Matokeo chanyA+ online




Tuesday, January 7, 2020

MFUMO WA MALIPO KWA MATOKEO KUIMARISHA MIOUNDIMBINU YA MAJI VIJIJINI

Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa


Serikali  katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 imepanga kutumia Tsh. Bilioni 301 kwa ajili ya kukamilisha miradi ya maji vijijini inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo fedha za ndani ni Tsh. Bilioni 224.03 na fedha za nje ni Tsh. Bilioni 77.22.

Pamoja na juhudi hizo za Serikali sekta ya maji imekuwa inakabiliwa na changamoto ya upotevu wa maji kutokana na uchakavu wa miundombinu iliyojengwa miaka mingi iliyopita.

Katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imeendelea na jitihada za uwekezaji katika ukarabati wa miundombinu chakavu maeneo mbalimbali ya mijini ikiwemo Mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Dodoma, Mwanza, Morogoro, Singida pamoja na ukarabati wa miradi ya kitaifa ya Makonde, Wanging’ombe, Maswa, Mugango Kiabakari na Chalinze.

Tanzania kupitia miradi ya maji vijijini imejenga zaidi ya vituo 80,000 vya maji ambavyo vimeunganishwa na mfumo wa maji ya bomba, ambapo baadhi ya vituo vimechakaa na kuhitaji matengenezo lakini ukosefu wa takwimu sahihi juu ya vituo hivyo kunaikwamisha Serikali kupanga bajeti ya kuwapatia wananchi wa vijijini huduma bora ya maji.

Takwimu zilizopo katika Ripoti ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ya mwaka 2016, zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2010/11 na mwaka 2015/16, Serikali ilipanga kujenga jumla ya vituo vya maji 99,515 lakini ilishia kujenga vituo 42,718 pekee.

Ripoti hiyo iliyotolewa Oktoba mwaka 2016 inaeleza kuwa theluthi moja ya miradi hiyo ya maji haikutekelezwa ndani ya awamu ya kwanza ya Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDPI) jambo lililofanya baadhi ya vituo vya maji vichelewe kujengwa.

Ili kuboresha upatikanaji wa maji maeneo ya vijijini, Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo imeendelea kuimarisha Programu ya Uendelevu wa Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini kwa kutumia Mfumo wa Malipo kwa Matokeo (Payment by Results – PbR) unaolenga kuongeza kasi ya uendeshaji, matengenezo na ukarabati wa miundombinu ya miradi ya maji vijijini.

Kupitia Programu hiyo, Serikali imeanza kuziwezesha Halmashauri za Miji nchini kuviendeleza vituo vya maji vilivyopo na kutumia takwimu kujenga vingine vipya katika maeneo yenye uhitaji mkubwa wa maji.

Ili kufikia malengo ya Programu hiyo, mwaka 2017 wataalamu hao walitembelea vituo 9,0000 katika Halmashauri 56 nchini vijiji ili kujionea hali halisi ya utendaji wa vituo vya maji, ambapo ilibainika kutofautiana kwa taarifa za baadhi ya vituo zilizopo Wizara ya Maji na Umwagiliaji na eneo kilipo ikizingatiwa kuwa maeneo mengi ya vijijini hayana anuani na mitaa yenye mpangilio mzuri.

Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2019/2020, Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa anasema katika jitihada za kuhakikisha miradi ya maji vijijini inakuwa endelevu, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Uingereza (DFID) inatekeleza Mpango wa Mfumo wa Malipo kwa Matokeo (Payment by Results – PbR) ambao una lengo la kuimarisha uendelevu wa miradi ya maji vijijini.

Anasema kuwa hadi April 2019, awamu ya pili ya programu hiyo imekamilika ambapo Halmashauri 95 zilifuzu na kupewa Shilingi bilioni 8.55 kati ya Shilingi bilioni 53.6 zilizotengwa katika mwaka 2017/2018, ambapo awamu ya tatu inaendelea na inahusisha Halmashauri 181 ambazo zitapewa fedha kwa vigezo vya idadi ya vituo vilivyojengwa na kutoa maji.

‘Kupitia PbR, Paundi 300 hutolewa kwa kila kituo kilichohakikiwa na kinachofanya kazi na Paundi 1,500 hutolewa kwa kituo kipya kitakachojengwa, Katika mwaka 2018/2019, jumla ya Paundi milioni 10 zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza programu hiyo kwenye Halmashauri zote nchini’’ alisema Waziri Mbarawa.

Aliongeza kuwa Hadi mwezi Aprili 2019, fedha zilizolipwa katika awamu ya tatu ni Paundi milioni 8.7 sawa na Shilingi bilioni 25.43. Katika mwaka 2019/2020, Shilingi bilioni 46.47 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa programu hiyo.

Maji ni rasilimali muhimu kwa maisha ya binadamu na maendeleo ya jamii na sekta mbalimbali za kiuchumi zikiwemo viwanda, kilimo, uvuvi na utalii, ili kufikia azma ya Serikali ya kuwapatia wananchi majisafi na salama pamoja na kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati kufikia mwaka 2025, Wizara inatekeleza mipango mbalimbali.

Ni wajibu wa wananchi na wadau wote kuhakikisha kunakuwepo na upatikanaji wa takwimu na taarifa za mwenendo wa rasilimali za maji ili kuimarisha usanifu wa miundombinu ya kusambaza maji nchini. 
Na Ismail Ngayonga,MAELEZO

DAR ES SALAAM

No comments:

Post a Comment