Waziri
wa Nishati Dkt Medard Kalemani na Ujumbe wake, wakikagua maendeleo ya ujenzi
unaolenga kupanua Kituo cha kupoza umeme cha Singida, akiwa katika ziara ya kazi
Aprili 18, 2020.
|
Veronica Simba – Singida
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amekagua
utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme mkoani Singida huku akitahadharisha
kuwa uwepo wa janga la Corona (COVID 19) nchini usitumike kama kisingizio cha
kukwamisha miradi hiyo.
Akizungumza kwa nyakati tofauti akiwa katika ziara
hiyo, Aprili 18 mwaka huu, Dkt Kalemani alisisitiza kuwa ni lazima watekelezaji
wa miradi husika kufuata maelekezo ya Rais John Magufuli na wataalamu wa afya
katika kujikinga na Corona lakini ni lazima pia kuendelea na kazi.
“Corona ipo, ni lazima tuchukue tahadhari zote za
kujikinga kama tunavyoelekezwa lakini kwa upande mwingine maisha inabidi
yaendelee hivyo tunawajibika kuendelea kufanya kazi.”
Mafundi
wakiendelea na kazi za ujenzi wa kituo cha kupoza umeme Singida. Taswira hii
ilichukuliwa wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo
pichani), Aprili 18, 2020.
|
Akieleza kwa kina dhamira ya ziara yake, Dkt Kalemani
alisema yeyé pamoja na viongozi wenzake wa sekta ya nishati, wanalazimika
kufanya ziara hizo ili kuhakikisha wakandarasi na wasimamizi wa miradi husika
hawabweteki na kutelekeza kazi hususan katika kipindi hiki cha janga la Corona.
Akifafanua zaidi, alisema hakuna anayejua janga hilo
litaisha lini hivyo ni lazima kuendeleza mapambano kwa kufanya kazi maana
Watanzania wangali wanahitaji umeme.
Hata hivyo, Waziri Kalemani alikagua miradi husika kwa
utaratibu tofauti na uliozoeleka ambapo haukuhusisha mikusanyiko ya wananchi
badala yake walioshiriki ni viongozi pekee wa ngazi za wilaya, kata, vijiji na
vitongoji.
Aliwataka wananchi kubaki majumbani na kwamba watapata
maelekezo ya Serikali kupitia kwa viongozi wao na katika vyombo vya habari.
“Nilitoa maelekezo kuwa katika kipindi hiki cha janga
la Corona, ziara zetu zitahusisha viongozi peke yake ili kuepusha mikusanyiko
ya watu, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo tuliyopatiwa na wataalamu wa afya
katika kujikinga na ugonjwa huu.
Katika ziara hiyo, Waziri aliagiza kusakwa na
kukamatwa Mkandarasi Emmanuel Nyigwa, anayedaiwa kuchukua pesa za wananchi kwa
makubaliano ya kufanya kazi ya kusuka mfumo wa nyaya za umeme (wiring) katika
nyumba zao lakini akatoweka pasipo kufanya kazi hiyo.
Aidha, kufuatia malalamiko hayo yaliyowasilishwa kwake
na Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu, Waziri alitoa maelekezo kwa
mameneja wote wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) nchi nzima, kuchukua
dhamana ya kuwasajili kwa kuwagongea muhuri wakandarasi wanaofaa kufanya kazi
ya kusuka mfumo wa nyaya katika majengo ili kuwaepusha wananchi na adha kama
hiyo iliyotokea.
Alisema uthibitisho huo wa Meneja husika utamaanisha
kuwa taarifa zote za Mkandarasi ikiwemo namba zake za simu na mahali anakoishi
zinafahamika na kurekodiwa ili kuwa na uhakika wa kumpata pindi anapokiuka
makubaliano.
Katika hatua nyingine, Waziri alikagua kazi
inayoendelea ya upanuzi wa Kituo cha kufua umeme cha Singida, ambayo ni sehemu
ya utekelezaji wa Mradi mkubwa wa umeme ujulikanao kama Backbone Transmission
Investment Project (BTIP) Awamu ya Pili.
Aliagiza kazi hiyo ikamilike ifikapo Julai mwaka huu
kama yalivyo makubaliano na kusisitiza kwamba kamwe Serikali haitaongeza muda
kwakuwa ilikwishafanya hivyo awali.
Waziri pia aliwasha umeme katika maeneo mbalimbali
ikiwemo vituo vya afya, sehemu za biashara na makazi ya wananchi katika vijiji
vya Nkuhi, Muungano, Matare na Mghamo katika Wilaya za Ikungi na Singida
Vijijini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi mbalimbali
akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Edward Mpogolo, Mbunge wa Singida Mashariki
Miraji Mtaturu na Mbunge wa Singida Kaskazini Justin Nonko, walipongeza
jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Wizara ya Nishati,
katika kuwapelekea wananchi huduma ya umeme hususan vijijini.
Waziri anatarajiwa kuhitimisha ziara yake mkoani humo,
Aprili 20, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment