Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamuhanga amesema kuwa Ofisi ya Rais inaendelea kufanya tathmini kwa
hospitali zote 67 kuhakikisha kwamba shilingi bilioni 100.5 ambazo zilitolewa kwa
ujenzi wa hospitali hizo kuwa zimetumika vizuri.
Alisema kuwa serikali ya awamu ya tano imejenga
hospitali 67 nchini na mkoa wa Rukwa umejengewa hospitali tatu za wilaya ambapo
Mhandisi Nyamuhanga aliweza kutembelea na kujionea maendeleo ya ujenzi wa hospitali
ya Wilaya ya Kalamnbo, katika mji mdogo wa Matai iliyopokea shilingi Bilioni
1.5 lakini hakuridhishwa na ujenzi wa hospitali hiyo.
“Kwa
halmashauri ambazo fedha hizi zitakuwa hazijatumika vizuri kwakweli tutachukua
hatua na katibu tawala wa mkoa kama nilivyoagiza jana, najua kuna vifaa ambavyo
tayari vimeshanunuliwa pale ambavyo bado havijawekwa, havijajengwa kwa mfano
maru maru na vifaa vingine uhakikishe kwamba kazi hiyo inaendelea ili vifaa
hivyo vikishawekwa tuvitathmini sasa kiwango cha ukamilishaji wa hospitali ile
ya halmashauri ya Wilaya ya Kalambo kabla hatujafikiria kutoa fedha nyingine za
kukamilisha,” Alisema.
Ameongeza kuwa halmashauri hiyo ya Kalambo imetaja
mahitaji ya shilingi milioni 700 ili kuweza kukamilisha ujenzi wa hospitali
hiyo jambo ambalo Mhandisi Nyamuhanga hakukubaliana nalo kutokana na tathmini
iliyofanywa ya mahitaji ya fedha walizotoa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali
hizo kuwa yangebaki mambo machache ambayo yasingeweza kuzidi shilingi milioni
300 na kuongeza kuwa anahitaji maelezo ya ziada kutoka katika halmashauri hiyo
ambayo hospitali yake imefikia ukamilifu wa asilimia 76 ambacho ni kiwango cha
chini cha ukamilishaji.
Katika hatua nyingine amesema kuwa mwezi Aprili mwaka
2019 Ofisi ya Rais TAMISEMI ilitoa shilingi milioni 400 kwaajili ya upanuzi wa
Zahanati ya Kijiji cha Samazi katika halmashauri ya Wilaya ya Kalambo ambapo
zahanati hiyo inapandishwa hadhi na kuwa kituo cha Afya lakini amesikitishwa na
malumbano yanayoendelea katika kijiji hicho juu ya eneo la ujenzi wa kituo
hicho jambo lililopelekea kushindwa kuanza kwa ujenzi huo.
“Ofisi ya Rais TAMISEMI imetoa maelekezo kwamba
upanuzi ufanyike katika eneo la zahanati iliyopo iongezewe majengo ili kiwe
kituo cha afya cha Samazi kiweze kukamilika ili kiweze kufanya kazi,
tusiendelee na malumbano tena tumeshatoa maamuzi kwamba upanuzi ufanyike pale
kwenye zahanati ili tukipandishe hadhi ikiwe kituo cha afya, tunategemea kazi
hiyo ianze mara moja na ikamilike ndani ya miezi mitatu,” Alisisitiza.
No comments:
Post a Comment