Serikali ya
Tanzania imeweka wazi mipango na mikakati yake ya ufanikishaji wa malengo ya
makubaliano ya kukuza uzalishaji, kujenga miundombinu na usambazaji wa nishati
katika Nchi 15 za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) yaliyofikiwa na
Viongozi Wakuu wa Kitaifa na Mawaziri wa sekta ya Nishati katika Jumuiya hiyo
Mwezi Agosti mwaka 2019.
Akizungumza
katika ufunguzi wa mkutano wa wataalamu wa nishati kutoka Nchi za SADC
unaoendelea Jijini Dar es Salaam leo Jumanne (Februari 25, 2020), Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi
Zena Said alisema mkutano huo unalenga kuanisha vyanzo na miradi mbalimbali ya
kimkakati itakayowezesha utoshelevu wa nishati katika nchi za SADC.
Mhandisi Zena
alisema kupitia Mkutano wataalamu wa sekta ya nishati wa Tanzania wataweza
kubainisha fursa zilizopo katika kuhakikisha utoshelevu wa sekta ya nishati nchini
ikiwemo Ujenzi wa Mradi Bwawa la
kuzalisha Umeme kwa Kutumia maporomoko ya maji ya Bonde la Mto Rufiji wa Julius
Nyerere (JNHPP) unaotarajia kuzalisha unaotarajia kuzalisha Megawati 2115.
‘’Tumeshuhudia majanga mbalimbali yanayotokana na mabadiliko ya baia
nchi, sasa wataalamu wetu wa masuala ya nishati, mafuta na gesi watakutana na
kujadili kwa pamoja ili kupata njia bora zaidi za kuweza kuzalisha nishati ya
umeme itakayoweza kuwasaidia wananchi wetu’’ alisema Mhandisi Zena.
Alisema mipango
na mikakati ya kuimarisha sekta ya nishati katika ukanda wa SADC ni utekelezaji
wa maagizo yaliyotolewa na Viongozi wa Kitaifa na Mawaziri wa sekta ya nishati katika
Jumuiya ya SADC na Tanzania imepanga kuutumia vyema mkutano huo ili kuhakikisha
kuwa sekta ya nishati inakuwa ya kibiashara na hivyo kuweza kutengeneza fursa
kwa Watanzania.
Kwa mujibu wa
Mhandisi Zena alisema mkutano huo wa wataalamu unatarajia kuhitimishwa mwishoni
mwa wiki hii, ambapo mwezi Mei mwaka huu kunatarajia kufanyika Mkutano wa Baraza
la Mawaziri wa sekta ya nishati katika Nchi wanachama wa Jumuiya ya SADC, ili
kuona namna bora zaidi ya utekelezaji wa miradi hiyo ili iweze kuleta tija na maendeleo
endelevu kwa wananchi wa ukanda wa SADC.
Aliongeza kuwa mbali na miradi hiyo ya kimkakati, wataalamu hao hao pia
watajadili fursa za nishati jadidifu na namna zinavyoweza kuongeza uwezo wa
upatikanaji wa nishati ya umeme ili kuwawezesha wananchi wa ukanda wa SADC
kuweza kuwa na nishati ya uhakika na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa
yanayochangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira.
Kwa upande wake Kamishna wa Nishati na Gesi kutoka Wizara ya Nishati,
Adam Zuberi alisema mkutano huo umeshirisha jumla ya nchi wanachama 12 wa
Jumuiya hiyo, ambao wanaandaa maazimio mbalimbali yanayotarajiwa kujadiliwa
katika Baraza la Mawaziri wa sekta ya Nishati wa Jumuiya hiyo mwezi Mei mwaka
huu.
Aliongeza kuwa katika mkutano huo, wataalamu hao pia watapata fursa ya
kushiriki semina zitakazohusisha uwasilishaji wa mada na makongamano mbalimbali
ya wadau wa sekta ya nishati ndani ya ukanda wa SADC.
No comments:
Post a Comment