Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) Mussa Azzan Zungu (mwenye kofia)
akiangalia athari za kimazingira zilizosababisha kukatika kwa
mawasiliano baada ya daraja la Mto Shaban Robert wilayani Mpwapwa mkoani
Dodoma kusombwa na maji.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) Mussa Azzan Zungu mwishoni mwa wiki
amefanya ziara ya kikazi wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma kukagua athari
zilizosababishwa na korongo kubwa kando ya Mto Shaban Robert.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo aliagiza Baraza la Taifa la
Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufanya tathmini ya haraka
kupata ufumbuzi wa tatizo hilo ili kunusuru wananchi kuzingirwa na maji
yanayojaa katika mto huo.
Waziri Zungu alisema pamoja na hayo Serikali kupitia Ofisi yake
imeichukua changamoto hiyo na kuahidi kukaa na wataalamu wa mazingira
kuanza utekelezaji wake.
”Athari hii sio ndogo ni kubwa na inahitaji uangalifu mkubwa katika kuitatua kwani
kila siku maji yanaongezeka katika mto huu, pia sisi kama Serikali tumetenga
fedha za kukabiliana na maafa kama kupitia mifuko ya kitaifa na ya kimataifa
hivyo tutazama tuone nini tunafanya,” alisema.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) Mussa Azzan Zungu akipewa maelekezo na
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma Jabir Shekimweri kuhusu namna
korongo lililopo katika Mto Shaban Robert linavyoathiri wakazi wa eneo
hilo wakati aliponya ziara ya kikazi wilayani humo.
Aidha Waziri Zungu aliwataka wananchi kuendelea kushiriki katika
suala zima la uhifadhi wa mazingira ikiwemo upandaji wa miti na
kuitunza ili kuepusha athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aliongeza kuwa shughuli za binadamu zinachangia kwa kiasi
kikubwa kwa matatizo hayo ambayo yamewaletea madhara ikiwemo kukatika
kwa mawasiliano baina ya eneo moja hadi lingine baada ya madaraja
kusombwa na maji ya mto yaliyofurika isivyo kawaida.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) Mussa Azzan Zungu (mwenye kofia)
akizungumza na wananchi wa Kata ya Mpwapwa Mjini alipofanya ziara ya
kikazi wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma kujionea na kusikiliza changamoto
za kimazingira zinazosababishwa na korongo lililopo kwenye Mto Shaban
Robert.
Pia waziri huyo aliwaahidi wananchi kuwasiliana na Wakala wa
Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dodoma kufahamu wana mkakati gani
katika kurudisha mawasiliano ya daraja lililosombwa na maji.
”Ombi langu kwenu muendele kulinda mazingira kwani tukiharibu mazingira
watoto wetu watateseka na dini zote zimesisitiza kulinda mazingira. Pia
tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu atunusuru na janga hili la Corona ili
Taifa letu liendelee na shughuli za kawaida na pia tuendelee kujikinga kama
wanavyoelekeza wataalamu wa afya”; alisisitiza.
Sehemu ya korongo kwenye mto
Shaban Robert wilayani Mpwapwa mkoania Dodoma ambalo limeleta athari kwa
wananchi wa eneo hilo pindi mvua inaponyesha na kusababisha maji
kuzingira makazi.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa Mhe. George Lubeleje
aliishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kutenga fedha
kiasi cha sh. bilioni 17.4 kwa ajili ya wilaya tano ikiwemo Mpwapwa
kutekeleza miradi ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mbunge huyo aliwaomba wananchi kuacha kufyeka na kuchoma miti
kwa ajili ya mkaa hususan katika maeneo ya milima kwa kuwa hatua hiyo
inasababisha kuharibiwa kwa vyanzo ya maji.
Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya
ya Mpwapwa, Emmanuel Lukumay aliahidi kuwa watafanyia kazi changamoto
hiyo kunusuru eneo la korongo kwa kutenga sh. milioni 457 kwa ajili ya
kujenga daraja la kudumu.
Sehemu ya nyumba za wakazi wa eneo
la Kata ya Mpwapwa Mjijni wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma ikiwa
imezingirwa na maji hatua liyosababisha baadhi ya nyumba kubomoka
kufuatia korongo lilipo katika Mto Shaban Robert.
Lukumay alibainisha kuwa daraja hilo lililojengwa zaidi ya miaka
60 iliyopita na kusombwa na maji hivi karibuni lilikuwa ni kiungo
muhimu kwa wananchi wa wilaya hiyo.
Aliongeza kuwa TARURA daraja liko chini ya mradi wa barabara ya
lami iliyoanza kujengwa katika wilaya hiyo na kusema kuwa tayari
wameomba fedha kwa ajili ya kulijenga.
No comments:
Post a Comment