Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge amekabidhi
pikipiki 28 kwa maafisa tarafa wa mkoa huo huku akiwatahadharisha
kutothubutu kuzitumia kwa biashara ya Bodaboda.
Pikipiki
hizo ni miongoni mwa pikipiki 448 zilizonunuliwa na serikali kwa
gharama ya sh bilioni moja na kugaiwa kwa maafisa tarafa nchini.
![]() |
Baadhi ya pikipiki zilizotolewa na serikali kwa ajili ya maafisa tarafa |
Akikabidhi
pikipiki hizo Machi 21 kwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Patrobas
Katambi kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya wa mkoa huo,Dkt Mahenge amesema
serikali imejitahidi kuondoa changamoto ya usafiri iliyokuwepo awali
hivyo matarajio yake ni kuona utendaji kazi unaenda kuimarika na sio
vinginevyo.
“Maelekezo
yangu kwenu, hizi ni pikipiki ni za kazi za Serikali, sio pikipiki za
bodaboda, matokeo yake tunatarajia kuona Maafisa Tarafa mnafika kwenye
maeneo yenu yote na kuwasilisha taarifa ya kazi mbalimbali kwenye maeneo
yenu na kusimamia utoaji wa huduma za kijamii, kiuchumi na
kiutawala.”alisema Dkt. Mahenge.
Amemuagiza
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Gilles Muroto, kuwaelekeza Wakuu wa
Polisi wa Wilaya zote mkoani humo kuwakamata na kuwachukulia hatua za
kisheria Maafisa Tarafa wote watakao zitumia pikipiki hizo za kwa
kufanyia biashara binafsi badala ya kuzitumia kuwafikia wananchi kwenye
maeneo yote ya Tarafa zao.
Dkt
Mahenge amesema serikali imefanya mengi kwenye sekta za afya,
miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege,sekta ya anga, reli, usafiri
wa majini, nishati, madini, elimu, ukusanyaji mapato na sasa katika
kuboresha utendaji wa serikali.
![]() |
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge akimkabidhi pikipiki Mkuu wa wilaya ya Dodoma Mjini Patrobas Katambi kwa ajili ya maafisa tarafa wa mkoa huo |
"Tunaona
serikali imeimarisha utendaji kazi wa Maafisa Tarafa ambao ni kiungo
muhimu kwa kuwawezesha usafiri wa pikipiki,hili ni jambo kubwa
sana,"aliongeza.
Kwa
upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Kessy Maduka amesema Mkoa
wa Dodoma una jumla ya Tarafa 28 na pikipiki hizo zinaenda kuimarisha
uwezo wa kuwafikia wananchi wote kwenye maeneo yao na kuongeza ufanisi
katika kusimamia shughuli za serikali.
Akipokea
Pikipiki hizo Katambi amesema changamoto kubwa iliyokuwa inawakabili
Maafisa Tarafa katika kusimamia na kutekeleza shughuli za Serikali
kwenye ngazi za Tarafa ilikuwa ni ukosefu wa Usafiri.
"Ndugu zangu niwaombe mkatunze vitendea kazi hivi,sitegemei kuona siku mbili vyombo hivi vimeharibika,"alisema Katambi.
Akishukuru
kwa niaba ya Maafisa Tarafa wote Mkoani Dodoma,Afisa Tarafa wa Zuzu
jijini Dodoma Lucas Mbise amesema pikipiki hizo ni ahadi ya Rais
Magufuli aliyoitoa Juni 4, 2019 alipokutana nao Ikulu Jijini Dar es
Salaam.
"Mheshimiwa
Rais alituahidi na kupitia serikali yake ametekeleza,tunamshukuru sana
na tumuahidi kuchapa kazi kama kauli mbiu yake inavyosema ya hapa kazi
tu,"alisema Mbise.
No comments:
Post a Comment