Matokeo chanyA+ online




Tuesday, February 25, 2020

RC RUKWA AZIPA MAJUKUMU KAMATI ZA ULINZI WA WANAWAKE NA WATOTO

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Joachim Wangabo amezitaka Kamati za ulinzi wa Wanawake na Watoto za Mkoa huo kuweka nguvu katika kuhakikisha wanatoa elimu itakayosidia kuondokana na vitendo vya ukatili.

Hayo yamesemwa  Wilayani Sumbawanga Mkoani Rukwa na Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mhe. Julieth Binyula kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wakati akiupokea Msafara wa kijinsia wa kutokomeza ukatili wa kijinsia.
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ambaye ni Mkuu wa Wilaya Kalambo Mhe. Julieth Binyula akizungumza wakati Msafara wa kutokomeza ukatili wa kijinsia ulipokuwa mkoani humo.
Msanii Nurdin Bilal Shetta na G Nako wakiimba katika viwanja vya Soko la Mandela  katika Wilaya ya Sumbawanga Mkoani Rukwa kwenye Msafara wa kutokomeza ukatili wa kijinsia.

Ameongeza kuwa Mkoa wa Rukwa umekuwa na changamoto kubwa ya Mimba na ndoa za utotoni hivyo nguvu kubwa inahitajika hasa ya kuelimisha wananchi kutambua madhara ya kuwapa mimba na kuwaozesha watoto na wanafunzi.

 
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ambaye ni Mkuu wa Wilaya Kalambo Bi. Julieth Binyula akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii  Mkoa wa Rukwa na Wasanii wakati Msafara wa kutokomeza ukatili wa kijinsia ulipokuwa Mkoani humo.
Mhe. Julieth amewataka wananchi wa Mkoa wa Rukwa kutoa taarifa za vitendo vya ukatili vinavyojitokeza katika familia na mitaa yao ili kuwezesha Serikali kuchukua hatua dhidi ya wanaofanya vitendo hivyo.

Ameongeza kuwa Mkoa wa Rukwa umekuwa na takwimu kubwa za vitendo vya ukatili hasa mimba na ndoa kwa watoto na wanafunzi hivyo nguvu kubwa inahitajika  kuhakikisha vitendo hivyo vinatokomezwa.

 
Wananchi waliojitokeza katika Msafara wa kutokomeza ukatili wa kijinsia uliosimama katika Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Katibu Mkuu Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Imelda Kamugisha amesema kuwa Wizara imeamua kuwa na msafara huo ili kutoa elimu kwa ukaribu zaidi kuhakikisha wananchi wanakuwa na uelewa wa kuwezesha kuibua vitendo vya ukatili hasa katika familia.

"Niseme jamii zetu zimepata muamko ila zinahitaji muamko zaidi ndio maana tumeamua kuja na Msafara huu ambao utasaidia kutoa muamko kwa wananchi katika kutoa taarifa ya vitendo vya ukatili" alisema

 
Mwanasheria kutoka Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Happy Msimbe na Afisa Ustawi wa Jamii Caren Mitta wakitoa huduma kwa mkazi wa Wilaya ya Mpanda wakati Msafara wa kijinsia wa kutokomeza ukatili uliposimama Wilayani hapo
Bi. Imelda amewaasa Watanzania kuungana kwa pamoja katika kuhakikisha wanapambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika maeneo yao ili kuweza kuwa na jamii yenye ustawi hasa kwa maendeleo ya watoto na wanawake.
 
Mwakilishi wa Katibu Mkuu Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Imelda Kamugisha akielezea lengo la msafara wa kutokomeza ukatili wa kijinsia wakati Msafara huo uliposimama Wilayani Sumbawanga Mkoa wa Rukwa.
Naye Meneja Miradi Shirika la Legal Services Facility Bw. Joseph Maganza ametoa wito kwa wadau kushirikiana na Serikali ili kuendeleza mapambano ya kuondokana na vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa katika maeneo ambayo hayana wadau wa kutosha wa kuweza kushirikiana na Serikali katika mapambano hayo.
 
"Sisi wadau tunaweka nguvu hasa katika kuhakikisha tunasaidiana na Serikali  kuondokana na tatizo hili la ukatili wa kijinsia" alisema.

No comments:

Post a Comment