Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor
Mpango, amewaagiza Wataalamu wa Wizara hiyo kushirikiana na Benki Kuu ya
Tanzania (BoT) kuangalia madhara ya Corona yanayoweza kujitokeza katika uchumi
wa nchi pamoja na namna ya kukabiliana nayo.
Agizo hilo amelitoa jijini Dodoma alipokuwa
akizungumza na watumishi wa Wizara hiyo kuhusu umuhimu wa kujikinga na Virusi
vya Corona vinavyosababisha ugonjwa hatari wa COVID-19.
“Nilikuwa naangalia taarifa ya Tume ya Uchumi ya
Afrika “Economic Commission of Africa” inayoelezea madhara ya ugonjwa wa COVID
19 unaosababishwa na Virusi vya Corona, kwa kweli inatisha, wanasema uchumi wa
Africa unaweza ukaanguka na kufikia asilimia 1.8, wastani huwa ni asilimia
3.2”, alisema Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango alisema kuwa ugonjwa huo ni hatari ni vema
Taifa liandaliwe upande wa uchumi ili kujiweka sawa ma kutafuta namna ya
kuchukua hatua katika kukabiliana na madhara yanayoweza kutokea kiuchumi
hususani kwenye biashara na utalii.
Aliwataka Watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango
kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo kwa kuzingatia taratibu za afya
katika maeneo ya kazi na kwenye familia zao.
“Kila mmoja ana wajibu binafsi, wajibu katika familia
na wajibu kazini ili tuendelee kukaa salama. Sitapenda kupoteza mtumishi hata
mmoja wala mtumishi kupoteza mwanafamilia wake kutokana na ugonjwa huu”,
alisema Dkt. Mpango.
Aliwaasa watumishi kuchukua tahadhari kwa kuiga mfano
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, wa kuacha mazoea ya kushikana mikono wakati wa kusalimiana.
“Kiafrika unaonekana unaringa kweli usipompa mtu
mkono, lakini kwa dharura tuliyonayo, muwafundishe na watoto wenu hakuna
kupeana mikono” alisisitiza Dkt. Mpango.
Na. Farida
Ramadhani na Saidina Msangi, WFM, Dodoma
Alifafanua kuwa katika kupambana na ugonjwa huo,
Wizara imeweka Kemikali maalum ya kunawia mikono (Sanitizer) inayoweza kuua vijijidudu
kwenye maeneo mbalimbali ya Majengo ya Wizara hiyo, hivyo aliwataka watumishi
wahakikishe wanaitumia wakati wanapoingia ofisini na kwa wenye uwezo wainunue
kwa ajili ya matumizi ya familia zao.
Aidha, Aliwataka watumishi hao kutoa elimu ya afya kwa
familia zao pamoja na kuepuka mikusanyiko na safari zisizokuwa za lazima za
ndani na nje ya nchi ili kujikinga na ugonjwa huo.
Alisema ugonjwa huu ni kama vita na kwasasa kwani
umeshafika katika nchi jirani za Kenya na Rwanda, hata hivyo alibainisha kuwa,
kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Wizara ya Afya, Tanzania iko salama.
No comments:
Post a Comment