Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, amezindua
Kituo cha Kupokea na Kutawanya Njia Kuu za Umeme (Switching Station) kilichopo
katika kijiji cha Ng’ami, eneo la Viwandani, wilayani Bariadi, Mkoa wa Simiyu.
Uzinduzi huo umefanyika Desemba 15, 2019 ambapo Kituo
hicho kinachukua umeme kutoka Kituo Kikuu cha Mabuki kilichopo Wilaya ya
Misungwi, mkoani Mwanza umbali wa kilomita 87.2, kupitia Njia ya kusafiri umeme
ya Msongo wa kV 33.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ( mwenye shati la bluu) akisalimiana na watumishi mbalimbali wa Mkoa wa Simiyu mara baada ya kufika katika uzinduzi wa Kituo cha Kupokea na Kutawanya Njia kuu za Umeme kilichopo eneo la Ng’ami wilayani Bariadi mkoani humo. |
Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya uzinduzi
huo, Dkt Kalemani, alisema kituo hicho kimezinduliwa rasmi kwa lengo la
kuimarisha hali ya upatikanaji umeme katika Mkoa wa Simiyu ambao
umejikita katika uwekezaji wa Viwanda , na hivyo unahitaji umeme wa uhakika.
Kutokana na uwepo wa Kituo hicho, Dkt. Kalemani
alisema “natoa agizo kwa Meneja wa Mkoa, mtafute eneo la kiwanja hapa, mjenge
eneo la makazi kwa ajili ya mtumishi atakayekiangalia kituo hiki kwa masaa 24,
kwa sababu ikitokea dharura haitowezekana mtu kutembea kilomita 10 kuja hapa
hivyo ni lazima mtu akae hapa.”
Aidha, Dkt Kalemani alitoa wito kwa Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu, Anthony Mtaka, kuwahamasisha
wananchi wa eneo hilo kutunza miundombinu ya kituo husika ili wananchi
wasifanye uharibu wa aina yoyote katika eneo hilo, ambalo ni muhimu kwenye
maendeleo ya shughuli mbali mbali za kiuchumi.
Vile vile, alisema ifikapo mwezi Machi mwakani Kituo
Kikuu cha Kupoza umeme cha Imalilo kilichopo wilaya ya Bariadi, mkoani humo nacho
kitakuwa kimekamilika ambapo kitawezesha wananchi wa Mkoa huo na maeneo ya
jirani kupata umeme wa uhakika na wakutosha kwa ajili ya matumiza ya kawaida
na Viwanda vilivyopo mkoani humo.
Aidha, alisema kuwa, Serikali imetoa zaidi ya shilingi
bilioni 4 kwa Mkoa huo ambazo zinatumika kwa ajili ya kufanya ukarabati wa
miundombinu ya umeme iliyoharibika na kusambazia umeme katika maeneo ambayo
bado hayajapata umeme.
Eneo la Kituo cha Kupokea na Kutawanya Njia kuu za Umeme kilichopo katika eneo la Ng’ami wilayani Bariadi mkoani Simiyu. |
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka aliishukuru
Serikali kwa kazi kubwa inayofanya ili kuhakikisha umeme unapatikana nchi
nzima.
Alisema, Mkoa huo unaenda kwenye Mapinduzi ya
Viwanda kwa haraka na ujio wa kituo hicho utaharakisha maendeleo ya Viwanda mkoani
humo.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nyasosi wilayani Bariadi kabla ya kuwasha umeme katika eneo hilo. |
Aliongeza kuwa, wawekezaji waliofika mkoani Simiyu
walitaka wajenge viwanda karibu na eneo ambalo lipo karibu na kituo hicho cha
umeme na Serikali imeridhia ombi hilo.
Katika ziara yake mkoani humo, Waziri wa Nishati, alitembelea
eneo kutakapojengwa Kituo cha Kupoza Umeme, Imalilo wilayani Bariadi na kuwasha
umeme katika kijiji cha Nyasosi kilichopo wilayani humo.
No comments:
Post a Comment