Matokeo chanyA+ online




Friday, December 20, 2019

KATIBU MKUU MWALUKO AWATAKA WATAALAM WA MAAFA KUTUMIA FURSA ZA MAFUNZO KWA MATOKEO CHANYA


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu na Uwekezaji, Dorothy Mwaluko amewataka wataalam wa masuala ya Maafa nchini kutumia fursa za mafunzo ya masuala ya maafa kwa kuhakikisha wanaleta tija katika kukabili majanga ya mafuriko na ukame.
Ametoa kauli hiyo Desemba 18, 2019 alipokuwa akifungua warsha ya mafunzo ya siku tatu kuhusu upunguzaji wa madhara ya janga la mafuriko na ukame yaliyofanyika Jijini Dodoma iliyoandaliwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupunguza Madhara ya Maafa ya kwa kushirikiana na Idara ya Menejimenti ya maafa Ofisi ya ofisi hiyo.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji) Bi. Dorothy Mwaluko akihutubia wakati wa warsha ya mafunzo kuhusu upunguzaji wa madhara ya janga la mafuriko na ukame iliyofanyika kuanzia tarehe 18 hadi 20 Desemba, 2019 katika Ukumbi wa Mikutano wa Dodoma Hotel Jijini Dodoma. 
Mwaluko aliwataka wataalam hao kutumia fursa za mafunzo kuhakikisha wanaandaa taarifa za wasifu wa nchi utakao bainisha maeneo yenye mafuriko na ukame ili kuwa msaada kwa vizazi vijavyo.
 “Taarifa hizi mnazoandaa hakikisheni mnawafikia walaji kwa kuzingatia matumizi sahihi ya lugha rahisi yenye kueleweka kwa walengwa ili kuwa na taarifa sahihi kuhusu masuala ya menejimenti ya maafa,”alieleza Mwaluko.
Aliongezea kuwa, wanapaswa kuifikia jamii kwa vitendo na si kushiriki katika vikao na warsha zisizoleta tija kwa kukosa matokeo chanya.
 “Hakikisheni mnatumia fursa ya warsha hii kuchakata vyema taarifa hizi ili kuleta matokeo chanya katika jamii yenye matarajio makubwa na Serikali yake,”alisisitiza Mwaluko.

Mwezeshaji wa masuala ya maafa kutoka Taasisi ya Tafiti ya CIMA Bw. Roberto Rudari akiwasilisha mada kuhusu masuala ya menejimenti ya maafa wakati wa mafunzo hayo.

Aidha alifafanua kuwa, wataalam hao wanawajibu wa kutumia ujuzi wao katika kutoa taarifa sahihi kwa wakati kwa kuzingatia athari za ukame na mafuriko nchini na kuwataka kuacha kutumia majukwaa ya makongamano kujifunza pekee pasipo kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi.
“Ni Lazima tufike mahali tuwe watekelezaji na si wazungumzaji, kwa kukaa kwenye viti vizuri wakati watumiaji wanaangamia hivyo ni lazima mkitoka katika mafunzo haya mje na mikakati inayofikika katika kukatua changamoto hizi za majanga nchini,”Alisisistiza
Kwa upande wake mwakilishi kutoka Taasisi ya Utafiti ya CIMA Bw. Roberto Rudari alieleza lengo la kuwakutanisha wataalam hao ni kuhakikisha wanawajengea uwezo juu ya masuala ya kuzuia madhara yatokanayo na majanga ya ukame na mafuriko kwa kuzingatia Tanzania ni miongozni mwa nchi zinazokubwa na aina hizo za majanga.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji) Bi. Dorothy Mwaluko (wa tatu kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya upunguzaji wa madhara ya janga la mafuriko na ukame yaliyoandaliwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupunguza Madhara ya Maafa ya UNDRR kwa kushirikiana na Ofisi yake Jijini Dooma. 
Alifafanua kuwa, taarifa hizi zitaisaidia nchi kuhakikisha wanaweka mazingira rafiki yenye lengo la kuratibu na kukakikisha majanga hayo yanapungua nchini.
Naye mtaalam wa masuala ya maafa kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. James Hela alieleza ni vyema taarifa za masuala ya majanga zikatolewa kwa wakati ili kusaidia kujipanga na kuhakikisha jamii haipati madhara ya majanga hayo.
“Kwa sasa kuna mabadiliko ya tabia nchi na ni vyema taarifa hizi zikaandaliwa kwa lugha rafiki na kuhakikisha inawafikia walengwa ili kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya Tano katika kuwatumikia Watanzania,”alisema Hela.
Aidha, Mhadhiri kutoka Idara ya Jiografia na Stadi za Mazingira kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma Dkt. Wilhelm Kiwango alipongeza jitihada za ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuandaa mafunzo hayo kwani yameongeza uelewa wa jumla juu ya vihatarishi na maeneo yanayoathiriwa na maafa na kutoa wito kwa Serikali kuendelea kutoa elimu hiyo katika ngazi zote na umma kwa ujumla.
“Mafunzo haya yametufaa, ni vyema yakatolewa katika ngazi zote na kusaidia kuongeza uelewa hususan kuimarisha mtaala wa elimu ya maafa ngazi zote hadi vyuo vikuu,”alieleza Dkt. Kiwango

No comments:

Post a Comment