Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Dkt Angeline Mabula amewataka Makamishna Wasaidizi wa Ardhi wa mikoa
kushirikiana na wakuu wa wilaya katika kutekeleza majukumu yao ili kufanya kazi
kwa ufanisi na kuondoa migogoro ya ardhi.
Dkt,Mabula alitoa kauli
hiyo jana alipokutana katika kikao maalum na Makamishna Wasaidizi wa ardhi wa mikoa
jijini Dodoma ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuanzishwa ofisi za ardhi za mikoa
ikiwa ni jitihada za Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kurahisisha
utoaji huduma za ardhi na kupunguza migogoro.
Alisema, ni vizuri
Makamishna wasaidizi wa Ardhi wa mikoa walioteuliwa kutumia nafasi zao kushirikiana na Wakuu wa wilaya na ofisi za
Wakuu wa mikoa sambamba na kutoa elimu kuhusiana na masuala ya ardhi ili
kuwajengea uelewa na ikiwezekana kuwapatia sheria za ardhi ili kupunguza
migogoro ya ardhi.
Aidha, aliwataka
watendaji hao wapya wa ardhi wa mikoa ya Tanzania Bara kusisitiza utendaji kazi
kwa ushirikiano kati ya wataalamu wa sekta ya ardhi na kutolea mfano maafisa ardhi
wanaweza kushirikiana na wataalamu wa fani nyingine za ardhi katika kuandaa
hati.
‘’Siyo afisa ardhi
pekee anaweza kushiriki katika uandaaji hati bali wataalamu wengine wa sekta
hiyo nao wanaweza kushiriki kazi hiyo maana wote wamesoma chuo kimoja na hilo
limefanyika kwa baadhi ya maeneo’’ alisema Naibu Waziri Mabula
Aliwataka Makamishna
hao Wasaidizi wa Ardhi wa mikoa kuhakikisha panakuwepo mawasiliano kutoka Afisa
mmoja kwenda kwa mwingine kwenye majalada ya ardhi na kuipongeza ofisi ya ardhi
ya Kanda ya Ziwa kwa kutoa mafunzo kwa watunza kumbukumbu wa ardhi katika ofisi
za halmashauri za kanda hiyo baada ya kuona watendaji wake kutofanya vizuri.
Akizungumzia utoaji
hati za ardhi, Dkt Mabula alitaka kasi ya utoaji hati iongezeke na kubainisha
kuwa ni vizuri waendaji hao wapya wa ardhi wa mikoa kuwasiliana na wakurugenzi
wa halmashauri ili hati zitolewe kwa pamoja badala ya kila mmiliki kuifuta
katika ofisi za Kanda au mkoa.
Vile vile, alisisitiza
suala la upimaji maeneo yate ya umma na kupatiwa hati kwa lengo la kuepuka
migogoro inayoweza kusababishwa na uvamizi wa maeneo hayo kutokana na
kutopimwa.
Aidha, Dkt Mabula aliwataka
makamishana hao Wasaidizi wa Ardhi wa Mikoa kuhakikisha wakati wa utendaji wao wanatilia
mkazo ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi sambamba
na kuingiza viwanja vyote kwenye mfumo wa kielektronik.
Kamishana Msaidizi wa
Ardhi Mkoa wa Shinyanga Hezekiel Kitlya aliishukuru Wizara ya Ardhi kwa uamuzi
wa kuanzisha ofisi za ardhi za mikoa na kueleza kuwa ofsi hizo zitasaidia sana
kutoa huduma za ardhi kwa wananchi sambamba na kupunguza migogoro ya ardhi.
Kwa mujibu wa Kitlya,
ili ofisi hizo za ardhi za mikoa ziweze kufanya kazi zake kwa ufanisi kuna haja
kwa wizara kuhakikisha ofisi hizo zinapatiwa vifaa pamoja na wataalamu wa kutosha
ili kukidhi mahitaji yote ya sekta ya ardhi.
Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
No comments:
Post a Comment