Serikali
imeuwezesha mkoa wa Mara kujenga Hospitali 4 za Wilaya, Vituo
vya Afya 13 kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Akizungumza
katika kipindi cha ‘TUNATEKELEZA’ Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Adam Malima amesema
mkoa huo umepiga hatua kubwa katika kuimarisha huduma mbalimbali za jamii ikiwemo
sekta ya afya kutokana na kutekelezwa kwa ujenzi wa miundombinu ya sekta hiyo kwa
ufanisi.
“Mradi
wa Hospitali ya Kanda ya Mwalimu Nyerere unaendelea vizuri na utawezesha
wananchi kupata huduma za kibingwa ikiwemo za mifupa na nyingine hali
itakayoondoa adha ya wananchi kusafiri hadi Hospitali ya Bugando kufuata huduma
hizo” Alisisitiza Malima.
Akifafanua
amesema kuwa mkoa huo umepata mafanikio makubwa katika sekta nyingine kama vile
elimu kwa kujenga miundombinu ya kisasa yakiwemo madarasa na maabara hali
iliyochangia kukua kwa kiwango cha elimu katika mkoa huo ikilinganishwa na
miaka iliyotangulia kabla ya uwekezaji huo.
Kwa
upande wa sekta ya madini amesema kuwa kuwepo kwa sheria nzuri na taratibu
zilizowekwa na Serikali ya Awamu ya Tano, mkoa huo umezalisha kilo 130 za
dhahabu kufikia Septemba mwaka huu hali inayochangia kukuza sekta ya madini na
uchumi kwa ujumla.
Akizungumzia
mikakati yake ya kukuza kilimo na uvuvi, Mhe. Malima amesema kuwa dhamira ya
mkoa huo ni kuona sekta hizo zinatoa mchango stahiki katika uchumi kutokana na
hatua zilizochukuliwa katika kokomesha uvuvi haramu katika mkoa huo.
Aidha,
Mhe. Malima amebainisha kuwa wamejipanga kukuza sekta ya utalii katika mkoa huo
ili kuongeza pato la mkoa huo hatua itakayowasaidia kuwainua wananchi kiuchumi
na Taifa kwa ujumla.
Kipindi
cha ‘TUNATEKELEZA’ kinarushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na
kuratibiwa na Idara ya Habari MAELEZO ambapo awamu hii inawashirikisha wakuu wa
mikoa yote Tanzania Bara.
No comments:
Post a Comment