Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo
amesema kuwa wanaopinga utaratibu wa vifurushi vya bima ya afya hawawatakii
mema watanzania.
Hayo ameyasema leo wakati akizindua mpango
wa uhamasishaji wa wananchi kujiunga na NHIF kupitia vifurushi vipya katika
soko la Mbauda jijini Arusha.
"Ukisikia mtu anapinga mpango huu
hakutakii mema kwani pindi unapopatwa na matatizo hatakuja kukusaidia hivyo
tuwapuuze na tujiunge na mapango huu wa bima ya afya," alisema Mhe. Gambo.
“Gharama za matibabu kwasasa ni kubwa sana,
unaweza kwenda hospotali gharama za matibabu zikawa ni kubwa kuliko kifurushi
cha bima ya afya, ndugu zangu tujiunge na mpango huu ili tuwe na uhakika wa
matibabu wakati wowote”-Alisisitiza Mhe. Gambo.
Kutokana na umuhimu huo amewataka viongozi wa mkoa pamoja na viongozi wa dini
kushirikiana kwa pamoja katika kuwahimiza na kuwakumbusha wananchi juu ya kuwa
na bima ya afya.
Alisema mpango wa vifurushi vya bima ya afya unamwezesha
mwananchi kupata tiba popote pale nchini bila ya usumbufu wowote.
"Bima ya Afya chini ya uenyekiti wa
Mhe. Mama Anne Makinda imekuwa ni bima ya afya iliyoimara sana, nakupongeza
sana kwa kazi kubwa uliyoifanya wewe na bodi yako," alisema.
Alisema kuwa pamoja na Serikali ya Awamu ya
Tano kuboresha Mfumo wa Bima ya Afya pia imeendele kuboresha miundombinu ya
maeneo ya kutolea huduma ili mwananchi
anapokuwa na kadi yake ya bima anakuwa na uhakika wa matibabu na yenye
kiwango bora.
"Mimi ni balozi mkubwa sana wa mpango
huu wa bima ya afya kwasababu najua umuhimu wake hasa wakati mtu anapopatwa na
maradhi, unapokuwa na kadi unakuwa na amani ndani ya familia yako wakati
wote," alisema.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF, Mama Anne
Makinda amesisitiza wananchi juu kuweka kipaumbele katika suala zima la bima ya
Afya ndani ya familia zao.
"Ukifanya kazi matumizi ya kwanza iwe
afya yako, tusiweke rehani maisha yetu, hautaweza kuwa na maendeleo kama hauna
uhakika wa huduma za matibabu," alisema Mama Makinda.
Alisema kuwa kadi ya vifurushi inamuwezesha
mwanachama kupata huduma za matibabu popote anapokuwa ndani ya nchi.
No comments:
Post a Comment