Naibu Waziri wa Uchukuzi
na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amezindua safari za ndege za mizigo kwenye
Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA) kwa ajili ya kuwawezesha wafanyabiashara,
wakulima wa mazao, matunda na mboga mboga wa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha,
Tanga, Manyara na mikoa ya jirani kutumia usafiri huo kusafirisha mizigo yao
kwenda nje ya nchi ya Tanzania
Nditiye amesema kuwa
uzinduzi wa safari za ndege za mizigo ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe wakati akizindua bodi
ya Maendeleo ya Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro (KADCO) mwaka jana mwezi
Desemba
“Niwapongeze sana KADCO
kupitia Kaimu Mkurugenzi Mkuu wenu, Christopher Mukomu na kwa kushirikiana na Umoja
wa Wakulima wa Mboga Mboga na Maua Tanzania (TAHA), mmeweza na kuhakikisha ujio
wa ndege hii muhimu kwa ajili ya kusomba mizigo yetu hapa Tanzania, hilo kwangu
mimi ni kitu kikubwa sana kwa sababu kwa miaka mingi hatukuwa na huduma ya
mizigo kwa ndege kubwa kama hii, naipongeza sana Ethiopian Airline kwa utayari wao wa kushirikiana na Serikali na
kuamua kuleta ndege yao ya mizigo kuja kubeba mizigo,” amesema Nditiye
Pia, amekagua chumba cha
barafu cha kuhifadhi mizigo inayosafirishwa na ndege kwenda nje ya nchi ya
Tanzania na kujiridhisha kuwa chumba
hicho cha kisasa kimejengwa, kinafanya kazi vizuri na kina uwezo wa kubeba tani
110 na kina hali nzuri na amewaomba wadau mbali mbali kutumia huduma hii
kusafirisha mizigo yao badala ya kupitisha nchi za jirani
Ameilekeza Mamlaka ya Usafiri
wa Anga Tanzania (TCAA) kukaa na wadau wa usafirishaji wa mizigo hiyo ili
kuweza kutoa kibali cha muda mrefu cha wiki mbili au hata mwezi ili kuwawezesha
wasafirishaji kutumia vizuri fursa hii na amewataka wazingatie sheria, taratibu
na kanuni husika na siyo kutoa kibali tu, bali kutoa kibali cha kuhakikisha
kuwa biashara hii inakuwa endelevu na kuzingatia usalama
Nditiye ametoa maelekezo
hayo baada ya Afisa Mtendaji Mkuu wa TAHA, Dkt. Jacquline Mkindi kuiomba
Serikali kuweka mazingira wezeshi ya usafirishaji wa mizigo kwenda masoko ya
Ulaya ikiwa ni pamoja na ndege hizo kuja nchini kwa gharama nafuu kwa kupunguza
tozo mbali mbali kwa ndege kila inapotua, kuongeza muda wa kibali cha ndege na
kuwa na tozo tofauti baina ya ndege za mizigo na za abiria ili kuendelea
kuzivutia ndege hizo na ndege nyingine za mizigo kuja KIA na kutumia fursa hiyo
kuiwezesha sekta binafsi na wakulima wa mboga mboga na maua kufanya biashara
kwenye soko lolote duniani
Uzinduzi wa safari za
ndege za mizigo umehudhuriwa na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga ambapo
ameshuhudia wakulima wa mboga mboga na maua wa TAHA wakipakia mizigo ya bidhaa
zao kwenda nje ya nchi ambapo Nditiye na Hasunga wameshiriki kupakia mizigo
hiyo
Naye Mkuu wa Mkoa wa
Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema kuwa Serikali inatambua mchango wa sekta
binafsi na wakulima na lazima sekta binafsi ikuzwe a ilelewe kwa kupewa mashaerti
nafuu ya kufanya biashara zao na itaendelea kuunganisha mnyororo wa thamani kwa
kutumia viwanja vyake vya ndege na kununua ndege za mizigo kama ambavyo
Serikali imefanya kwa kununua ndege za abiria
Nditiye amefafanua kuwa
kwa muda mrefu ndege ya KLM imekuwa ikitumia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere uliopo Dar es Salaam kusafirisha mizigo kwenda nchi mbali mbali,
Serikali imeanza kujenga chumba cha barafu cha kuhifadhi mizigo kwenye uwanja
wa ndege wa Mbeya na katik mwaka wa fedha wa 2020/2021, Serikali kupitia Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imetenga fedha ya kununua ndege ya
kusafirisha mizigo
No comments:
Post a Comment