
Aidha,
Dkt Kalemani aliiagiza Bodi na Menejimenti ya TANESCO kuhakikisha kuwa maeneo
yote nchini yanaunganishwa na umeme wa Gridi ifikapo mwezi Juni 2022 ili
wananchi wapate umeme wa uhakika na pia Serikali kuokoa fedha zinazotumika
kununulia Mafuta ili kuendesha mitambo ya umeme kwenye baadhi ya maeneo nchini.
Kuhusu
kazi ya usambazaji umeme vijijini, alisisitiza kuwa lengo la Serikali ni
kufikisha umeme kwenye vijiji vyote ifikapo mwezi Juni mwaka 2021 na asilimia 85 ya wananchi wanapata umeme hivyo TANESCO ina
jukumu la kuhakikisha kuwa lengo hilo linafanikiwa.
Vilevile,
Dkt Kalemani aliiagiza TANESCO kuhakikisha kuwa, kila kiwanda au Taasisi ya
umma inapojengwa, inafikishiwa umeme lengo likiwa ni kuongeza mapato ya Shirika
na pia kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii nchini.
Aidha,
aliiagiza Bodi na Menejimenti ya TANESCO kuongeza ukusanyaji wa mapato ya
Shirika kutoka shilingi Bilioni 46 zinazokusanywa sasa kwa wiki hadi kufikia
Bilioni 52 kwa Wiki.
Dkt.
Kalemani aliongeza kuwa, Shirika hilo pia linapaswa kumaliza madeni yake
ifikapo mwaka 2026, linaboresha nidhamu ya watumishi ili kuweza kutoa huduma
bora kwa wananchi na kuhakikisha kunakuwa na mpango wa ukarabati wa miundombinu
ya umeme kwenye maeneo yote nchini.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, pamoja na kuipongeza
TANESCO kwa majukumu mbalimbali wanayofanya, aliiagiza Bodi kujielekeza pia
kwenye ukusanyaji wa madeni ya TANESCO kutoka kwa wateja mbalimbali zikiwemo
Taasisi za umma kwani fedha zitakazopatikana zitasaidia Shirika kuweza
kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Aidha,
aliiagiza TANESCO kuangalia suala la malipo ya huduma ya umeme ili kuwe na
utaratibu wa malipo hayo kufanyika kwa awamu ili kuweza kuunganishia umeme
wananchi wengi zaidi na hivyo miradi hiyo ya umeme kuleta tija.
Kamishna
Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga, alisema kuwa, hali ya umeme nchini
imeimarika hivyo TANESCO inapaswa kujikita pia kwenye kazi ya kuongeza wateja
wa nishati hiyo ili kuongeza mapato.
Vilevile,
alisisitiza kuhusu suala la mikoa yote nchini kuunganishwa na gridi ya Taifa
ili kuimarisha hali ya umeme kwenye mikoa hiyo.
No comments:
Post a Comment