Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamuhanga amepongeza juhudi zinazofanywa
na watumishi kituo cha afya cha Mazwi, Manispaa ya Sumbawanga baada ya kuona namna
wanavyokabiliana na ongezeko la wateja wanaohitaji huduma za afya katika kituo
hicho ambacho huzalisha wajawazito wapatao 373 kwa mwezi.
Amesema kuwa kabla ya hapo kituo hicho kilikuwa kidogo
sana na kushindwa hata kutoa huduma za upasuaji jambo ambalo lilipelekea
hospitali ya rufaa ya mkoa kuzidiwa na wagonjwa lakini hali hiyo kwa sasa ni
tofauti baada ya upanuzi wa kituo hicho ambacho kutokana na huduma zake wateja
wengi huvutiwa kufika na kupata huduma.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamuhanga |
Amesema kuwa serikali inatoa fedha nyingi kupata dawa
pamoja na vifaa tiba hivyo kinachotegemewa katika kituo hicho ni huduma bora ya
afya na kuongeza kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe
Magufuli imejenga vituo vya afya zaidi ya 352 ambapo mojawapo ya vituo hivyo ni
kituo cha afya cha Mazwi katika Makispaa ya Sumbawanga ambapo walipatiwa
shilingi milioni 500 na sasa kituo hicho kimekamilika na kuanza kutoa huduma.
“Nimefurahishwa kwa upanuzi ambao umefanyika katika
kituo hiki cha Mazwi, kilikuwa kituo kidogo tu nakumbuka siku za nyuma lakini
kimekarabatiwa kimekuwa kituo kizuri na kinapendeza lakini kitu cha kufurahisha
ni kwamba kinahudumia wateja wengi lakini na huduma inayotolewa hapa nimetoka
kukagua katika maeneo mbalimbali katika wodi kwakweli nimeridhika na huduma
ambazo zinatolewa, changamoto ni kwamba wameongezeka wateja baada ya ukarabati
kufanyika, tunashukuru wataalamu wetu wanajitahidi kuwahudumia,” Alisema.
Wakati akitoa taarifa ya kituo cha Afya cha Mazwi
Mganga Mkuu wa halmashauri ya manispaa ya Sumbawanga Dkt. Archie Hellar alisema
kuwa kuanzia mwezi Januari hadi Novemba kituo hicho cha afya kimezalisha
wajawazito 4,103 na kati ya hao waliofanyiwa upasuaji ni wajawazito 426 na
kupatikana vifo viwili kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo katika
harakati za kuwafanyia wajawazito hao upasuaji..
“Kwajhiyo changamoto tunazozipata ni kwamba wateja ni
wengi zaidi wanaichukulia hospitali hii ni kama ya mkoa na wengine wanatoka nje
ya manispaa n ahata nje ya Wilaya nyingine kuja kujifungua hapa, sasa
ukilinganisha watumishi pamoja na rasilimali fedha unakuta kituo kinaelemewa,
lakini hata hivyo tunajitahidi kwa kushirikiana na Mkurugenzi wetu wa manispaa
Jacob Mtalitinya kwakweli anatiupa nguvu na kutusaidia sana kufanikisha kutoa
huduma,” Alisema.
Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga ilipata shilingi
milioni 500 za kupanua ujenzi wa kituo cha Afya cha Mazwi pamoja na kupewa
shilingi milioni 400 kwaajili ya ujenzi wa kituo cha Afya kipya kilichopo
katika kata ya Katumba azimio ikiwa ni kilometa 12 kutoka katika kituo cha afya
cha Mazwi.
No comments:
Post a Comment